JAJI Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta, amelaani vurugu zilizofanywa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na baadhi ya ndugu wa mtuhumiwa wa kesi ya kuua bila kukusudia, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri.
Akilaani vurugu hizo, Jaji Samatta alionya kuwa, nchi inaharibiwa na baadhi ya watu wenye tabia ya kudharau amri na hukumu zitolewazo na mahakama kwa matakwa binafsi.
Samatta, alisema hayo jana mjini hapa, baada ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la ghorofa tatu la Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.
Alisema kuwa, kupuuza amri na hukumu za mahakama kutaipeleka nchi kusikotakiwa, na kwamba fujo zitatawala nchi huku wababe wakifurahia hali hiyo na wanyonge wakinyimwa haki zao.
Aidha, alisema kuwa watumishi wa mahakama wanatakiwa kufanya kazi zao katika mazingira tulivu na kusisitiza kwamba, mahakama ni mahali pa haki, hivyo lazima heshima na hadhi ya mahakama izingatiwe.
“Mahakamani ni mahali pa heshima, pana hadhi yake, hivyo watu wote wanatakiwa kuipa hadhi inayostahili mahakama kwa masilahi ya watumishi wa umma na wananchi,” alisema Jaji Samatta.
Alisema vurugu hizo zimelitia aibu taifa na kuwataka viongozi wa ndani na nje ya mahakama kuchukua hatua zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi, kuhakikisha aibu kama hiyo haitokei tena.
Jaji huyo, alisema hakuna aliye juu ya sheria, hivyo mahakimu na majaji watumie sheria kuwahukumu watuhumiwa bila kujali vyeo vyao kwa jamii, ikiwa watadharau amri au hukumu za mahakama, na ikibidi watu hao wafungwe jela.
Jaji Samatta aliweka jiwe hilo la msingi wakati tayari jumla ya sh milioni 710 zimeshatumika hadi sasa na kukamilisha ujenzi wa ghorofa moja.
Jaji Samatta yupo katika ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama mkoani Kagera na leo anaendelea na ziara hiyo kwenye wilaya za Ngara na Biharamulo, ambapo atazungumza na watumishi wa Mahakama.
Alhamisi wiki iliyopita, vurugu zilizuka Mahakama Kuu baada ya ndugu wa Ditopile na baadhi ya askari kuwapiga waandishi wa habari na wapiga picha kwa lengo la kuwazuia wasimpige picha mtuhumiwa huyo aliyeachiwa kwa dhamana.
Kuachiwa kwa Ditopile kumeamsha hisia tofauti miongoni mwa jamii na wanaharakati, hasa baada ya vurugu hizo na maneno ya kejeli dhidi ya serikali yaliyokuwa yakitolewa na ndugu hao.