Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mahakama: Uchaguzi Tunduru utaendelea
Mahakama: Uchaguzi Tunduru utaendelea
By Habari Tanzania | Published  03/17/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Happiness Katabazi na Lucy Ngowi

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imetupilia mbali ombi la Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, la kutaka uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Tunduru mkoani Ruvuma, usimamishwe.

Katika ombi hilo, Mtikila aliiomba mahakama isitishe maandalizi ya uchaguzi huo kwa kuwa unakwenda kinyume cha katiba na maamuzi ya Mahakama Kuu.

Ombi hilo lilisikilizwa na kutolewa maamuzi na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Othman Chande, akisaidiwa na Amir Mruma na Robert Makaramba.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Chande, alisema umezingatia kigezo cha uwiano wa yupi kati ya mlalamikaji na mdaiwa, ambaye ni serikali, ataathirika zaidi.

Jaji Chande alisema, hadi sasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekwishatumia sh 243,126,860, kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi huo na wananchi 118,000 wa Tunduru wapo tayari kupiga kura.

Alisema idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na idadi ya watu 11,552 ambao watakosa haki yao ya kupiga kura kama ilivyoelezwa na Mtikila.

Aidha, alisema kuwa, watu watano wanaogombea ubunge katika jimbo hilo, hawakushirikishwa kwenye ombi hilo.

“Idadi ya wanaotaka kupiga kura ni kubwa na kwenye ombi hili wagombea watano hawakushirikishwa… hivyo mahakama imeona si busara kutoa maamuzi ambayo yatawaathiri hao ambao ni wengi na pia hawakushirikishwa kwenye kesi hii,” alisema Jaji Chande.

Hata hivyo, jopo hilo lilikubaliana na hoja kadhaa zilizotolewa na wakili wa mlalamikaji, Mpale Mpoki, kwamba watu ambao wamenyimwa fursa ya kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi huo, wamenyimwa haki yao kikatiba.

Wakati huo huo, Mpoki alisema amepokea uamuzi huo kama ulivyotoka kwa kuwa misingi na hoja zote alizozitoa hazijakataliwa na jopo hilo na ana imani kwamba, atafanya vizuri kwenye kesi ya msingi itakayoanza kusikilizwa Mei 17 mwaka huu, mbele ya jopo hilo.

Katika hatua nyingine, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ameunga mkono kuwepo kwa mgombea binafsi, hoja inayopigiwa upatu na Mtikila.
Akitoa mada katika kongamano la amani jijini Dar es Salaam jana, Tendwa alisema kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, kutaondoa migogoro na migongano isiyokuwa ya lazima katika nchi.

Alisema baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza kuimarika na kueleweka zaidi miongoni mwa Watanzania, jambo la msingi la kufanya hivi sasa ni kupanua demokrasia zaidi.

Alisema hali hiyo itaepusha migogoro na kusaidia katika kutunza na kulinda amani na utulivu nchini.

Tendwa alisema, kwa upande wake, anaamini kuwa mfumo wa vyama vingi umeleta neema kubwa nchini, ingawa hakuna kitu kisichokuwa na upande wa pili, yaani mabaya.

Aliainisha faida za mfumo wa vyama vingi hapa nchini kuwa ni pamoja na kupanua wigo wa demokrasia na pia kuifanya serikali na chama tawala kuwa makini zaidi katika utekelezaji wa sera na majukumu yake kwa wananchi.

“Vyama vya siasa ambavyo havipo kwenye serikali, kazi yake ni kuchambua, kukosoa, kutoa maoni mbadala kuhusu serikali na chama tawala vinavyotekeleza sera na majukumu yao. Wakati wa chama kimoja watu walikuwa na mawazo na itikadi zao tofauti rohoni, wakiogopa kuzisema hadharani,” alisema Tendwa.

Alisema vyama ambavyo havipo katika serikali, vinasaidia sana kukifanya chama tawala kisilale kwa kuogopa kila siku kupoteza imani na kura za wananchi katika chaguzi mbalimbali ambazo zote huhusisha vyama vingi vya siasa.

Alisema pamoja na faida hizo, pia kuna matatizo yaliyojitokeza ndani ya mfumo wa vyama vingi, ikiwa ni pamoja na taasisi nyingi za kiserikali kutovikubali vyama visivyo ndani ya serikali na hivyo kuvikebehi.

“Sehemu ambapo vyama hivi vya siasa vya upinzani vimeimarika, huduma muhimu zilizorota. Hata hivyo juhudi mbalimbali zimefanywa na taasisi mbalimbali za kiserikali na za kibinafsi ili kuyaondoa matatizo yaliyojitokeza,” alisema Tendwa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.