SAKATA linalomhusisha mfanyabiashara mmoja anayedaiwa kuwalawiti wanafunzi wa shule moja wilayani Kyela, mkoani hapa, limechukua sura mpya baada ya mwandishi wa habari wa gazeti hili kutishiwa maisha.
Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka Kyela na Mbeya Mjini zinaeleza kuwa mtu aliyemtishia maisha mwandishi huyo wa habari, ni mmiliki wa nyumba moja maarufu ya ya kulala wageni, wilayani Kyela.
Taarifa zilizomkariri mwandishi huyo wa habari, Christopher Nyanyembe zinasema kuwa, mfanyabiashara huyo, amechukua hatua hiyo baada ya nyumba yake hiyo ya wageni kudaiwa kutumiwa na mtu anayekabiliwa na tuhuma za kuwalawiti wanafunzi kadhaa wa shule ya msingi hivi karibuni
Inadaiwa kuwa, mfanyabiashara huyo maarufu wilayani hapa (jina tunalo) aliitoa vitisho hivyo akitumia simu ya mkononi iliyokuwa imeficha nambari zake.
Nyanyembe alimweleza mwandishi wa gazeti hili kwamba, mtu huyo alimweleza kuwa alikuwa akitegemea kuchukua hatua dhidi yake ambayo hata hivyo hakuifafanua.
Kwa mujibu wa Nyanyembe, muda mfupi baada ya kupokea vitisho hivyo, alilazimika kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova na akamweleza kupokea vitisho hivyo.
Mwandishi huyo anaamini kuwa, kikubwa kilichosababisha mfanyabiashara huyo kufikia hatua hiyo, ni baada ya kulituhumu gazeti hili kuandika habari ambazo ziligusa eneo lake la biashara.
Hatua ya mfanyabiashara huyo, inakuja siku chache tu baada ya polisi mkoani Mbeya kumnasa mfanyabiashara mwingine ambaye anadaiwa kuwalawiti wanafunzi kadhaa.
Taarifa kuhusu kulawitiwa kwa wanafunzi, kwa mara ya kwanza zilitolewa na wazazi wa wanafunzi hao, ambao vitendo hivyo vimesababisha baadhi yao kufikia uamuzi wa kuwahamisha watoto wao kutoka shule hiyo.
Habari ambazo gazeti hili limekuwa likiziandika kwa siku kadhaa sasa, zinaeleza kuwa, wazazi hao walifikia hatua hiyo baada ya malalamiko yao yaliyothibitishwa na vipimo vya daktari kwamba watoto hao wamefanyiwa vitendo hivyo, kuachwa pasipo kufanyiwa lolote na Jeshi la Polisi wilayani Kyela.
Siku mbili baada ya gazeti hili kuandika taarifa kuhusu tukio hilo la aina yake, Kamanda Kova alituma makachero wa polisi wilayani Kyela, kilometa zipatazo 80 kutoka Mbeya Mjini kwenda kufanya uchunguzi wa kina.
Makachero hao wakiwa Kyela, walikwenda hadi katika nyumba ya wageni inayomilikiwa na mfanyabiashara huyo na kufanya upekuzi baada ya kuelezwa kwamba humo ndimo walimokuwa wakilawitiwa wanafunzi.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kwamba, mfanyakazi mmoja wa nyumba hiyo ya wageni, alitajwa kuwa ndiye aliyekuwa akitumiwa kumpa vyumba mfanyabiashara aliyekuwa akiwalawiti wanafunzi.
Katika hali ambayo hadi hivi sasa, haijaweza kupatiwa majibu, mfanyabiashara ambaye sasa analalamikiwa kutoa vitisho, alimkana mfanyakazi wake huyo.
“Namshangaa sana huyu mfanyabiashara, anaelewa kabisa mazingira ya tukio hilo na vikao walivyoketi, alimkana mfanyakazi wake aliyekuwa akiwapangishia vyumba walawiti, akidai hamfahamu kama ni mfanyakazi,” alisema Nyenyembe ambaye amekuwa akiifuatilia habari hiyo kwa karibu kabisa.
Kamanda Kova alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alikiri kupigiwa simu na mfanyabiashara huyo aliyekuwa akihoji kuwapo kwa habari hiyo.
Kova alilieleza gazeti hili kwamba, alimthibitishia mfanyabiashara huyo kuwa, baada ya makachero wake kufanya uchunguzi, walitoa taarifa ya maandishi kwa vyombo vya habari kuelezea tukio hilo zima.
Kamanda huyo alisema kuwa, maofisa wa jeshi hilo wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Emmanuel Kabwogi, walikwenda hadi kwenye nyumba hiyo wakiongozwa na wanafunzi.
“Tumekwenda hadi kwenye nyumba ya kulala wageni ya… na kuonyeshwa na wanafunzi hao. Hiyo ni taarifa yangu rasmi niliyoitoa kwenye vyombo vya habari kimaandishi, nikiitaja nyumba hiyo, sasa asilete maneno ya uchonganishi,” alisema Kamanda Kova akielezea tukio hilo.
Tanzania Daima ilifichua tuhuma nzito za kulawitiwa kwa wanafunzi wa shule hiyo kulikokuwa kukifanywa na watu wazima, akiwamo mfanyabiashara mmoja ambaye baada ya upelelezi wa polisi alikamatwa.
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa kwenye gazeti hili la Machi 9, iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Babu Seya anaswa Kyela’ ndani yake iliitaja nyumba hiyo ya kulala wageni kuwa ndiyo iliyohusishwa na tukio hilo la kulawiti wanafunzi wa kati ya miaka 13 na 14.