CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kwamba baadhi ya vyama vimewafanyia ‘usanii’, baada ya kujua hakuna watakachopoteza kwa kumpigia debe mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Mazee Mzee katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Tunduru utakaofanyika leo.
Mgombea wa nafasi ya ubunge wa jimbo hilo kupitia CHADEMA, Shaibu Akwilombe, alisema mwaka 2005, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema na Sengondo Mvungi wa NCCR-Mageuzi, hawakupata kitu Tunduru, katika harakati zao za kuusaka urais.
Alisema kwamba, anashangazwa kuona sasa wamerejea kwa nguvu jimboni humo wakimpigia debe mgombea wa CUF, katika kampeni za uchaguzi mdogo.
Akwilombe ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema kwamba, wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, TLP haikuwa na tawi hata moja jimboni humo, na NCCR nayo haikuwa na wanachama na inashangaza kuona sasa wanaungana.
Alihoji: “Muungano huo ni wa nini iwapo vyama hivyo havina wanachama wala matawi?”
Kauli hiyo ya Akwilombe inafuatia uamuzi wa viongozi wa NCCR-Mageuzi na TLP kupiga kambi jimboni humo wakiisaidia CUF kumnadi mgombea wake katika uchaguzi huo.
“Jamaa wamekuja kuhutubia kwenye sherehe za watu, hakuna muungano hapo, ni usanii tu,” alisema Akwilombe.
Alisema madhumuni ya kuanzishwa kwa vyama vingi ni kutoa nafasi kwa wagombea wengi zaidi kushiriki ili wananchi wapate nafasi pana ya kuchagua mtu wanayemtaka, hivyo, alisema kuunganisha vyama ni kuminya haki hiyo.
“Lazima watu wapewe nafasi kuchagua chama chenye sera wanazoona zinawafaa, sio kukimbilia kuungana, huo ndio mwanzo wa kuua vyama,” alionya Akwilombe na kuhoji: “Ni uchaguzi upi CUF iliwahi kuunga mkono vyama vingine?”
Pamoja na kuvilalamikia vyama hivyo, karibu wabunge wote wa CHADEMA wapo jimboni humu kwa wiki kadhaa sasa, wakiwa wamegawana kata za kumfanyia kampeni Akwilombe ambaye amejitosa katika kinyang’anyiro hicho.