OFISI ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) visiwani hapa imetaka isilaumiwe kutokana na kitendo cha mahakama kuzitupilia mbali kesi zinazowakabili viongozi kadhaa kuhusiana na ubadhirifu wa mali ya umma.
Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Othman Masoud, alisema kesi nyingi za wizi wa mali ya serikali zinatupwa na mahakama visiwani humu kutokana na Polisi kuchelewesha kukusanya ushahidi.
Masoud aliyasema hayo jana baada ya mahakama kufuta kesi tatu za wizi wa mamilioni ya fedha za serikali, kutokana na Polisi kushindwa kukamilisha ushahidi ndani ya miezi minne kama sheria inavyoelekeza.
Kesi zilizotupwa na mahakama ni iliyokuwa ikiwakabili watumishi kadhaa wa serikali waliokuwa wakichota fedha kwa njia ya mishahara hewa, pamoja na kesi ya ubadhirifu iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Suleiman Ali Juma.
Mkurugenzi huyo wa Mashitaka alisema kesi hizo zimetupwa kutokana na Polisi kuchelewesha kuwasilisha majalada ya ushahidi na hivyo mahakama kulazimika kuzitupa.
“Sheria yetu mpya ya mwenendo wa makosa ya jinai inataka ushahidi kupelekwa mahakamani ndani ya miezi minne, la sivyo kesi hiyo inaweza kuondolewa mahakamani,” alisema.
Alitaka wananchi waache kuilaumu ofisi yake kwa kuwa kazi yake kubwa ni kupitia ushahidi ili kubaini iwapo kuna kesi ya kujibu na kuiwasilisha mbele ya mahakama.
“Kwa upande wetu tunatekeleza majukumu ipasavyo, lakini kuna tatizo la kukusanya ushahidi na ndiyo maana kesi hizo zimetupwa,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwamba kwa mujibu wa sheria hiyo ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2004, na marekebisho yake, upande wa mashitaka umepewa miaka mitatu kuirejesha kesi mahakamani, kama Polisi watakamilisha ushahidi.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ramadhan Kinyogo, alisema ni kweli kesi hizo zimefutwa kutokana na muda wa kuwasilisha ushahidi kupita.
Akiitetea ofisi yake, Kinyogo alisema kesi za ubadhirifu zinahitaji muda wa kutosha kukusanya ushahidi na ndio maana majadala ya kesi hizo huchelewa kuwasilishwa mahakamani.
Alieleza kwamba muda wa miezi minne uliowekwa na sheria ni mdogo kwa vile kesi kama hizo zinahitaji muda mwingi ili kupata vielelezo vya kutosha kuthibitisha mashitaka yatakayofikishwa mbele ya mahakama.
“Kwa kuwa sheria bado inatupa nafasi ya kuirejesha kesi mahakamani pale tutakapoona kuna kesi ya kujibu, basi tunaweza kuzirejesha mahakamani baada ya kukamilisha ushahidi,” alisema DCI Kinyogo.
Akielezea sababu nyingine inayowafanya wachelewe kukamilisha upelelezi, Mkurugenzi huyo alisema kwamba mabadiliko ya sayansi na teknolojia pia yanachangia kuwapa wakati mgumu, hasa katika kesi za kughushi.