ZIARA ya siku moja aliyoifanya Rais Jakaya Kikwete nchini Zimbabwe juzi, inaonekana kuzaa matunda kwani Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo, ameonyesha kulegeza msimamo katika msuguano na nchi za Magharibi.
Wakati wa ziara hiyo, Mugabe si tu alikiri kuwa hali ya uchumi wa nchi hiyo imefika pabaya, bali pia alikubali kushirikiana na Kikwete kutatua matatizo ya kiuchumi na kisiasa yanayoikabili nchi hiyo.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi kuhusu ziara hiyo.
“Rais wetu amefanya mazungumzo na Rais Mugabe na wamekubaliana kutatua matatizo ya kiuchumi na kisiasa yanayoikabili nchi hiyo na kusababisha maendeleo ya kiuchumi kupungua,” alisema Membe.
Alisema katika ziara hiyo Kikwete alimwelezea Mugabe kuhusu msimamo wa nchi za Ulaya ambazo amezitembelea hivi karibuni.
Aidha, Membe alisema Mugabe naye alitumia fursa hiyo kumweleza Kikwete hali halisi nchini Zimbabwe, hasa kuhusu tukio la Machi 12, mwaka huu lililohusisha kupigwa na polisi kwa wafuasi na viongozi wa vyama vya upinzani na kusababisha mfuasi mmoja wa chama cha MDC kupoteza maisha.
Alisem a uchumi wa Zimbabwe hadi hivi sasa si mzuri kutokana na mgomo huo na kumekuwepo na mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 1700 hali ambayo inazidi kufanya maendeleo ya nchi hiyo kupungua.
“Nchi ya Zimbabwe inahitaji mazungumzo iweze kuwa na muafaka katika uchumi na siasa ili nayo ipige hatua katika maendeleo,” alisema Membe.
Akitoa mfano, Membe alisema kuwa licha ya kuwa maskini, Tanzania imepiga hatua katika maendeleo, na inawajibika kuisaidia Zimbabwe ili iondokane na migogoro iweze kujenga uchumi wake.
Membe alisema katika ziara yake ya hivi karibuni katika nchi kadhaa za Ulaya, Kikwete alijifanya balozi wa nchi hiyo na kuwaelezea viongozi wa nchi hizo kuwa iwapo wataendelea kuitenga Zimbabwe, nchi za Afrika nazo zinaweza kususa kuhudhuria mikutano inayoandaliwa na nchi hizo kama njia ya kuonyesha mshikamano.
Katika hatua nyingine, amesema kutakuwa na mkutano baadaye mwezi huu jijini Dar es Salaam kuzungumzia muafaka wa nchi hiyo.