Na Jonas Songora
SERIKALI za Tanzania na Japan jana zilitialiana saini mikataba ya mikopo na msaada itakayogharimu jumla ya Sh102.4 bilioni.Utiaji saini huo wa mikataba mitatu tofauti, ulifanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha, ambako Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gray Mgonja, alitia saini kwa upande wa Tanzania na Balozi wa Japan nchini, Makoto Ito, akiiwakilisha nchi yake.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini huo, Mgonja alisema mkopo wa muda mrefu wa Yen 600 milioni za Japan, sawa na Sh6.5 bn za Tanzania, utatatumika moja kwa moja katika Mpango wa Kupunguza Umasikini nchini (Mkukuta), fedha ambazo zitaingizwa katika bajeti ya serikali katika mwaka ujao wa fedha.
Aliongeza kuwa mkopo wenye masharti nafuu wa Yen 2 bilioni (karibu sawa na Sh21.7 bilioni) zimetolewa kupitia mfuko wa kusaidia kupunguza umasikini (PSRC) na kufadhiliwa na Benki ya Dunia.
Kati ya fedha hizo, sh74.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutengeneza barabara ya Arusha - Namanga. Mgonja alisema barabara hiyoi mepewa umuhimu mkubwa ikizingatiwa kuwa karibu asilimia 20 ya bidhaa zinazosafirishwa na kuingia nchini kutoka Kenya hupitia barabara hiyo itakayojengwa kwa kiwango cha lami.
"Barabara hii itaimarisha uchumi wa nchi na pia kuongezea kipato kwa wakazi waishio kando ya barabara hiyo," alisema Mgonja.
Balozi wa Japan nchini aliyefuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Japan ya Maendeleo ya Dunia, Koji Tanami, aliahidi nchi yake kuendelea kutoa misaada na mikopo kwa serikali ya Tanzania kutokana na usimamizi mzuri wa fedha hizo.
Hata hivyo alisema serikali yake itasimamia kwa karibu matumizi ya fedha hizo ili ihakikishe kuwa zinatumika kama makubaliano yanavyoanisha na si vinginevyo.