JUZI, ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, walihitimisha vituko walivyoanza navyo wiki kadhaa zilizopita kwa kufanya vurugu kubwa katika eneo la Mahakama Kuu Tanzania.
Ndugu na jamaa hao wa Ditopile ambaye alikuwa katika mahabusu ya Keko tangu Novemba mwaka jana, wakilindwa na polisi waliokuwa katika sare na mavazi ya kiraia, walianzisha vurumai kubwa kuwazuia wanahabari kumkaribia au kumpiga picha mwanasiasa huyo ambaye alipewa dhamana.
Vurugu hizo ambazo zilisababisha waandishi kadhaa kujeruhiwa na wengine kuharibikiwa vitendea kazi vyao, zikiwamo kamera, ziliambatana na uamuzi wa makusudi na kibabe wa jamaa hao wa Ditopile kurusha ngumi na kuwapiga vichwa na mateke wapiga picha waliokuwa wakijaribu kumpata ndugu yao ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akificha sura yake kwa kofia kubwa aina ya pama.
Matukio hayo yalikwenda sambamba na maamuzi ya kidhalilishaji ya watu hao kuwamwagia maji wanahabari na kutoa maneno ya kuidhalilisha kwa serikali na hata viongozi wake wakuu.
Gazeti hili katika toleo lake la jana liliwaelezea ndugu hao wa Ditopile kuwa ni watu wasio na staha, walioshindwa kujiheshimu, wapungufu wa hekima, waliokosa subira na walioamua kwa makusudi kuidharau mahakama na taaluma ya habari.
Lakini si hilo tu, ndugu na jamaa hao wa Ditopile ambao kimsingi walipaswa kuonyesha vitendo vya kuguswa na pengine kuhuzunishwa kweli kweli na shauri baya linalomkabili ndugu yao, waliamua kuuthibitishia ulimwengu kuwa hulka zao zilikuwa zikitawaliwa na ujinga uliovuka mipaka ya kushindwa hata kuelewa maana ya mahakama na ulazima wa wao wa kutii mamlaka za dola.
Tukio hilo la kufedhehesha lilisababisha mpiga picha wa gazeti hili, kukumbwa na zahama hiyo ambayo ilimsababishia majeraha kutokana na kujikuta akipigwa na mmoja wa watu hao wakati akiwa katika harakati za kupiga picha na kumnusuru mwenzake ambaye alikuwa ameangushwa chini na majahili hao.
Kwa maneno rahisi, matendo hayo ya kishenzi ambayo yamelaaniwa tayari na watu na taasisi mbalimbali zinazothamini uhuru wa habari, yameharibu kabisa hisia za huruma na za kumuombea heri ndugu yao ambaye wajihi wake wa siku za mwanzo mahakamani ulikuwa ukionyesha sura ya wazi ya namna alivyokuwa akiguswa na tukio zima lililomfikisha hapo.
Kutokana na hilo, basi tunapenda kuchukua fursa hii kuwalaani ndugu na jamaa hao wa Ditopile, na wakati huo huo kuvitaka vyombo vya usalama kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine na vurugu hizo.
Wakati tukisema hayo, tunapenda kueleza bayana kwamba, kauli ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, kutamka tu kuwaomba radhi wanahabari na mahakama haitoshi.
Badala yake, Jeshi la Polisi linapaswa kuwasiliana na vituo vya televisheni vilivyorekodi vurugu zile na kuwatumia wanahabari waliokuwa eneo hilo ili kuwanasa wale wote walioshiriki kati vurugu zile na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria, ili liwe fundisho kwa wengine wote wasioheshimu mahakama zetu na taaluma muhimu ya habari.
Aidha, jamaa na ndugu hao wa Ditopile wanapaswa kubeba gharama za matibabu ya wanahabari waliojeruhiwa kutokana na vurugu zao, sambamba na kufidia gharama za vifaa vyao vilivyoharibiwa