Rais Jakaya Kikwete amesema changamoto kubwa kwa taifa sasa nikuandaa sera ambayo itakabiliana na tatizo la matokeo ya ukame pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta.
Alisema kwa sasa matatizo ya ukame na kupanda kwa bei kubwa ya mafuta yamekuwa yakiathiri kukua kwa uchumi katika pato la nchi na kusababisha mfumuko wa bei.
Rais Kikwete alisema hayo katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia Rais wa Ireland, Bi. Mary McAleese, Ikulu Jijini Dar es Salaam juzi.
Dhifa hiyo ilihudhuriwa pia na Marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa, mawaziri, viongozi mbalimbali wa serikali na mabalozi wanaofanyakazi nchini.
Alisema atahakikisha kwamba Serikali na taasisi zake zinaboresha utendaji wa kazi zake na kujenga uchumi imara unaokua haraka.
Akizungumzia suala la Mpango wa Kuondoa Umaskini na Kukuza Uchumi nchini (MKUKUTA), Rais Kikwete alisema nguvu kubwa inaelekezwa katika kuboresha kilimo, mifugo na uvuvi.
Aliishukuru serikali ya Ireland kwa misaada yake katika sekta hiyo ambayo alisema ni uti wa mgogo wa uchumi wa nchi.
Katika dhifa hiyo, Rais Kikwete alimhakikishia Rais huyo wa Ireland, kuwa serikali yake itakuwa makini katika kutumia misaada inayotolewa na wahisani.
Alisema anaamini kuwa ziara ya Rais McAleese nchini, inaweza kutoa nafasi ya kuongeza biashara na uwekezaji wa moja kwa moja kati ya nchi mbili hizo.
Rais McAleese ambaye amefuatana na mume wake, Dk. Martin McAleese yupo nchini kwa ziara ya siku tano.