Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  12 wafariki katika ajali
12 wafariki katika ajali
By Habari Tanzania | Published  06/21/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Watu 12 wamekufa papo hapo wakiwemo polisi wanne na watu wengine 45 kujeruhiwa katika ajali tatu tofauti zilizotokea katika mikoa ya Tanga, Pwani na Lindi.

Katika ajali ya kwanza iliyotokea mkoani Tanga, polisi wanne pamoja na raia mmoja, walikufa papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa baada ya magari matano kugongana kwa mpigo katika kijiji cha Kwamkonga, wilayani Handeni.

Polisi wote hao ni wa kituo cha Kabuku, Wilayani Handeni na walikuwa katika gari maarufu kama ’kigofu’ lenye namba za usajili PT 0101.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Bw. Issaya Mngulu, alisema ajali hiyo lilitokea juzi saa 5:00 usiku baada ya gari lenye namba za usajili T136 ADW aina ya Rhino likitoka Moshi, kuserereka na kuligonga kwa nyuma gari hilo la polisi lililokuwa limesimama wakati askari hao wakiwa katika doria.

Kamanda Mngulu aliyekuwepo eneo la tukio jana, aliwataja askari waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni D 6948 Station Sajenti Pastory Kazabila aliyekuwa dereva wa gari hilo.

Wengine ni F 5460, Konstebo Lugoe Obadia, F 5523, Konstebo Richard Katumbuku na F 8116, Konstebo Zuberi Amiri Mbaga, wote askari wa kituo cha Kabuku.

Kamanda Mngulu alimtaja mtu mwingine aliyekufa kwenye ajali hiyo ambaye alitambuliwa kwa jina moja kuwa ni Daud aliyekuwa dereva wa gari la mafuta.

Majeruhi wa ajali hiyo ambao pia wamelazwa katika hospitali hiyo wametambuliwa kuwa ni Joseph Lukindo (34), mkazi wa Kinondoni, Jijini Dar es Salaam aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Starlet na Yusuph Abbas.

Kamanda Mngulu alifafanua kuwa katika ajali hiyo, gari aina ya Rhino lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye hakupatikana, lililigonga gari lingine la kubeba mafuta aina ya Isuzu lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Tanga lenye namba T 537 ACD na kisha gari hilo kuserereka na kuligonga gari la polisi.

Alisema baada ya gari hilo la polisi kugongwa, pia liliyagonga magari mengine mawili yaliyokuwa yamesimama yakitokea mpaka wa Holili, mkoani Kilimanjaro.

Kamanda Mngulu aliyataja magari hayo kuwa ni yenye namba za chassis EP 910245651 aina ya Toyota Stalert na nyingine chassis TA 01W837923 aina ya Suzuki Escudo.

Kamanda Mngulu aliongeza kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi wa gari aina ya Rhino ambapo lilipofika katika eneo hilo dereva alishindwa kusimama licha ya kwamba yalikuwepo magari manne yaliyokuwa yamesimama.

Alisema katika eneo ilipotokea ajali hiyo, juzi mchana gari moja aina ya Scania iliyokuwa na chassis namba XLER 62000264520 lilianguka na kichwa chake kung’oka na kuangukia katikati ya barabara.

’’Kwa kweli gari letu la polisi licha ya kuwapoteza askari wetu, halifai tena, maana limepondeka, hata miili yao tulipata shida kuitoa,’’ alisema Kamanda Mngulu na kuongeza kuwa, hiyo ilikuwa ni ajali mbaya kuiona.

Katika ajali iliyotokea mkoani Pwani, watu watano wamekufa papo hapo na wengine 36 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Diplomatic Comando lililokuwa likielekea mkoani Lindi, kupinduka katika kijiji cha Kitembo Kibitim, wilayani Rufiji, anaripoti Aboubakary Mlawa wa PST, Pwani.

Basi hilo lenye namba T457ADG ,lilipinduka baada ya kupasuka gurudumu la mbele ambapo kati ya watu waliokufa, wamo watoto watatu ambapo wawili ni familia moja.

