Na Patricia Kimelemeta
MKURUGENZI wa Taifa wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amemtaka Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kusimamia mwenyewe tatizo la msongamano wa abiria na kushughulikia ujenzi wa barabara kuliko kuziachia manispaa.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mnyika alisema suala la usimamiaji wa barabara na miundombinu ni jukumu la Serikali Kuu na si Manispaa, hivyo yeye kama kiongozi mkuu wa serikali anao wajibu wa kutoa amri kwa wakandarasi kutekeleza amri yake mapema.
"Waziri Mkuu lazima awajibike kwenye ujenzi wa barabara kwa sababu ni wa Serikali Kuu na iko chini ya ofisi yake, si kutoa amri kwa halmashauri huko, alisema Manyika na kuongeza kuwa huko ni kuzibebesha mzigo bila sababu.
Alisema kuwa Waziri Mkuu anapaswa kutoa muelekeo wa serikali yake inakwenda wapi, na inafanya nini, huku akitengenza miundombinu na uwajibikaji mzuri.
Mnyika alisema kazi ya vyama vya upinzani ni kuweka wazi madahifu yanayofanywa na serikali ili waweze kutetea jamii katika kuleta maendeleo ya kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi Taifa.
Mnyika pia alisema Taasisi ya Kuzuia Rushwa (Takuru) isiwe chini ya Rais bali kiwe chombo huru kikiongozwa na Bunge ambacho kitapambana na wala rushwa wa pande zote bila woga ili kuleta haki.
"Sisi kama wapinzani tunaitaka Takuru iwe chini ya Bunge na si Rais, ili kiwe chombo huru ambacho kitatenda haki kwa pande zote," alisema Mnyika.