Na Waandishi Wetu
WANAHARAKATI na watu kutoka taasisi mbalimbali, wamelaani vikali vitendo vya vurugu vilivyofanywa na watu wanaodhaniwa kuwa ni ndugu wa Mkuu wa zamani wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri kwa waandishi wa habari katika Mahakama Kuu Dar es Salaam juzi.
Kauli hizo zimekuja siku moja baada ya watu hao kuwapiga, kwamwagia maji na kuwazuia waandishi wa habari waliokuwa mahakamani hapo kufanya kazi yao.
Katika taarifa yake, Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (Misa-Tan), imelaani vitendo hivyo ilivyoviita vya kihuni na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na hatimaye kuwachukulia hatua watakaobainika kufanya vurugu hizo.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Ayub Rioba, ilisema waandishi wa habari hawakuwepo mahakamani kuamua kesi au kumhukumu mshtakiwa, bali walikuwa wakitekeleza majukumu yao kama desturi ilivyo inapotokea mahakama kuwa na kesi yenye mvuto na maslahi kwa jamii.
"Tunashindwa kuelewa madhumuni hasa ya ya watu hao wanaodhaniwa ndugu wa mshtakiwa kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa kazini kupata habari ambazo Watanzania wote wana haki ya kuzipata," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa jamii ilitarajia ndugu hao kuwa na mwenendo wa kiungwana na majuto, lakini jeuri na tambo zao kama zilivyoripotiwa katika vyombo vya habari, zinaweza kujenga picha katika jamii kuwa hata mshtakiwa mwenyewe ana hisia kama za ndugu zake.
Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia nchini (DP) kimetishia kufungua kesi ya jinai dhidi ya Jeshi la Polisi kama litashindwa kuwachukulia hatua watu wote waliohusika kufanya vurugu na kusema kuwa vitendo vilivyofanyika ni kuidharau mahakama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Saalaam, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, alisema anaamini baadhi ya waliokuwa wakifanya vurugu hizo ni askari polisi waliovaa kiraia na akaonyesha wasiwasi wake juu ya askari hao kutochukua hatua yoyote kuwazuia ndugu wa mshtakiwa.
Alisema kupitia picha za televisheni, ameweza kuwabaini baadhi ya askari walioshiriki katika vurugu hizo na kusema yupo tayari kutoa ushahidi mahakamani dhidi yao.
Nayo klabu ya Haandishi wa Habari wa Dar es salaam (DCPC), imeelezwa kusikitishwa kwake na kitendo polisi waliokuwa mahakamani kushindwa kudhibiti vurugu walizofanyiwa waandishi wa habari.
Katika tamko lake kwa vyombo vya habari, lililosainiwa na Mwenyekiti wake, John Mapinduzi, klabu hiyo imeonyesha mashaka makubwa juu ya mustakbali wa vyombo vya habari na utendaji wake hapa nchini.
Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) kilisema vitendo vya aibu vilivyofanywa na polisi na ndugu wa mshtakiwa mahakamani juzi ni uthibitisho wa kiwango cha juu cha dharau kwa mahakama na mmomonyoko wa misingi ya utawala wa sheria nchini.
Mwenyekiti wa LHRC, Hellen Kijo Bisimba, alisema katika taarifa yake kuwa ni aibu kwa chombo kinachoaminika kama polisi kutenda kitendo kinachoidhalilisha heshima ya mahakama.
"Hii si tu ni kudharau mahakama, bali pia ni uthibitisho wa kiwango cha juu cha kutoogopa mamlaka na kumomonyoka kwa misingi ya utawala wa sheria," alisema.
Wakati huo huo, Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeelezea kusikitishwa na kitendo cha kupigwa kwa waandishi hao na kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema, kuwachukulia hatua kali askari polisi waliohusika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Katibu Mtendaji wa MCT, Anthony Ngaiza, alilitaka jeshi hilo pia kutoa maelezo ya kina pamoja na kuomba radhi kutokana na kitendo hicho alichokielezea kuwa ni mlolongo wa vitendo vibaya dhidi ya waandishi wa habari ambavyo wamekuwa wakitendewa na ndugu wa Ditopile, huku polisi wakiona na kukaa kimya, bila ya kuchukua hatua yoyote.
“Matukio ya jana (juzi) yamekuwa ni mlolongo wa vitendo ambavyo wamekuwa wakifanyiwa waandishi wa habari na jamaa wa Ditopile tangu aanze kufikishwa mahakamani, bila kupata usaidizi wowote kutoka kwa polisi,” alisema Ngaiza.
Alifafanua kuwa hali hiyo imekuwa ikiwafanya waandishi wa habari watende kazi zao katika mazingira yenye mashaka kwa usalama wao.
