Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Hivi hizo takwimu za uchumi zinatoka wapi?
Hivi hizo takwimu za uchumi zinatoka wapi?
By Habari Tanzania | Published  03/17/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

ZANZIBAR imekumbwa na mvutano mkubwa wa hoja, baada ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani Abeid Karume, kutangaza kukua kwa uchumi visiwani humo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Karume katika taarifa yake hiyo ya uchumi aliyoitoa hivi karibuni, alisema katika kipindi hicho kiwango cha umasikini Zanzibar kimepungua kutoka asilimia 60 hadi 49.

Rais huyo aliyekuwa akizindua Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) alisema pia kwamba, hali hiyo imetokana na kukua kwa uchumi.

Hakuishia hapo, alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa, uchumi wa Zanzibar umekua hadi kufikika asilimia 6.8 mwaka 2005 kutoka asilimia 5.6 ilivyokuwa mwaka 2002.

Hoja hizo za Karume zilipokewa kwa hisia tofauti na viongozi wengine wa kisiasa kutoka kambi ya upinzani, ambao wote kwa nyakati tofauti walieleza kushtushwa na takwimu hizo.

Katibu Mkuu wa TADEA, Juma Ali Khatib, yeye alizielezea takwimu hizo za Karume kuwa ni kejeli kwa Wazanzibari, hasa wale wa kipato cha chini, ambao wanakabiliwa na ugumu wa maisha kutokana na kudorora kwa uchumi.

Kiongozi huyo aliwalaumu watalaamu wa uchumi Zanzibar kwa kuwahadaaa wananchi kuhusu hali ya uchumi na umasikini, wakati ukweli ukionyesha kuwa hali ya kimaisha ya wananchi ni mbaya.

Alisema sekta ya biashara, inayotegemewa na watu wengi Zanzibar, imeanguka kwa kiasi kikubwa na kusababisha mzunguko wa fedha kuyumba.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani, alikuwa na maoni kama hayo yanayofanana na kiongozi wa TADEA.
Bimani yeye alisema chama chake kilikuwa kimeshtushwa na takwimu hizo zinazoonyesha mafanikio wakati katika hali halisi, maisha yanapopimwa na vigezo vya huduma za jamii yanaonekana kudorora.

Kiongozi huyo wa CUF alisema kwamba, watu wanaomudu huduma za jamii ni wale wenye uwezo, wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na baadhi ya wafanyabiashara.

Akitoa mfano alisema katika kipindi hiki cha sasa, idadi ya ombaomba wakiwamo vijana, imeongezeka sana tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Kama hiyo haitoshi, Bimani alisema sekta ya viwanda, ambayo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa lolote, imedorora hali ambayo ni ushahidi mwingine wa kudorora kwa uchumi.

Maoni kama hayo pia yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Hamad Mussa Yussuf, ambaye alisema vigezo vinavyotumika katika kupima ukuaji uchumi Zanzibar vina utata mkubwa.

Alisema kikubwa katika matangazo hayo ni ukweli kwamba, takwimu hizo zinakwenda kinyume cha hali halisi ya maisha ya kawaida.

Mabishano hayo ya hoja kati ya serikali kwa upande mmoja na wadau wengine kwa upande mwengine si ya kwanza katika historia ya taifa hili katika miaka ya hivi karibuni.

Wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa takwimu kama hizo zilizotolewa na Karume, mara kadhaa zilikuwa zikisababisha mvutano mkubwa wa hoja kati ya wananchi na serikali yao.

Kimsingi mwenendo huu wa mambo umekuwa ukiwashangaza watu wengi na kusababisha maswali mengi, kubwa kati ya maswali hayo likiwa ni lile liulizalo, hivi vigezo vya uchumi vinavyotoa takwimu hizo hufanya hivyo kwa kuzingatia hali halisi ya maisha?

Mara nyingi jibu lake huwa ni hapana. Kwa sababu hiyo basi, na sisi tunapenda kuungana na viongozi hao wanaopingana na takwimu hizo za Karume, ambazo kwa kiwango kikubwa zimekuwa hazielezi kwa uhakika kabisa hali halisi ya maisha. Tunapaswa kutafuta kipimo kingine cha uchumi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.