Na Mwandishi Wetu
Serikali ya Tanzania imeendeleza kampeni yake ya kuhakikisha inafikia azma yake ya kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki bila ya kujali maoni ya wananchi, licha ya kutumia fedha nyingi katika kuyakusanya.
Serikali kwa sasa inakusanya maoni ya kama kuna haja ya kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki, kazi inayofanywa na Kamati inayoongozwa na Profesa Samuel Wangwe, inatarajiwa kufikia kiasi cha Sh2.8 bilioni hadi itakapomaliza ukusanyaji maoni, huku ikiwa imetangaza zoezi la kusaka wimbo wa shirikisho hilo.
Kwa upande wake, Kamati ya Wangwe inaendelea kupata upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi katika sehemu mbalimbali nchini, ambao ama hawataki shirikisho au kulikubali, wakiomba liwepo miaka mingi ijayo, uzinduzi wa wimbo wa taifa unaonyesha kuwa shirikisho hilo ambalo mikataba yake ilishapitishwa na viongozi wa juu wa serikali, haliwezi kwa njia yoyote kukwamishwa na maoni ya wananchi.
Serikali tangu awali iliamua kutumia nguvu katika kujiingiza kwenye ushirika huo wenye lengo la kuunda taifa la Afrika Mashariki bila ridhaa ya wananchi wake.
Kwa mfano, baadhi ya watu waliozungumza na Mwananchi Jumapili wanahoji kuundwa kwa Bunge la Afrika Mashariki lenye makao yake jijini Arusha, kisha kupisha mkataba wa soko huru kwa nchi hizi ambao haujafikiwa, sasa mkataba unaotaka kuwepo kwa shirikisho la kisiasa.
Wasiwasi wa wananchi ni kutokuwa tayari kwa serikali yao kuwahusisha katika kila hatua zinazochukuliwa, mambo ambayo yamekuwa hayafanyiki huku serikali yao ikitumia fedha nyingi kugharimia uratibu wa shughuli hizo.
Katika kuonyesha kuwa serikali tayari imeshaamua kuwa wananchi watake wasitake lazima shirikisho la kisiasa lifikiwe katika muda ambao serikali tatu za Kenya, Tanzania na Uganda zinataka, wananchi hao walieleza kuwa ndio maana wiki jana hatua zimeanza katika kunadi nyimbo kadhaa ili mmoja utumike kama wimbo wa taifa litakaloundwa ifikapo 2013.
Nchini Tanzania, harakati za kunadi nyimbo sita zilitangazwa wiki hii na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib.
Katika hafla hiyo, waziri huyo aliwataka Watanzania kusikiliza nyimbo hizo zitakazokuwa zikipigwa katika vituo mbalimbali vya redio na kisha kutoa maoni yao kuhusu wimbo upi wanaupenda.
Zoezi la uchaguzi wa nyimbo linamaanisha kuwa kazi ya kuundwa taifa la Afrika Mashariki inaelekea mwisho wake.
Serikali, kwa upande wake inajionyesha wazi kuwa imedhamiria kufanya lile ililoamua kulifanya hata kama kamati ya Wangwe itatoka na maoni yanayopingana na kile inachokitaka serikali.
Kuanzia mwanzo, wakati kamati ya Wangwe ilipoanza kukusanya maoni, wananchi wengi waliojitokeza wamekuwa wakipinga kitendo cha kamati hiyo kuanza kutoa majibu ya wachangiaji badala ya kukusanya kile kinachotolewa.
Mara kadhaa iliripotiwa katika vyombo vya habari kuwa wajumbe wa kamati ya Wangwe walikuwa wakitoa majibu kwa wananchi, hasa wale walioonekana kupinga shirikisho.
Kitendo hiki kimekuwa kikitafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini, kama lengo la kuhakikisha kamati hiyo inapata mawazo yanayokubaliana na shirikisho hilo kuwepo kwa mujibu wa ripoti ya Wako.
Profesa Wangwe licha ya mara kwa mara kuulizwa na waandishi kuhusu tabia hiyo ya kamati yake na pia kama kamati hiyo imebeba agenda ya siri, hakupinga wala kukubali na badala yake akawaacha wajumbe wa kamati yake kuendelea na utaratibu huo ulio kinyume na kazi yao ya awali iliyotangazwa kwa umma.
Kuna dhana ya wazi kuwa serikali kwa kutumia mbinu zake itawapeleka Watanzania katika shirikisho hilo licha ya kuwa nchi hiyo ndiyo inaonekana kuwa katika hasara zaidi ukilinganisha na majirani zake, Kenya na Uganda.
Zoezi hili la kuwataka wachague wimbo wa taifa la Afrika Mashariki ni kama linapigilia msumari katika maamuzi ya serikali na ili Watanzania waepuke kunahitajika nguvu ya vyombo vingine kama vile Bunge.
Kwa wafuatiliaji wa mfumo wa uendeshaji wa Bunge la Tanzania, kuna walakini mkubwa kuhusu uwezo wa bunge hilo hilo linaloongozwa na CCM kuweza kukataa Tanzania isiingie katika shirikisho kama serikali Kuu itataka ifanyike hivyo kama inavyojionyesha.
Matukio kadhaa yanaonyesha kuwa bunge hilo limeamua kupitisha maamuzi kwa misingi ya kichama zaidi kuliko kutazama nafasi ya taifa na ushirikishanaji wa wananchi.
Hivi karibuni Jaji Joseph Sinde Warioba alizungumzia ukiukaji wa sheria kwa kuundwa kwa Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki kulikofanywa na marais wa nchi hizi.
Badala ya kusikiliza ushauri wake, Bunge la Tanzania likaridhia jambo ambalo linaashiria pia kuwa kuna agenda ya siri katika kufanikisha shirikisho hili.
Hii inaweza kuwa hatari nyingine, Watanzania kuingia katika shirikisho kwa sababu ya agenda za siri za viongozi wao. Athari hii inaweza kufanya shirikisho hili lisidumu kama ilivyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliyokufa mwaka 1977.
Wananchi mbalimbali waliozungumza na gazeti hili wanaeleza kuwa, wananchi wana hofu na viongozi wa nchi hizi kama wanaweza kukabili kuongoza taifa kubwa huku wakiwa wameshindwa kuyapeleka mbele kimaendeleo mataifa yao ya sasa, wakati huu yakiwa bado madogo kwa umbo na mahitaji.