Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kila la kheri uchaguzi mdogo Tunduru
Kila la kheri uchaguzi mdogo Tunduru
By Habari Tanzania | Published  03/18/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

HATIMAYE uchaguzi mdogo katika Jimbo la Tunduru kujaza nafasi ya ubunge iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Juma Jamaldin Akukweti, unafanyika leo.

Uchaguzi huo unafanyika huku hali ya mambo ikionyesha kuwapo kwa mchuano mkali kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Wakati vyama hivyo viwili kila kimoja kikitamba kuchukua kiti hicho, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chenye mgombea Shaibu Akwilombe, ambacho hivi sasa kimepeleka makada wake kadhaa maarufu wakiongozwa na timu ya wabunge wake, nacho kimekuwa kikitamba kunyakua kiti hicho katika mazingira ambayo kimeyaeleza kuwa yatawashangaza viongozi wa CCM na CUF.

Majemedari wa kampeni wa CCM, iliyomsimamisha Mtutura Abdallah Mtutura, Makamu Mwenyekiti wake, John Malecela na Katibu Mkuu wake, Yussuf Makamba katika mikutano kadhaa ya kampeni wiki hii, wamekuwa wakieleza bayana uhakika wa kuendelea kukikalia kiti hicho, pamoja na kuwapo kwa kelele nyingi kutoka kwa wafuasi wa CUF wanaoungwa mkono na wenzake wa vyama vya NCCR-Mageuzi na Tanzania Labour (TLP).

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anafika mbali zaidi, akitamba kuwa, mgombea wa CUF, Mazee Rajab Mzee, ataibuka na ushindi kwa asilimia 85 kutokana na tathmini iliyofanywa na CUF katika kipindi chote cha kampeni.

Anatoa tambo hizo ilhali akiungana na vyama vingine kulalamikia kile kinachodaiwa kuwa ni rafu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wapinzani wanadai kwamba, NEC imeshindwa kuwapatia vifaa vya kura, na badala yake wamepewa taarifa za mdomo tu jinsi uchaguzi huo utakavyoendeshwa.

Kilio cha wapinzani hao ni mwendelezo wa vituko ambavyo vimekuwa vikitokea tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo.

Tunadhani, kama hatimaye vyama vyote vimeingia salama katika siku ya mwisho ya uchaguzi, ni vyema busara zikatumika kuhakikisha kwamba, uchaguzi unamalizika salama.

Si busara kwa viongozi wa vyama vinavyochuana tu, bali hata kwa NEC ambayo imedaiwa kukiuka taratibu kadhaa za uchaguzi.

Tunaamini dosari ndogo zilizojitokeza zinaweza kurekebishwa haraka, na hivyo kuondoa manung’uniko kutoka kwa vyama na wafuasi wa wagombea waliotumbukiza kete zao katika kuwania kiti kilichoachwa na hayati Akukweti.

Hili likifanikiwa, tuna uhakika wa kushuhudia mshindi akitangazwa na Watanzania kuingia katika ngwe nyingine ya kutafuta mikakati ya kuhakikisha nchi inasonga mbele.

Hatutarajii kusikia uchaguzi huo ukigeuzwa jukwaa jipya la mjadala, huku akipinga lile na yule akipinga hili, eti tu kwa sababu ya kutoridhishwa na mchakato wa uchaguzi.

Lengo letu ni kuona hata baada ya uchaguzi huo, amani, upendo na mshikamano unakuwepo baina ya Wanatunduru na hata baina ya vyama vya siasa na wafuasi wao.

Ndiyo maana tunasema; kila la kheri uchaguzi mdogo Tunduru.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.