JUMUIYA ya kimataifa imesema kuanzishwa kwa mazungumzo yanayolenga kuleta maelewano ya kisiasa na kijamii Zanzibar kutasaidia juhudi za kujenga uchumi zinazoendelea.
Hayo yameelezwa jana na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Iscar Fernandez Taranco, katika hotuba aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA).
Alisema maelewano baina ya wananchi ni muhimu ili mpango wa kupunguza umaskini ufanikiwe.
“Washirika wa maendeleo tunaunga mkono juhudi za serikali kufungua mazungumzo kisiasa, kijamii na kiuchumi ili wananchi wote waweze kushirikishwa na kupata huduma kwa usawa,” alisema Taranco.
Alieleza kwamba hali hiyo pia itachangia Zanzibar kuwa na utulivu na hivyo kupata urahisi katika kukuza maendeleo yake.
Taranco alisema kwamba mazungumzo yanayoendelea yataleta faida kubwa na ndiyo njia muafaka ya kuharakisha maendeleo katika visiwa hivyo.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo katika mazungumzo na Chama cha Wananchi (CUF) yanayolenga kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar, baada ya chama hicho cha upinzani kutangaza kutoitambua Serikali ya Zanzibar.
“Changamoto zinazoukabili MKUZA ni kuondoa kasoro zinazojitokeza katika utekelezaji wake,” alisisitiza.
Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kutopatikana kwa takwimu sahihi katika ngazi mbali mbali za serikali, ambazo ndizo zinazowezesha kuchukuliwa maamuzi sahihi ya utekelezaji wa mipango mbali mbali.
Alisema jmuiya ya kimataifa itaendelea kuunga mkono juhudi za kupunguza umaskini zinazoendelea na kusifu hatua ya ushirikishwaji wa jumuiya za kiraia na sekta binafsi katika uetekelezaji wa MKUZA.
Akihutubia katika uzinduzi huo, Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume alisema miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa MKUZA ni pamoja na kupunguza idadi ya watu waliokuwa wakiishi katika kiwango kikubwa cha umaskini.
Alisema kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 60 hadi 49 ilipofika 2005, tangu kuanza kwa mpango huo mwaka 2002.