Waliokufa ni watoto Abdullah Rashid Mawa, Yassin Abdulrahaman na Rose Paul ambao ni ndugu.

Wengine ni Bi. Amina Mmaliwa Likayomba na Maneno Juma Philipo.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika kituo cha Afya cha Kibiti.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Christine Ishengoma, aliyetembelea eneo la ajali, ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kumkamata mara moja mmiliki na dereva wa basi hilo aliyetajwa kuwa ni Hamis Chikomera kwa kosa la kusafirisha abiria wakati basi likiwa ni bovu.

Majeruhi wa ajali hiyo walipatiwa matibabu katika hospitali ya misheni ya Mchukwi na Kituo cha Afya cha Kibiti ambapo pia maiti zimehifadhiwa hapo.
Katika hatua nyingine, kampuni ya Diplomatic Comando, ilipeleka basi lingine T471ADG kuwapeleka Lindi abiria waliopata nafuu huku.

Hata hivyo, matairi ya basi hilo ni mabovu hali iliyomfanya Mkuu wa Mkoa kulizuia hadi hapo litakapowekwa matairi mengine.

Kutoka Lindi, mwandishi Said Hamdani, wa PST anaripoti kuwa, watu wawili wamekufa papo hapo na wengine sita kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti zilizotokea katika maeneo tofauti.

Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Bw Saimon Dau, alisema ajali hizo zilitokea mwishoni mwa wiki majira ya mchana.

Kamanda Dau aliwataja waliokufa katika ajali hizo kuwa ni Mohamed Salum (22), mkazi wa kijiji cha Mtua Tinduru ya Leo, Wilaya ya Ruangwa na Nishel Rajabu (12), mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Rahaleo, ya mjini Lindi.

?Aliwataja majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo ya Mkoa ya Sokoine kuwa ni Mwajuma Mecknard (22), mkulima wa kijiji cha Kingolwira, mkoani Morogoro ambaye amekatika kiganja cha mkono wa kushoto, Sophia Mohamed (38), mkazi wa Kilwa Masoko, aliyekatika unyayo wa mguu wa kushoto na Deogratius Abeid (32), aliyekatika vidole viwili vya mguu wa kushoto.

?Wengine ni Justine Thomas (23), aliyeumia kifua, Hassan Mbaura (30), aliyepata michubuko kwenye mwili wake na Mohamed Twalib (24), aliyeumia goti la mguu wa kulia, wote ni wakazi wa kijiji cha Nangumbu, wilayani Ruangwa.

?Alisema ajali ya kwanza iliyosababisha kifo cha mtu mmoja (Mohamed Salum) na majeruhi sita, ilitokea baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka mkoani Lindi kwenda? Jijini Dar es Salaam kupinduka.

Kamanda Dau alisema gari hilo lilipinduka baada ya kushindwa kupanda mlima Mamburu katika barabara ya Mingoyo-Lindi-Kibiti.

?Bw. Dau alisema gari hilo lori aina ya Fusso lenye namba za usajili T. 922 AJJ lilikuwa likiendeshwa na Abdulrahaman Omari (37), mkazi wa Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.

Alisema lori hilo lilikuwa limebeba viroba 125 vya mahindi kupeleka Dar es Salaam.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe uliotokana na dereva kubadili gia katikati ya mlima wakati akifahamu kuwa mlimani mkubwa huku gari yake ikiwa na mzigo.

Alisema dereva anashikiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani kujibu shtaka la kusababisha kifo.

Katika ajali ya pili, Kamanda Dau alisema mwanafunzi Rajabu alikanyagwa kichwani na gari aina ya Toyota Hiace yenye namba T. 634 ACT iliyokuwa ikiendeshwa na Bakari Nachungu (35).

Alisema ajali hiyo ilitokea Barabara ya Jamhuri, eneo la Briji Mjini Lindi, wakati mwanafunzi huyo akiendesha baiskeli.

Alisema dereva huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.