Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kiwingu Tunduru
Kiwingu Tunduru
By Habari Tanzania | Published  03/18/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Charles Mullinda, Tunduru

UCHAGUZI mdogo katika Jimbo la Tunduru kujaza nafasi ya ubunge iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Juma Jamaldin Akukweti, unafanyika leo wakati hali ya mambo ikionyesha kuwapo kwa mchuano mkali kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Wakati vyama hivyo viwili, kila kimoja kikitamba kuchukua kiti hicho, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho hivi sasa kimepeleka makada wake kadhaa maarufu, wakiongozwa na timu ya wabunge wake, nacho kimekuwa kikitamba kunyakua kiti hicho katika mazingira ambayo kimeyaeleza kuwa, yatawashangaza viongozi wa CCM na CUF.

Majemedari wa kampeni wa CCM, Makamu Mwenyekiti wake, John Malecela na Katibu Mkuu wake, Yussuf Makamba, katika mikutano kadhaa ya kampeni wiki hii, wamekuwa wakieleza bayana uhakika wa kuendelea kukikalia kiti hicho, pamoja na kuwapo kwa kelele nyingi kutoka kwa wafuasi wa CUF, wanaoungwa mkono na wenzake wa vyama vya NCCR-Mageuzi na Tanzania Labour (TLP).

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyeambatana na Mwenyekiti wa Chama wa TLP, Augustine Mrema na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alitamba kuwa, mgombea wa CUF, Mazee Rajab, ataibuka na ushindi kwa asilimia 85 kutokana na tathmini iliyofanywa na CUF katika kipindi chote cha kampeni.

“Tuna uhakika wa ushindi asilimia 85, lakini hatuna imani na matokeo yatakayotangazwa na tume. Kabla ya kuja Tunduru nilikuwa nadhani tutashinda kwa asilimia 70, lakini baada ya kupita vijijini nimeridhika na ushindi ni zaidi ya asilimia hiyo.

“Vijijini CUF inakubalika sana, wanaimba hata wimbo wa taifa wa CUF bila wasiwasi, tatizo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vya dola.

“Kuna kura za uchina china (za wizi) zinashughulikiwa na maboksi zaidi ya 100 yanaandaliwa, tunawaonya hatutaki yatokee ya Zimbabwe hapa Tunduru. Nimemwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ahakikishe vyombo vya dola havitumiki vibaya,” alisema Lipumba.

Pamoja na kutamba kutwaa ushindi, Lipumba ameungana na vyama vingine vya upinzani kulalamikia kile walichodai kuwa ni ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Katika madai yao hayo, walidai kuwa NEC imeshindwa kuwapatia vifaa mbalimbali vitakavyotumika leo wakati wa upigaji kura na badala yake wamepewa taarifa za mdomo tu jinsi uchaguzi huo utakavyoendeshwa.

Aidha, wameilalamikia CCM iliyomsimamisha mgombea, Mtutura Abdallah Mtutura, kwa kuandaa mbinu chafu za kujihakikishia ushindi, lakini wakaonya kuwa, iwapo chama hicho tawala kitathubutu kufanya hivyo, watajibu mapigo.

Wakijinadi katika nyakati tofauti siku ya mwisho ya kampeni jana, wagombea na viongozi kutoka kambi ya upinzani, walidai kuwa wana uhakika kuwa kambi yao itaibuka na ushindi kutokana na maandalizi waliyoyafanya na ukweli kwamba CCM iliyojaza viongozi wake wakuu wakiwamo Makamu Mwenyekiti, John Malecela na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, haikubaliki miongoni mwa wananchi jimboni humu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari juzi jioni, viongozi hao walisema iwapo uchaguzi utakuwa wa huru na haki, CCM itapata aibu kubwa ambayo ni ya kwanza tangu kilipoanzishwa.

Lipumba, aliwaambia waandishi wa habari kwenye ofisi za CUF kuwa, NEC haijaonyesha wagombea vifaa vitakavyotumika kupigia kura, na sehemu vitakakopelekwa, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za uchaguzi.

