*Anafungua kesi kutaka ashitakiwe kwa mauaji
*Adai kuna mashahidi wanne muhimu walioachwa
*Ataiomba mahakama iwalinde mashahidi wake
*Mmiliki wa daladala aibuka na madai mengine
Na Kizitto Noya
WIKI chache baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, kuachiwa kwa dhamana, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, akisaidiwa na jopo la mawakili wanne, anakamilisha taratibu za kufungua kesi nyingine kuitaka mahakama imbadilishie kesi hiyo ili iwe ya mauaji ya kukusudia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mtikila alisema kesi hiyo inayotarajiwa kufunguliwa wiki hii, na akasema itafuatiwa na maandamamo makubwa ya kulaani mauaji hayo.
Alisema kesi hiyo mpya itasimama katika maelezo ya mashahidi wanne ambao katika kesi ya sasa, ushahidi wao haukusomwa mahakamani na akadai kuwa anaamini uliachwa kwa makusudi ili kumlinda mtuhumiwa.
Alisema ombi la kwanza atakalitoa kwa Mahakama Kuu katika kesi hiyo mpya ni kuitaka iwahakikishie ulinzi mashahidi wake.
“Kuua bila kukusudia ni kosa ndogo lisilokuwa na adhabu, ni vile tu jaji atakavyoridhika na kutoa hukumu isiyopungua miaka mitano wala kuzidi miaka saba,” alisema Mtikila na kuongeza;
"Lengo langu leo ni kuwaonyesha mashahidi wangu wa kesi hiyo mpya ili jamii iwajue na wanaotaka kuwadhuru ili wasitoe ushahidi washindwe…Wanasheria wangu pia wataiomba mahakama iwahakikishie ulinzi mashahidi hao kwani ushahidi wao ni nyeti."
Akiwa na baadhi ya mashahidi hao, Mtikila alidai watu walioandaa ushahidi wa kesi ya Ditopile, wameudanganya umma na Mahakama Kuu kwamba Ditopile aliua bila kukusadia wakati ushahidi ambao yeye anao ni kwamba ameua kwa kukusudia.
Alisema ushahidi huo ambao utatolewa na watu walioshuhudia tukio hilo kwa karibu zaidi, akiwamo mmiliki wa gari, ambaye siku hiyo alikuwa kondakta wa daladala iliyokuwa ikiendeshwa na marehemu Hassan Mbonde, haukufikishwa mahakamani, ingawa ulitolewa katika kituo cha polisi.
Alisema kesi hiyo itafunguliwa kulingana na ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayomtaka kila raia kuwa na wajibu wa kuilinda sheria za nchi zisipindishwe wala kutumika kwa maslahi ya binafsi ya watu.
“Kesi yetu itakuwa na sehemu mbili, kwanza kuitaka mahakama ibatilishe uamuzi wa awali kwamba kesi hiyo ni ya kuua bila kukusudia na pia ianze upya upepelezi wa kesi hiyo kupata ushahidi kuwa ni ya mauaji ya kukusudia,” alisema Mtikila.
Akizungumza katika mkutano huo, Thomas Mwita, mmliki na aliyekuwa kondakta wa daladala hilo siku ya tukio, aliwaambia waandishi wa habari kuwa siku ya tukio, kwa namna hali ilivyokuwa, Ditopile alimuua Mbonde kwa kukusudia.
“Mahakama ya Kisutu ilitakiwa kuwaita mashahidi wote kuja kuthibitisha maneno yao…lakini yenyewe imesikiliza ushahidi huo kwa maandishi na kujiridhisha kuwa ni kesi ya kuua bila kukusudia,” alisema Mtikila.
Ditopile alikamatwa Novemba mwaka jana kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa daladala katika makutano ya barabara ya Kawe. Aliwekwa rumande kwa zaidi ya miezi mitatu huku akisubiri upelelezi wakesi yake.
Hivi karibuni aliachiwa kwa dhamana baada ya Jaji wa Mahakama Kuu kuridhika kuwa kesi hiyo ni ya mauaji ya bila kukusudia.