Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uchaguzi Tunduru waingia mashakani
Uchaguzi Tunduru waingia mashakani
By Habari Tanzania | Published  03/14/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Leon Bahati
MAHAKAMA Kuu leo itatoa uamuzi kama uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Tunduru, mkoani Ruvuma  unaotarajia kufanyika Jumapili usimamishwe au la.

Lakini mahakama hiyo imetupilia mbali hoja za utetezi za  wadaiwa ambao ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali za kutaka uchaguzi huo uendelee kama ulivyopangwa.

Uamuzi wa leo unahusu ombi la Mwenyekiti wa Domocratic Party, Mchungaji Christopher Mtikila, kutaka uchaguzi huo usimamishwe, wakati mahakama inaendelea kusikiliza kesi ya msingi ya kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuzuiwa kuendesha chaguzi hadi mchakato unaoruhusu wagombea binafsi uingizwe katika kanuni za chaguzi.

Pia katika ombi hilo, Mtikila anaomba uchaguzi wa Tunduru usimamishwe ili zaidi ya watu 11,000 walionyimwa haki ya kuajiandikisha kwa kutokuwemo katika Daftari la kudumu lililoandaliwa kabla hawajafikisha umri wa miaka 18 wapewe haki hiyo.

Jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo linaongozwa na Jaji Othmani Chande jana liliwataka mawakili wanaomtetea Mtikila kufanyia marekebisho hati yao ya kiapo kwa kuwa walitaja kipengele namba nne badala ya mbili kinachohusiana na taratibu za kufungua kesi mahakamani (Judicator Application of Law).

Mara baada ya kusikiliza hoja za pande zote jana mchana, majaji hao waliahirisha kesi hiyo hadi saa tisa ili kutoa umauzi, na waliporejea Jaji Chande kwa niaba ya wenzake, alisoma maoni ya majaji hao, lakini akaahirisha uamuzi rasmi utakaosomwa leo.

Jaji huyo alikuwa anasaidiana na Jaji Robert Makaramba na Jaji Amir Mruma, alitupa hoja kadhaa zilizotolewa na jopo la wanasheria wanne, Mathew Mwaimu, Abraham Senguji, Paulo Ngwembe na Nikson Ntimbwa wanaoitetea Tume ya Taifa ya Uchaguzili na Mwanasheria wa Serikali.

Hoja zilizotupwa, ni ya kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali kwa kuwa haiwezi kusikilizwa na mahakama hiyo na kwamba serikali tayari imekata rufaa kupinga kuwepo kwa mgombea binafsi.

Akifafanua juu ya hoja hizo, Jaji Chande alisema kwamba mahakama hiyo ina haki ya kusikiliza kesi hiyo kwa kuzingatia ibara ya 33 ya Katiba inayohusu mtu kujitetea katika kupata haki.

Kuhusiana na rufaa ya serikali, Jaji Chande alisema kwamba rufaa ya serikali haiwezi kuizuia kesi iliyofunguliwa na Mtikila kwa sababu ni tofauti na zote zinaweza kusikilizwa na mahakama.

Jaji Chande pia alitupilia mbali hoja ya utetezi kwamba hakuna mtu aliyeiendea Tume ya Uchaguzi Tunduru kutaka aandikishwe na ombi lake likakataliwa.

Hii ilitokana na hoja ya wakili Mwaimu kuitaka mahakama hiyo itupilie mbali kipengele kilichotolewa na wakili anayemtetea Mtikila kwamba baadhi ya wakazi wa Tunduru wamenyimwa haki ya kupiga kura kwa kutopewa fursa ya kujiandikisha.

Mwaimu aliiambia mahakama kuwa hakuna mtu aliyeiendea Tume ya Uchaguzi akakataliwa kuandikishwa.

Mahakama iliikataa hoja hiyo kwa sababu tume ingeweza kutoa utaratibu utakaowezesha wale ambao hawajaandikishwa na wamefikia umri unaowaruhusu kupiga kura waorodheshwe.

Awali, wakili anayemtetea Mtikila, Mpale Mpoki alikuwa ameiambia mahakama kuwa Tume ya Uchaguzi tayari ilikuwa imetoa waraka unaoonyesha kuwa watakaoshiriki katika uchaguzi huo ni wale tu ambao wameandikishwa katika daftari la wapiga kura kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita (2005).

Jaji Chande alisema kwamba baada ya mahakama kupokea marekebisho ya hati ya kiapo iliyotumika kuifungua kesi hiyo, itatoa hukumu ya ombi la upande wa walalamikaji la kuomba uchaguzi wa Tunduru usimamishwe kwa kuwa taratibu zimekiukwa.

