Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Luteni (Mstaafu) Yusuf Makamba aliyeteuliwa na Rais kuwa Mbunge wiki iliyopita, ameapishwa rasmi leo asubuhi.
Mzee Makamba alikula kiapo saa 3:10 kabla ya kipindi cha maswali na majibu.
Mbunge huyo mpya alisindikizwa na wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam wakati anatinga ndani ya nyumba.
Pia nje kulikuwa na wawakilishi wawili kutoka Jijini Dar es Salaam waliotumwa rasmi kuleta mashada ya kumpamba.
Wawakilishi hao mmoja ametoka katika ofisi yake ya mkoa wakati mwingine ametoka Kinondoni.
Wakati huohuo teknolojia katika ukumbi mpya wa Bunge ilileta gozi gozi tena kiasi cha ’maiki’ kushindwa kufanya kazi.
Kwa mtaji huo, muuliza swali alilazimika kuhamia sehemu wanayosimama mawaziri ili aweze kusikika.
Tatizo hilo liliathiri pia watalaam wa kurekodi kumbukumbu za Bunge na mjadala unaoendelea Bungeni.
Hadi tunakwenda mitamboni, tatizo hilo lilikuwa linaendelea kutafutiwa ufumbuzi.