Na Waandishi Wetu
MGOMO wa mahabusu wa kupinga kucheleweshewa kesi zao ulioanza katika Mahakama ya Kisutu juzi, umeendelea jana na kusambaa katika mahakama nyingine jijini Dar es Salaam na mjini Arusha.
Jijini Dar es Salaam, mahabusu hao waligoma kwa mara ya pili kushuka katika karandinga, wakishinikiza Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Mary Nagu, atoe tamko juu ya kesi zao ambazo wanadai zimechukua muda mrefu bila ya upelelezi wake kukamilika.
Mgomo huo uliingia siku ya pili jana, baada ya juzi mahabusu hao kukataa kushuka katika karandinga kwa ajili ya kusikiliza kesi zao, wakishinikiza upelelezi wa kesi zao ufanywe haraka kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila ya kukusudia.
Mgomo huo ambao unaonekana kuishika pabaya serikali, uliendelea tena jana kwa nyakati tofauti katika mahakama ya Kisutu na mahakama za wilaya za Ilala na Temeke ambako mahabusu waligoma kushuka huku wakisisitiza kuwa hawatafanya hivyo hadi hapo serikali itakapotoa tamko kuhusiana na madai yao.
Wakiwa ndani ya makarandinga ya polisi katika mahakama hizo, mahabusu hao waliendelea na staili yao ya kuimba nyimbo za kudai haki na kuishutumu serikali kuwa inafanya upendeleo katika kushughulikia kesi za vigogo na walalahoi.
Walimtaka Dk Nagu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) watoe tamko litakalofafanua muda ambao mtuhumiwa wa mauaji anastahili kukaa mahabusu wakati upelelezi wa kesi yake ukiendelea kwa kile walichoeleza kuwa upo upendeleo wa dhahiri katika kushughulikia kesi hizo.
Walisema tatizo zaidi linakuwa katika kesi zinazohusisha vigogo wa serikali na watu maarufu, huku zile zinazowahusu walalahoi zikipuuzwa na upelelezi wake ukichukua muda mrefu na kuwaacha wakiteseka gerezani bila ya kupatiwa haki za msingi.
Pia walimtaka Waziri Nagu, atembelee magereza aweze kujionea mwenyewe hali halisi, ili ajue kuwa kuchelewesha kesi hizo ni kuwaumiza na kuwapa mateso makubwa mahabusu.
Katika Mahakama ya Kisutu, jana, karandinga la kwanza lililochukua mahabusu kutoka Gereza la Keko lilifika saa 3.30 asubuhi na kama ilivyokuwa juzi, waligoma kushuka na baada ya muda mfupi walirudishwa gerezani.
Karandinga la pili lilifika saa 4.38 asubuhi, likiongozwa na gari la polisi namba T 220 AMV Land Rover, lakini mahabusu waliokuwamo pia waligoma kushuka na kurudishwa mahabusu.
Katika mahakama za wilaya za Ilala na Temeke, kesi zote zinazohusu mahabusu waliotoka katika magereza ya Keko na Segerea, ziliahirishwa jana baada ya mahabusu kugoma kushuka kwenye karandinga wakidai kucheleweshwa kwa upelelezi wa kesi zao.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya mahabusu waliokuwa wakitarajia dhamana, waliangua kilio baada ya kuwaona ndugu zao waliofika mahakamani hapo kwa ajili ya kuwawekea dhamana.
Katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, waliobahatika kushuka kwenye karandinga ni mahabusu wanawake kutokana na wao kuwekwa katika chumba tofauti na wanaume ndani ya gari lililowafikisha mahakamani hapo.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Joyce Minde, alisema kuwa amewasiliana na polisi ili wafuatilie suala hilo.
Mjini Arusha, mahabusu wanaokabiliwa na kesi mbalimbali nao waligoma kushuka katika karandinga katika viwanja vya Mahakamani Kuu wakitaka kuonana na Rais Jakaya Kikwete ambaye alikuwa jirani na mahakama hiyo, ilipo Ikulu ndogo wakilalamikia kucheleweshwa kesi zao.
Mahabusu hao wanaokaridiwa kufikia 70, walipaza sauti wakilalamikia kuachiwa kwa dhamana kwa Ditopile huku wao wakiachwa wateseke gerezani.
Mahabusu hao baadaye walianza kuimba kwa sauti kubwa "polisi wanataka nini...wanataka rushwa na Ditopile kawapa nini, kawapa rushwa" hatua ambayo ilizuwa tafrani kubwa mahakamani hapo na kwa maafisa wa usalama ambao walikuwa viwanja vya Ikulu.
Tukio hilo lilianzaa majira ya saa 3.30 mara baada ya mahabusu hao kuwasili katika gari lao lenye namba za usajili STG 9266 na lilidumu hadi saa 4.11 pale maafisa kadhaa wa polisi walipowasili na kuamuru mahabusu hao kurejeshwa magerezani.
Maafisa wa polisi wakiwa katika gari lenye namba za usajili T638AJR na polisi wengine wa kutuliza ghasia wakiwa katika gari lenye namba za usajiri T 447 APF waliwaondoa mahabusu hao kupitia njia tofauti na ambayo hutumika, hivyo kukwepa Rais Kikwete asisikia kelele hizo.
Awali, mahabusu hao huku wakipiga mayowe, walikuwa wakilalamikia polisi kuchelewesha kesi zao na hasa upelelezi, hatua ambayo inachangia kukaa muda mrefu magerezani.
Hata hivyo, hakuna hakimu ambaye alikuwa tayari jana kuongelea tukio hilo kwa maelezo kuwa wanaolalamikiwa ni polisi na sio wao.
Katika mgomo wa juzi katika mahakama ya Kisutu, Mahabusu wanaokadiriwa kuwa kati ya 250 hadi 300 wakitokea katika magereza ya Keko na Segera, waligoma kushuka ndani ya magari ya polisi STH 3058 na STJ 903 wakilalamikia ucheleweshwaji wa upelelezi wa kesi zao.