Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Madaktari mikoani Tanzania walia njaa
Madaktari mikoani Tanzania walia njaa
By Habari Tanzania | Published  03/10/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Ramadhan Semtawa

WATAALAM wa afya 3,150 wakiwemo madaktari waliopelekwa kwenye halmashauri mbalimbali za wilaya nchini tangu Desemba 6, mwaka jana, wako katika hali mbaya kutokana na kutolipwa mishahara yao hadi sasa.

Idadi hiyo iliyojazwa ni kati ya nafasi 3,680 ambazo zinatakiwa kujazwa na watalaamu hao nchini kote. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mizengo Pinda, hakukubali wala kukataa kutolipwa kwa watumishi hao, lakini alithibitisha watalaam hao wa afya kupelekwa mikoani na wilayani kujaza nafasi hizo.

Pinda alifafanua zaidi kwamba atafuatilia kwa karibu kuona jumla ya wataalam waliopelekwa mikoani na wilayani ambao hawajalipwa na halmashauri zao.  

“Nitalifuatilia kwa karibu, nataka kuona ni wataalam wangapi na kutoka halmashauri zipi nchini hawajalipwa mishahara yao,” alisema Pinda na kuongeza;

“Utaratibu wa sasa si kama ule wa kutangaza nafasi za kazi, kuona kama kweli waombaji wana sifa, hakuna sababu za kuchelewa zaidi kwa mishahara ya watumishi na kuingizwa katika mfumo wa kompyuta.”

Kwa mujibu wa Pinda, serikali iliamua kuondoa utaratibu wa zamani wa kutangaza nafasi za kazi na kuanza kuchukua wahitimu wa mafunzo ili kuziba pengo la uhaba wa wataalam hao hivyo ni lazima walipwe mishahara kwa wakati.

Taarifa za ndani kutoka kwa baadhi ya ndugu wa wataalam hao zinasema kutokana na kutolipwa mishahara tangu waanze kazi, watalaam hao wanaishi maisha magumu, wengi wakitegemea misaada kutoka kwa ndugu zao.

Wataalamu hao ni pamoja na maafisa uuguzi, wauguzi, madaktari wa magonjwa ya binadamu na maafisa tabibu.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimethibitishwa na mmoja wa afisa wa juu wa Wizara ya Afya zinasema wataalamu hao huenda wakachelewa kwa zaidi ya mwezi mmoja zaidi kuingizwa katika mfumo wa malipo ya kompyuta.

“Jinsi ninavyofahamu mimi, miezi miwili  kutoingizwa katika mfumo wa kompyuta si mingi sana, inaweza kwenda hadi miezi minne,” alisema afisa huyo.

 Alisema uzoefu unaonyesha sababu za kuchelewa kuingizwa katika mfumo wa malipo wa kompyuta zinalenga kupata taarifa za kina za wataalam hao, kwani mara nyingi wanapopelekwa katika vituo vijijini huwa wanarudi mijini.

Pinda akizungumzia zaidi suala hilo, alisema atalishughulikia kwa karibu kuona sababu za msingi za kuwepo hali hiyo.

Alisema ingawa wakati mwingine inawezekana mtumishi akachelewa kuingizwa katika mfumo wa kompyuta kutokana na kutaka taarifa zake za kina, lakini chini ya utaratibu wa sasa, hakuna mlolongo mrefu unaoweza kusababisha wataalam hao kucheleweshewa mishahara yao.

Chini ya utaratibu wa sasa, wataalam, wakiwamo walimu, hupelekwa katika vituo vya kazi kutokana na maombi ya halmashauri kwenda katika wizara husika kwa kuzingatia upungufu uliopo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.