Na Waandishi Wetu
WATU 11 wamekufa katika ajali za barabarani na moto zilizotokea Mbeya na Rukwa mwishoni mwa wiki.
Mwandishi Brandy Nelson anaripoti kutoka Mbeya kuwa watu saba walikufa jana na wengine 14 kujeruhiwa, akiwamo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbozi (OCD), Yesaya Swilla (57), katika ajali iliyohusisha magari matatu kugongana jana usiku eneo la Mpemba, Barabara ya Mbeya- Tunduma Wilayani Mbozi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova aliwataja waliokufa kuwa ni pamoja na Brian Samweli, mtoto mdogo mwenye umri wa miezi saba, mkazi wa Maporomoko Tunduma ambaye alitambuliwa na mama yake aliyekuwa amempakata wakati wa ajali ikitokea.
Wengine ni Swedi Kilindu (25) mkazi wa Old Vwawa, Mbozi, Robert Shombe (25), mkazi wa Ihanda, Mbozi, Frank Sanga (36), mfanyabiashara wa Tunduma na Jane Sanga ( 22), fundi cherehani mkazi wa Tunduma.
Hata hivyo, Kamanda Kova alisema kuwa hadi jana wanaume wawili walikuwa bado kutambuliwa na kwamba inasemekana kuwa ni wafanyakazi wa moja ya magari hayo yaliyogongana.
Kuhusu tukio hilo, Kamanda Kova alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari lenye namba za usajili T335 Toyota Hiace lenye abiria lililokuwa likiendeshwa na mtu aitwaye Christopher ambaye alitoroka baada ya ajali hiyo.
Gari hilo lilikuwa likitokea Mbeya kuelekea Tunduma na lilipofika Mpemba kulikuwa na gari lenye namba za usajili T 904 AMN aina ya Isuzu lori lililokuwa limeegeshwa pembeni kushoto likiwa limeharibika.
Alisema kuwa baada ya Hiace hiyo kufika eneo hilo ililigonga kwa nyuma lori hilo na kisha kuyumba na kuligonga gari jingine dogo aina ya Mark II lenye namba za usajili T.187AJA lililokuwa ikitokea Tunduma na kuendeshwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ( OCD). Kufuatia mtikisiko huo, hiace hiyo iligonga ukuta mdogo wa barabara na kupinduka mara kadhaa.
Majeruhi katika ajali hiyo ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbozi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Yesaya Swilla (57) aliyeumia vibaya usoni upande wa kulia na kupata majeraha chini ya pua na taya na amehamishiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kwa ajili ya uhunguzi na kupata matibabu zaidi.
Wengine 13 waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ni Rudi Mgodi (29), mkazi wa Nakonde, Zambia , Pendo Mashaka (22), mkazi wa Kaloleni, Tunduma, Ibrahimu Msukwa ( 30),Naomi Daudi ( 16), Joyce Wilson ( 26), Leza Amon (21), Kennedy Simubaya (35), Stephen Samweli, Tatu Mahenge, Love Ambonisye (34) na Eugenia Namwanza (35) na mwingine aliyetambuliwa kama Zawadi. Kamanda huyo alisema hali zao zinaendelea vizuri.
Naye Doris Mageta anaripoti kutoka Sumbawanga kuwa watu wanne wa familia moja katika Kijiji cha Kisumba, Wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamefariki dunia katika ajali ya moto uliosababishwa na mafuta ya petroli.
Kati ya waliokufa yumo mama mjamzito katika tukio hilo la Machi 9, saa 12.45 asubuhi katika nyumba walimokuwa wakiishi uliotokana na moto huo wa jiko na kusababisha tukio hilo.
Baba wa familia hiyo, Alex Mpaja(44) aliyelazwa wodi namba mbili katika
Hospitali ya Mkoa wa Rukwa, ambaye pia ni Mratibu Elimu, Kata ya Kasanga aliiambia Mwananchi kuwa mafuta hayo yalikuwa kwa ajili ya shughuli za kuhamasisha kilimo.
Mpaja alisema kiasi cha lita 67 zilikuwa mali ya serikali na zilizobaki zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya pikipiki yake.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Saduni Kabuma alisema kuwa hospitali hiyo ilimpokea majeruhi wa ajali hiyo mmoja akiwa katika hali mbaya ambaye alikuwa ameungua mwili wote kasoro uso tu.
Alimtaja kuwa ni Bahati Mpaja(9) na kuongeza kuwa alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
Mganga huyo alisema kuwa maiti tatu zilipokewa hospitalini hapo kutoka Kituo cha Afya Ngorotwa, ikiwamo ya Asha John (36)ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi tisa
Aliwataja wengine waliokufa kuwa ni, Dorah Mpaja(12), Atupele Mpaja(6), ambao wote walikuwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisumba na kuongeza kuwa Alex Mpaja amehamishiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi