Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kampeni chafu zaanza uchaguzi mdogo Tunduru
Kampeni chafu zaanza uchaguzi mdogo Tunduru
By Habari Tanzania | Published  03/10/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Muhibu Said

MBIO za kuelekea uchaguzi mdogo wa Mbunge katika Jimbo la Tunduru, zimeingia katika  sura mpya, baada ya watu wasiojulikana kuanzisha kampeni chafu dhidi ya wagombea wa Chadema, CCM na viongozi wa kitaifa wa vyama hivyo.

Kampeni hizo chafu zilizoanza jana, zinaendeshwa na watu hao kupitia waraka uliosambazwa katika maeneo mbalimbali ya mjini na vijijini wilayani hapa.

Wanaoshambuliwa na waraka huo ambao Mwananchi ina nakala yake, ni pamoja na mgombea wa CCM, Mtutura Abdallah na wa Chadema, Shaibu Akwilombe.

Viongozi wa kitaifa wa CCM wanaoshambuliwa na waraka huo, ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho (bara), John Malecela na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba.

Uongozi wa CCM na Chadema kwa nyakati tofauti, wamekihusisha Chama cha Wananchi (CUF) na waraka huo wakidai ndicho kilichouandaa na kuusambaza.

Kwa upande wake, CUF kimekanusha kuhusika kwa namna yoyote na waraka huo wenye kichwa: "Alaa Kumbe."

Waraka huo unahoji sababu za Mtutura kuomba ubunge Tunduru badala ya Newala mkoani Mtwara, ambako anadaiwa kuwa amezaliwa.

Pia unawataka wapigakura kutomchagua Akwilombe kwa madai kwamba kufanya hivyo kutazigawa kura za upinzani na kumpa ushindi Mtutura.

"Alaa Mtutura anaomba ubunge Jimbo la Tunduru badala ya kuomba jimbo la Newala. Kumchagua Akwilombe ni kuzigawa kura za upinzani na kumpitisha Mtutura," unasema waraka huo.

Umeongeza; "vigogo wa CCM wanatoa fedha katika kampeni hii badala ya kuomba kura kwa ahadi za kimsingi kwa wapiga kura...kampeni ya CCM wazawa (wayao) hawathaminiwi kwenye misafara yao badala yake wanang'ara akina Malecela na Makamba ambao wanaropoka tu majukwaani bila kujali matatizo ya msingi ya Tunduru kama vile bei ya korosho.

"Mtutura anaonekana muhimu sana ndani ya CCM kuliko wananchi wenyewe, kiasi CCM inatumia mamilioni ya shilingi ambayo yangeweza kutumika kununulia dawa n.k. Kwa mantiki hii gharama hizi zinazotumika kumtangaza zitalipiwa na  nani?" Unasomeka waraka huo.

Waraka huo umeendelea; "Kumchagua Mtutura ni kuzidi kukaribisha matatizo na umasikini hapa Tunduru kwa  sababu Mtutura hatakuwa na uwezo wa  kuhoji jambo lolote linalohusu matatizo ya wana Tunduru kwa sababu wanaompigia debe ndio wanaosababisha hali hii iliyopo sasa.

"Magari ya fahari zaidi ya 20 yenye thamani ya zaidi ya Sh3.6 bilioni hapa Tunduru, maafisa mbalimbali zaidi ya 100 wanalipwa posho si chini ya Sh75,000 kwa  siku, muda wa siku 26, mafuta yanayotumika katika magari haya yanagharimu fedha nyingi, gharama hizi zitalipwa na nani? Wayao?" unahoji waraka huo.

Alipoulizwa kuhusu waraka huo, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi cha CCM, ambaye pia ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM, Matson Chizi, alikiri kuuona na akasema hizo ni propaganda za kisiasa zinazoenezwa na CUF.

Chizi alisema propaganda zisizokuwa na tija hazina msingi katika maendeleo ya wananchi. "CCM haitatumia propaganda chafu, bali itatumia kampeni za kiungwana na  hoja sahihi kwa wananchi ili mgombea wake aweze kuchaguliwa tena kwa kura nyingi," alisema.

Katibu wa Chadema Wilaya ya Tunduru, Mwindadi Saidi, alisema waraka huo una kila ishara kuwa ama umeandaliwa na wanachama, viongozi au mashabiki wa CUF.

"Aliyeandika waraka huu hajazingatia suala la wanachama na uchaguzi, haelewi kura za wapinzani zinaweza kupatikana kutoka kwa wafuasi wa vyama mbalimbali," alisema Saidi.

Lakini Katibu wa CUF Wilaya ya Tunduru, Rashid Mchileka, alisema wanaokihusisha chama chake na waraka huo hawawezi kuthibitisha madai yao kwa kuwa waraka huo hauna nembo, saini wala alama  yoyote inayoonuesha kuwa umeandaliwa na CUF.

Vyama vinavyoshirini uchaguzi huo utakaofanyika Machi 18, ni CCM, CUF, Chadema, UDP na DP.

Katika tukio jingine, jana wafuasi wa watatu  Chadema walifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo kwa tuhuma za kumpiga na kumchania fulana ya kampeni, yenye  thamani ya Sh30,000 mwanachama wa CCM katika Kijiji cha Majimaji wilayani hapa.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jana, Hakimu wa Mahakama hiyo, Amina Chungulu, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Abdallah Suleiman (24), Sued Hassan (26) na Yasin Simba (24), wote wakazi wa kijiji hicho.

Hakimu Chungulu alisema watuhumiwa wanadaiwa kumfanyia mambo hayo Rashid Omar Machi 7, 2007 saa 2.00 usiku kujijini hapo.

Hata hivyo, alisema watuhumiwa hao wapo nje kwa dhamana na kesi yao itatajwa Machi 21, mwaka huu. Mlalamikaji jana hakufika mahakamani.

Vumbi hilo likiwa halijatua, wafuasi wa CUF, wamempa kipigo mwananchi ambaye hakufahamika mara moja baada ya kutuhumiwa kumkashifu Katibu Mkuu wao, Seif Sharif Hamad.

Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Mbesa wilayani hapa ambapo mgombea wa  CUF, Mazee Rajab alikuwa akifanya kampeni. Mwanakijiji huyo ambaye aliokolewa na mgambo, anadaiwa kuandika  kwenye ubao wa shule ya msingi maneno ya matusi dhidi ya Maalim Seif na kwamba CUF ni chama cha Waarabu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.