Alisema badala yake, NEC imewapiga marufuku viongozi wa upinzani kupita katika vituo vya kupigia kura na kuangalia mwenendo wa upigaji kura, jambo ambalo limekuwa likifanywa katika chaguzi mbalimbali zilizopita.

Naye mgombea wa CHADEMA, Shaibu Akwilombe, aliilaumu NEC kwa kutowashirikisha wagombea wa upinzani na wasaidizi wao katika maandalizi ya uchaguzi huo.

Alisema NEC inafanya kazi zake kama uchaguzi ni mali yake na wagombea hawahusiki na uchaguzi huo. Hata hivyo, alitamba kuwa ana uhakika na ushindi kutokana na kampeni alizofanya pamoja na timu ya wataalamu wake kuwafikia wapiga kura.

Alisema ana uhakika wa kushinda kwa kati ya asilimia 46 na 48 iwapo kura zake hazitaporwa na vyama vingine.

“Nimeridhika na mwitikio wa watu ingawa nilitatizwa na kutowafikia wapiga kura kutokana na ubovu wa barabara na mvua zinazonyesha, timu yetu ya kampeni imefanya kazi kitaalamu na imefanya tathmini na kubaini ushindi wangu utakuwa ni wa asilimia 46 na 48 kulingana na idadi ya wapiga kura,” alisema Akwilombe.

Aidha, alisema kuwa CHADEMA inafahamu kuwa CCM haiwezi kushinda iwapo uchaguzi huo utakuwa huru na haki ndio maana (CCM) wanatumia hila, lakini wao (CHADEMA) wameandaa wakala wao kuwadhibiti wana CCM watakaojaribu kuiba kura.

Mrema alisema kuwa, tathmini aliyoifanya inaonyesha kuwa CCM itapata aibu kubwa na kushindwa vibaya tangu kuanzishwa kwake.

Mrema aliyewasili hapa siku kadhaa zilizopita akiipigia debe CUF, alisema dalili zote zinaonyesha kwamba CCM watatumia hila kushinda, lakini alionya dhidi ya hila hizo akisema kuwa wapinzani watachukua hatua kali.

“Biashara ya jumla tumeshindwa… ya rejareja lazima tutashinda… kama serikali imesalimu amri kwa wafungwa, isicheze na wananchi wa Tunduru,” alisema Mrema.

Alisema CCM wanajua kuwa wameshashindwa Tunduru, lakini kwa sababu vyombo vya dola vyote vipo chini yake, lolote linaweza kutokea.

Naye alisema CCM inaogopa ushindani wa kweli na ikibaini sehemu yenye ushindani wa kweli inaheshimu na kutoa huduma zote muhimu.

Mbatia alisema amefurahishwa na uasi wa wana Tunduru kwa CCM na akawataka wasitishwe na idadi kubwa ya polisi walioletwa wilayani hapa wakati huu wa uchaguzi.

Msimamizi wa uchaguzi huo alipotafutwa jana ili atoe ufafanuzi kuhusu madai hayo, hakupatikana na ilielezwa kuwa alikuwa akihudhuria mkutano muhimu.

Uchaguzi mdogo wa Tunduru unafanyika kufuatia kifo cha Akukweti aliyefariki dunia Januari 3 mwaka huu huko Afrika Kusini alikopelekwa kwa matibabu zaidi ya majeraha ya moto aliyoyapata katika ajali ya ndege iliyotokea Desemba 16 mjini Mbeya alikokwenda kukagua athari za ajali ya moto katika soko la Mwanjelwa.

Ajali ya Mbeya pia iligharimu maisha ya watu wengine waliofuatana na Akukweti, akiwamo mwanahabari Teddy Nyantori wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Nathaniel Katimila aliyekuwa, Ofisa wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Mwingine ni ofisa kutoka kitengo cha maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu, George Bendera.

Rubani wa ndege hiyo aina ya Cessna, Martin Sumari na Nisetus Kaje aliyekuwa msaidizi wa Akukweti, wamesalimika kifo, lakini baada ya kulazwa kwa siku kadhaa wakitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako pia Akukweti alilazwa kabla ya kukimbizwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi Desemba 27.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.