SASA ni dhahiri kwamba mgomo wa siku nne wa mahabusu umeitikisa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, baada ya jana mawaziri wake wanne waandamizi kulazimika kwenda katika Gereza la Keko kuzungumza na mahabusu hao.
Hatua hiyo imetokana na agizo la Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwa mawaziri hao la kuwataka washirikiane ili kutatua tatizo hilo.
Mawaziri hao walifanya hivyo jana baada ya juzi mahabusu hao kugoma kuonana na makamanda wa juu wa Jeshi la Polisi kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Katika madai yao, walisema wanataka kukutana na mawaziri na iwapo itawezekana, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye hivi sasa yupo katika ziara mkoani Kagera.
Waliofunga safari jana hadi Gereza la Keko ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Dk. Batilda Buriani, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mary Nagu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai na Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, baada ya mkutano na mahabusu hao, Waziri Nagu alisema kuwa mahabusu hao, ambao wanawawakilisha mahabusu wote nchini, wameahidi kusikitisha mgomo na kuendelea kuhudhuria mahakamani.
“Ni mategemeo yangu Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya DPP na Polisi, watachukua changamoto hii kurekebisha kasoro zilizojitokeza,” alisema Waziri Nagu.
Alisema kuwa katika mkutano huo uliofanyika saa 9 alasiri, mahabusu hao waliainisha malalamiko mbalimbali, yakiwamo ya ucheleweshaji wa upelelezi wa kesi zao, wakitaja kusikitishwa kwao na kuendeshwa kwa haraka kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ditopile Mzuzuri na ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Abdallah Zombe.
Malalamiko mengine ni kubambikiwa kesi, hasa kwa makosa yasiyokuwa na dhamana, kunyimwa dhamana, hasa katika mahakama za mwanzo na wilaya, kuwapo vikao vichache vya Mahakama Kuu na mahakama kutotumia kifungu namba 225 kufuta kesi, baada ya siku 60 tangu kufunguliwa, na kushindwa kuanza kusikilizwa bila ya sababu za msingi.
Malalamiko mengine ya mahabusu hao ni kuchelewa kufanyika kwa ‘committal proceedings’, kuchelewa kupatikana kwa taarifa za wataalamu kama ripoti za madaktari kuhusu vyanzo vya vifo (Postmortem Examination Report).
Dk. Nagu alisema kwa kuzingatia ambavyo serikali inawajali wananchi wake wakiwamo mahabusu, hatua zimechukuliwa kukabiliana na matatizo hayo.
“Serikali katika kulishughulikia suala kama hili inafanya kazi kama timu, kwa kutambua kuwa wizara au idara moja peke yake haiwezi kulimaliza. Yapo mambo yanayofanywa na Wizara ya Usalama wa Raia, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Mahakama. Hatua za pamoja ndizo zitaweza kutoa suluhisho la kudumu la matatizo haya,” alisema Waziri Nagu.
Alisema kuwa kuhusu baadhi ya kesi kuchukua muda mfupi kuliko nyingine katika upelelezi, wanao uzoefu kupitia Ofisi ya DPP kuhusu masuala hayo.
Alisema kuwa kesi nyingine huchelewa kutokana na mazingira ya kesi husika, na akaongeza kuwa wapo watuhumiwa wengine hutoa taarifa za matukio polisi na kisha kutoa ushirikiano unaohitajika katika upelelezi wa kesi zao, hivyo kufanya kesi zao kwenda haraka.
“Ni wazi katika hali na mazingira ya namna hiyo, upelelezi utawahi kukamilika kuliko inavyokuwa katika matukio ambayo mtuhumiwa husika hatoi ushirikiano unaohitajika,” alisema.
Aidha, Waziri Nagu alieleza kuwa kesi moja huweza kuchelewa upelelezi wake kutokana na ugumu wa kukusanya ushahidi kuliko ilivyo katika kesi nyingine.
“Kwa ujumla kila kesi inastahili iangaliwe kwa mazingira yake. Katu upelelezi hautegemei hali aliyokuwa nayo wakati au kabla ya tukio. Sitatoa maelezo zaidi kuhusu hili kwa sababu Idara ya Polisi ilishatoa maelezo kuhusu suala hili,” alisema waziri huyo.
Hata hivyo, Waziri Nagu alisema kuwa serikali haipuuzi malalamiko kuwa haki haitendeki.
Alisema kuwa serikali inakabiliana na upungufu wa mahakimu na majaji, ili kuwezesha kesi nyingi zaidi kusikilizwa na hivyo kupunguza tatizo la kuahirishwa kwa kesi mara kwa mara.
Pia alisema vikao vya Mahakama Kuu vimeongezwa katika kila kanda kutokana na kuteuliwa kwa majaji wapya hivi karibuni. Alisema kuwa hali hiyo itaongeza kasi ya usikilizaji wa kesi katika ngazi hiyo.
Waziri Nagu alisema kuwa mahakama imekuwa ikizingatia sheria za nchi zinazohusu utoaji wa dhamana kwa mahabusu wanaokabiliwa na makosa ambayo yanaruhusu dhamana.
Hata hivyo, alisema utoaji huo wa dhamana lazima ufuate misingi ya kisheria, ambapo msingi mkuu ni kuhakikisha kuwa mwenye kupewa dhamana anahudhuria mahakamani kila kesi yake inapopangwa kusikilizwa.
“Masharti ya dhamana yanatolewa kuzingatia msingi huu, na hivyo ni wazi anayeshindwa masharti ya dhamana hataweza kupewa dhamana hiyo. Tutahimiza mahakama kutumia uwezo wao wa kutoa dhamana pale ambapo sheria haiwabani,” alisema.
Alisema kuwa hatua nyingine ambazo serikali imekuwa ikichukua katika kukabiliana na hali hiyo ni kusikiliza mashauri katika awamu mbili kwa siku, ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa majengo na vyumba kwa shughuli za mahakama.
Pia utaratibu wa vikao vya kufuatilia mwenendo wa mashauri (Case Flow Management Committee) katika ngazi ya taifa, kanda, mkoa na wilaya, ili kushughulikia matatizo yote ya ucheleweshaji wa kesi, utaimarishwa, pamoja na manufaa mengine, unaweza kusaidia kubaini kesi ambazo ni za kubambikizwa.
Kwa utaratibu huo, alisema kesi ambazo zilichelewa kusikilizwa hujadiliwa na kupatiwa ufambuzi kwa wakati.
Waziri Nagu alitoa wito vikao hivyo vifanyike kama inavyotakiwa katika ngazi mbalimbali, ili kuondoa adha inayowakabili watu wanaolazimika kukaa magerezani kwa kipindi kirefu.
Kwa majalada yanayokamilishwa kufanyiwa upelelezi na kupelekwa katika Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali, alisema kuwa watahakikisha yanashughulikiwa ndani ya siku 14 kama ilivyoainishwa katika mkataba wa huduma kwa mteja.
Alisema katika kutambua msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani, serikali itaendelea kutoa msamaha kwa wafungwa mara kwa mara.
Mgomo huo ulianzishwa Jumatatu na mahabusu katika Mahakama ya Kisutu kabla ya kusambaa katika mahakama nyingine za Dar es Salaam na hatimaye katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Shinyanga.