Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tujitokeze kukisaidia Chuo Kikuu Mzumbe
Tujitokeze kukisaidia Chuo Kikuu Mzumbe
By Habari Tanzania | Published  03/16/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

LEO, Waziri Mkuu Edward Lowassa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya elimu ya kukichangia Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Harambee hiyo itakayofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, inalenga kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanafunzi wanawake, hatua ambayo itaongeza udahili wa wanachuo wa kike.

Taarifa ya chuo hicho inaonyesha kwamba lengo lao ni kuhakikisha idadi ya wanafunzi wa kike inakuwa nusu ya wale wa kiume ifikapo mwaka ujao wa masomo (2007/08).

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Moses Warioba, malengo hayo ya kuongeza uwiano kijinsia katika udahili yanakwenda sanjari na Sera ya Kijinsia ya Chuo Kikuu cha Mzumbe ya mwaka 2004 na ile ya Taifa ya Elimu ya Juu ya mwaka 1995.

Katika kuonyesha namna walivyojipanga kutimiza azima hiyo, Profesa Warioba alisema mkakati wao wa kuongeza udahili umeshaonyesha mafanikio katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kumekuwapo ongezeko la idadi ya wanachuo wa kike wanaodahiliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe katika miaka mitatu iliyopita.

Akitoa mfano, alisema asilimia 23 ya wanachuo wote waliojiunga na chuo hicho mwaka wa masomo 2002/03, walikuwa wa kike na mwaka uliofuata idadi hiyo ilipanda hadi kufikia asilimia 30.7, na hatimaye mwaka 2004/05 wakafikia asilimia 35, kabla ya kuhitimisha na kugota asilimia 40 mwaka jana - 2005/06.

Hata hivyo, makamu mkuu huyo wa chuo alisema wamelazimika kuitisha harambee hiyo baada ya kubaini kuwa, lengo lao la kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike linaweza kukwamishwa na uwezo mdogo kifedha walionao.

Kwa sababu hiyo basi, kwa kutambua umuhimu wa hilo, chuo hicho kimeamua kuchangia wajibu wa serikali wa kuongeza majengo na rasilimali nyingine kwa kuanzisha mradi maalumu unaokadiriwa kugharimu shilingi milioni 600, ambao ndio utakaofanikisha azima yao hiyo.

Sisi tunapenda kukipongeza chuo hicho kwa dhati kabisa kwa namna kilivyoweza kufanikisha azima yake hiyo ya kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike wanaodahiliwa chuoni hapo katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo iliyopita.

Tunaamini pia kwamba, uamuzi huo wa kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike, haufanywi kwa sababu tu ya kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike, bali hufanywa kwa kuangalia sifa za kitaaluma za wanafunzi hao wanaodahiliwa.

Tunasema hivyo tukitambua kuwapo kwa haja ya lazima ya kuhakikisha kuwa, ongezeko hilo la wanawake linafaa kwenda sambamba na kuangaliwa kwa uwezo wa kitaaluma wa wanafunzi hao, ili kukihakikishia chuo kuwa idadi ya wanaodahiliwa ndiyo ile ile inayohitimu masomo katika kipindi cha miaka mitatu.

Wakati tukikipongeza chuo hicho, tunapenda kuwahamasisha wananchi wa kada mbalimbali wanaotambua umuhimu mkubwa wa elimu ya juu kwa wakati huu kujitokeza kwa wingi kukichangia chuo hicho ambacho kwa miaka nenda – rudi, kimekuwa moja ya vyuo vya mfano hapa nchini.

Tunasema hivyo tukitambua kuwa, mahitaji ya watu wenye elimu ya juu wakati huu wa utandawazi ni makubwa na kwamba nchi yetu inapaswa kuhakikisha ikijizatiti vyema kiushindani, kitaaluma dhidi ya majirani zetu ambao wana vyuo vingi vya juu kuliko sisi.

Tunaamini kwamba, tukijitokeza kwa wingi kukichangia chuo hicho, tutakuwa tumepiga hatua kubwa ya ukombozi wa kielimu wa mwanamke, ambaye tunaelezwa na wahenga kwamba, kumuelimisha mwanamke mmoja ni sawa na kuelimisha taifa zima.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.