NG’OMBE wanane wanaofugwa katika shamba la mifugo linalomilikiwa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa lililopo Handeni, mkoani Tanga wameibwa.
Habari za uhakika kutoka Tanga zilizothitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Isaya Mngulu zinaeleza kuwa wizi wa ng’ombe hao, wanaofugwa kisasa, ulitokea katika shamba hilo na mfanyakazi mmoja wa Waziri Mkuu ambaye jina lake halikuweza kupatikana, anadaiwa kuwa ndiye aliyewaiba.
Kwa mujibu wa habari hizo, tukio hilo ambalo lilimfadhaisha Lowassa, lilifuatiwa na msako mkali ulioendeshwa na Jeshi la Polisi katika maeneo ya karibu ya shamba hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, siku chache tu baada ya wizi huo kutokea, Waziri Mkuu akiwa ameongozana na wanafamilia yake, alikwenda Handeni.
Akiwa huko, taarifa zimemkariri Waziri Mkuu anayetoka katika kabila maarufu la wafugaji la Kimasai, akieleza kusikitishwa na tukio hilo la wizi ambalo kwa kiwango kikubwa linaonyesha udhaifu katika suala zima la ulinzi katika eneo hilo.
Kamanda Mngulu alipopigiwa simu na mwandishi wa habari wa gazeti hili ili kujua ukweli kuhusu tukio hilo, alikiri kulifahamu na akasema kuwa aliyehusika na wizi huo ni mfanyakazi katika shamba hilo ambaye hata hivyo hakumtaja.
Awali, chanzo kimoja cha habari kilichowasiliana na gazeti hili, kilieza kwamba, ng’ombe walioibwa katika shamba hilo ni 90 na si wanane kama ilivyoelezwa na Kamanda Mngulu.
“Ni kweli kulikuwa na tukio hilo la ng’ombe wa Waziri Mkuu kuibwa, ingawa si kweli kwamba walioibwa ni ng’ombe 90, bali ni wanane tu.
“Aliyefanya wizi huo ni mfanyakazi mmoja katika shamba hilo ambaye alishapatikana akiswaga ng’ombe wawili katika eneo la Kilindi,” alisema Kamanda Mngulu.
Kamanda huyo alilieleza gazeti hili kwamba, muda mfupi baada ya wizi huo kufanywa, ng’ombe sita kati ya wanane walioibwa, walipatikana baada ya kurejea wenyewe baada ya mwizi huyo wa ng’ombe kushindwa kuwamudu.
Alipoulizwa iwapo safari ya mwishoni mwa wiki ya Lowassa ilikuwa ina uhusiano wowote na tukio hilo la wizi, Kamanda Mngulu alikanusha na akasema, alikwenda huko kutembelea shamba lake.
Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu, Said Nguba, alipotafutwa kwa simu jana, alisema hakuwa na taarifa zozote kuhusu suala hilo na akamtaka mwandishi wetu kumpa muda wa kuwasiliana na wenzake kabla ya kutoa taarifa kamili.
Kabla ya kuahidi kutafuta ukweli kuhusu suala hilo, Nguba alimtaka mwandishi amueleze ni wapi alikuwa amezitoa taarifa za tukio hilo.
Alipopiga simu jana jioni, Nguba alikiri kuwapo kwa tukio hilo na akasema taarifa alizokuwa nazo zilikuwa zikieleza kuwa, ng’ombe walioibwa walikuwa wawili tu, ambao hata hivyo walikwishapatikana.
Kama ilivyo kwa Lowassa, viongozi kadhaa walio madarakani na wale waliostaafu, wamekuwa wakijihusisha sana na umiliki wa mashamba ya mifugo katika maeneo mbalimbali nchini.
Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye naye anamiliki shamba kubwa la mifugo huko Kiluvya, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ambako nako miezi ya hivi karibuni kulikuwa na taarifa za ng’ombe wake kadhaa kuibwa.
Kiongozi mwingine mwenye ranchi kubwa ya mifugo ni Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya, ambaye eneo lake lililoko Sumbawanga na lililowahi kuzusha utata mkubwa, lilitembelewa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa hivi karibuni