Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Iddi Simba: Watanzania bado wamelewa ujamaa
Iddi Simba: Watanzania bado wamelewa ujamaa
By Habari Tanzania | Published  03/16/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Saada Said

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mtetezi mkubwa wa sera ya uzawa, Iddi Simba, ameibukia Zanzibar na kulaumu maamuzi yaliyofanywa na viongozi waliobadili mfumo wa uchumi, yaliyofanywa zaidi ya miaka 20 iliyopita, kutoka ujamaa kwenda ubepari.

Akizungumza katika semina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Simba alisema viongozi hao walifanya makosa makubwa kwa kutowashirikisha wananchi katika mchakato wa kubadili sera hizo.

“Njia kuu za uchumi wa Tanzania, zilizokuwa zinamilikiwa na wananchi wazalendo kupitia sekta ya umma inayofahamika, zilihamishwa kwenda sekta binafsi ambayo mwelekeo wake mpaka sasa hado haujaeleweka,” alisema.

Alisema kwamba kosa kubwa lililofanywa na uongozi wa kisiasa wakati huo ni kubadilisha mfumo wa kiuchumi ulioitwa ‘ujamaa’ na kuingia katika mfumo wa ‘kibepari’ bila ya wananchi kupewa nafasi na muda wa kuuelewa mfumo huo.

Alisema chini ya mfumo wa ujamaa, Watanzania hawakulelewa katika mfumo wa ujasiriamali binafsi na badala yake walifundishwa na kuzoeshwa kudharau na hata kuchukia ujasiriamali binafsi, na hadi sasa akili na mwelekeo wa baadhi ya watu haujabadilika bado.

Simba alibainisha kuwa kuna hatari zaidi mbele kwa sababu kutokana na sababu za kihistoria, imekuwa taabu mno kutenganisha hata nafasi ya mihimili mikuu ya nchi kama Bunge na Serikali.

“Bunge ambalo lina madaraka ya kutunga sheria na kudhibiti mwenendo wa serikali, mpaka hivi sasa halina uhuru kamili wa kufanya kazi zake bila ya ridhaa ya serikali. Bajeti ya Bunge inakadiriwa na serikali, na wafanyakazi wa Bunge ni watumishi wa serikali na wanawajibika huko. Hali hii ikichanganywa na maovu mengi yaliyoikumba jamii, inavuruga misingi ya utawala bora,” alisema Simba.

Kwa sababu hizo, Simba aliionya na kuitaka Tanzania kutoharakisha kujiunga na Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu za kisiasa, akifananisha shirikisho kilo na ndoa changa.

Alisema ndoa ina misukosuko mingi, na Tanzania imechelewa kuwaandaa wananchi, na endapo suala hilo litaharakishwa, kuna hatari ya ndoa hiyo kufungwa kabla haijabalehe.

“Zoezi la kuwaandaa wananchi wetu lilistahili kufanywa zaidi ya miaka 20 iliyopita. Tumechelewa mno na tukiharakisha sana maandalizi haya, tutaoana kabla ya kubalehe. Misukosuko ya ndoa katika hali hiyo itatupa taabu sana,” alisema.

Alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya jinsi ya kuwaandaa wananchi waweze kujiunga katika mkondo wa uchumi wa kisasa.

Kabla ya kujiunga na shirikisho hilo, alisema ni vema Tanzania ikajitazama hali yake ilivyo hivi sasa kiuchumi, huku ikiwaangalia watu wake, hasa wanataaluma kama madaktari, wahandisi, wahasibu, wanasheria pamoja na wananchi wa kawaida, watakavyoshindana katika soko la pamoja.

Akitoa takwimu, Simba, ambaye ni mtetezi mkubwa wa sera ya uzawa, alisema Watanzania wanakadiriwa kuwa milioni 34, ambapo asilimia 50 ni mchanganyiko wa watu wasioweza kufanya kazi.

Alisema kwamba kati ya watu milioni 17 wanaoweza kufanya kazi, ni milioni mbili pekee ndio wamo katika sekta rasmi ya uchumi ambao ndio wanaolipa kodi ya mapato na ndio wanaojulikana.

Alisema ni vyema Watanzania wakafahamu kwamba mabenki yote nchini hivi sasa hayana akaunti za biashara zinazozidi 60,000, kwa kuwa kiwango cha uzalishaji mali ni kidogo ukilinganishwa na ukubwa wa nchi.

Alisema utafiti unaonyesha kwamba kati ya watu milioni 15 walio katika sekta isiyo rasmi, wanaofanya kazi ni milioni tisa tu. Hii inaacha asilimia sita ya watu ambao hawafanyi kazi, ingawa wana uwezo wa kufanya kazi.

“Hiyo imeongeza idadi ya watu tegemezi na kuwa watu milioni 23, sawa na asilimia 68 ya Watanzania wote,” alisema.

Alisema hata mgawanyo wa kazi miongoni mwa walioajiriwa unatia shaka, kwani Watanzania wengi wamebakia kufanya kazi zisizo na maana huku nafasi kubwa zikishikwa na wageni.

Alisema kutokuwapo kwa sera madhubuti ya elimu ni miongoni mwa matatizo yanayowakabili Watanzania.

Alisema uwekezaji katika elimu umekuwa mdogo nchini kiasi cha baadhi ya wazazi kutofahamu umuhimu wa elimu kwa watoto wao na kudiriki kukatisha masomo kutokana na sababu za kiuchumi na kimila.

Alisema walimu wamekuwa hawaheshimiwi ipasavyo na badala yake masheha, madiwani wahandisi na madaktari ndio wanaopewa heshima zaidi.



How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Jered)
    Rating
    Kikwete na Lowassa inabidi wajifunze kuongea kutoka kwa watu wenye busara kama Iddi Simba. Sijawasikia hata siku moja wakitoa hoja kama hizi, wanaongea tu kama wajinga na wala hawana takwimu.

    Kazi kutoa amri kama askari wa kikoloni. Kikwete and Lowassa, you have a long way to go.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.