Katika kesi ya msingi, Mtikila anataka mahakama iamuru  Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoendesha uchaguzi wowote hadi mchakato unaomruhusu mgombea binafsi nchini uingizwe katika kanuni za uendeshaji wa chaguzi.

Kesi hiyo ilifunguliwa baada ya Mahakama Kuu mwaka jana kutamka kuwa katiba ya Tanzania inatoa haki kuwepo kwa mgombea binafsi katika chaguzi mbalimbali kwenye kesi iliyokuwa imefunguliwa na Mtikila.

Hata hivyo, serikali tayari imekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Rufaa kupinga uamuzi huo jambo ambalo lilielezwa mahakamani na mawakili wanaomtetea mtikila kuwa ni ‘rafu’ dhidi ya kesi yao ambayo imeandamana na ombi la kutaka kuusimamisha uchaguzi mdogo Tunduru.

Katika hatua nyingine, Muhibu Said anaripoti kutoka  Tunduru kuwa zikiwa zimesalia siku nne kufanya uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Tunduru mkoani Ruvuma, kamatakamata inayohusishwa na  hisia na shinikizo la kisiasa imeendelea baada ya wafuasi watatu wa Chama cha Wananchi (CUF) kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kumng'oa meno mfuasi wa Chama cha mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, habari kutoka kijijini hapo zilizothibitishwa a  baadhi ya wanakijiji, zilieleza kuwa aliyedaiwa kung'olewa meno, Jafar Bakari,  ambaye hadi sasa hajafika kituoni kuandikisha maelezo, amekuwa na mapengo kinywani mwake tangu miaka mingi.

Mbali na kukamatwa vijana hao wanadaiwa kupekuliwa na polisi wakituhumiwa kuficha silaha. Pia wanadaiwa kupewa adhabu na polisi ya kufyeka nyasi nje ya kituo cha polisi, kusomba matofari na  kufagia nje na ndani ya kituo na kupigwa virungu, ngumi, makofi na mateke.

Askari hao wa kituo cha Lukumbule  wanadaiwa pia kuwatolea maneno ya kejeli, ikiwa ni pamoja na  watahakikisha hawashiriki katika uchaguzi huo wa Jumapili.

Pia wanadaiwa kuwazuia vijana hao kupata huduma mbalimbali za kibinadamu, ikiwamo maji na kuwafukuza ndugu zao kuwawekea dhamana.

Kutokana na mkong'oto na adhabu waliyopewa na askari hao, mmoja wa vijana hao amejeruhiwa mkononi, mwingine usoni na wa tatu mguuni.

Vijana hao ni Ausi Rashid (24),  Hussein Makwaya (25) na Ajali Rashid (26), wote wakazi wa Kijiji cha Mitwana, kaya ya  Lukumbule.

Baada aya kutiwa nguvuni vijana hao walishikiliwa kuanzia saa 11.00 jioni hadi asubuhi juzi, walipoondolewa na kupelekwa kituo cha polisi mjini Tunduru chini ya ulinzi wa Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Mbaralah Maharagande alisema hapa jana kuwa imebidi uongozi wa chama hicho kuonana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tunduru, ili kuwawekea dhamana vijana hao.

Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma, Falhum Mshana, hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.

Wakati huo huo, Kizitto Noya anaripoti kuwa wenyeviti wa vyama vya CUF na NCCR- Mageuzi, Ibrahim Lipumba na James Mbatia, wanatarajia kuondoka leo kuelekea Tunduru kunakofanyika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge, pamoja na mambo mengine, kushinikiza kuapishwa kwa mawakala 60 wa CUF.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibarahim Lipumba alisema jana Dar es Salaam kuwa Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Tunduru amegoma kuwaapisha mawakala wa chama hicho kwa sababu zisizojulikana.

Alisema wakati mawakala wengine wote waliapishwa juzi, mawakala wa CUF katika kata za Mlingoti Magharibi, Muhuwesi na Kidodoma walikataliwa kuapishwa na maafisa watendaji wa kata hizo na kwa mujibu wa maelekezo ya msimamizi huyo hawataruhusiwa kuingia kwenye vyumba vya kuhesabia kura siku ya kupiga kura.

“Barua ya msimamizi wa uchaguzi huo iliwataka mawakala wote kuapishwa Machi 12 na kinyume chake wakala asiyeapishwa hataruhusiwa kuingia kwenye chumba cha kuhesabia kura, uamuzi huo wa kutowaapisha mawakala wetu umelenga kutuhujumu,” alisema Prof Lipumba

Uchaguzi mdogo wa Tunduru ni kwa ajili ya kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Juma Akukweti kufariki dunia


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.