Ngaiza alisema jukumu la polisi lilikuwa ni kulinda amani hasa ukizingatia mahakamani ni sehemu nyeti inayopaswa kuheshimiwa, lakini kinyume chake waliendeleza vitendo vya kihuni ambavyo vilikuwa vinatendeka tangu kesi hiyo ilipokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Ngaiza alikielezea kitendo hicho kama ni doa katika mahusiano mazuri ya utendaji wa kazi kati ya Jeshi la Polisi na baraza hilo, ambayo yalikuwa yamekwishaimarika.
“Wakati Baraza na Jeshi la Polisi vimekuwa katika harakati za kujenga uhusiano mzuri wa utendaji wa kazi, limesikitishwa kuona vitendo ambavyo polisi wanashiriki katika kuzuia waandishi wa habari wasifanye kazi zao na kuwalinda wanaowanyanyasa na kuwafanyia fujo,” alilalamika Ngaiza.
MCT lilisisitiza kwamba habari ni haki ya kila raia na kamwe halitavumilia vitendo vyovyote ambavyo vitafanywa na ama na raia au taasisi yoyote ile ya kuwanyima wananchi haki hiyo kwa nia ya kulinda maslahi ya mtu au kikundi cha watu.
Ngaiza aliahidi kuwa MCT itashirikiana na taasisi nyingine zinazotetea haki ya jamii kuhakikisha kuwa waandishi waliojeruhiwa wanapata haki zao ikiwa ni pamoja na mali zilizopotea.
Kwa upande mwingi baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam, wamelaani vurugu zilizofanywa na ndugu wa Ditopile mahakamani juzi wakati ndugu yao alipoachiwa kwa dhamana.
Vile vile wananchi mbalimbali wakazi wa Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti walikieleza kitendo hicho kuwa kimekosa ustaarabu na kinatakiwa kulaaniwa.
“Kutokana na kitendo kile, ni vyema serikali iingilie kati ili waone kuwa serikali ni serikali, madaraka ni madaraka na mtuhumiwa ni mtuhumiwa na ni lazima sheria za mahakama ziheshimiwe.
"Wasijione kuwa nchi hii ni yao kwani wapo watu wengi gerezani kwa muda wa miaka 10 kwa tuhuma za mauaji bila ya kesi zao kusikilizwa lakini ndugu zao hawafanyi fujo,” alisema kwa uchungu mwanachi mmoja aliyefika katika ofisi za Mwananchi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Mahakama Kuu ya Tanzania, juzi zilizuka vurugu kubwa baada ya ndugu na jamaa wa Ditopile kuwashambulia waandishi wa habari kwa ngumi, mateke na kuwamwagia maji, wakiwazuia wasimpige picha ama kumhoji ndugu yao kabla ya kuingia na baada ya kutoka mahakamani hapo.
Inadaiwa kuwa pamoja na vurugu hizo kufanywa mbele ya askari polisi waliokuwa wamejaa mahakamani hapo, hawakuchukuwa hatua zozote kuzuia hali hiyo na badala yake baadhi yao walishiriki katika vurugu hizo
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limewaomba radhi waandishi wa habari na Mahakama Kuu kutokana na vurugu vurugu hizo.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alferd Tibaigana, alisema kutokana na vurugu hizo, Jeshi la Polisi limefungua faili la kesi huku likifanya uchunguzi ili askari na watu wote watakaobainika walisababisha vurugu hizo, waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Hata hivyo, pamoja na Tibaigana kuomba radhi kwa tukio hilo, aliwatetea askari wake kuwa wakati wakifanyakazi zao walishindwa kutofautisha ndugu wa Ditopile na Waandishi wa habari.
Alisema kutokana na watu wengi waliojitokeza mahakamani, polisi walipata wakati mgumu wa kuwadhibiti watu waliofanya vurugu hizo.
“Waandishi wa habari walikuwa wengi mno na wengi wao hawana alama maalum ya kuwatofautisha na ndugu zake Ditopile. Katika hali kama hiyo polisi walishindwa kufanyakazi yao ya kuwalinda waandishi dhidi ya ndugu zake Ditopile,” alisema Tibaigana.
Wakati Tibaigagana akitoa utetezi huo, watu walioshuhudia sakata hilo la juzi, walisema si kweli kuwa polisi hawakuwatambua waandishi wa habari, bali walichofanya ni kuungana na ndugu wa Ditopile kuwashambulia waandishi kwa makusudi wakati mwingine kwa kutumia vitako vya bunduki.
Watu hao walisema ilikuwa ni rahisi kwa polisi kuwatambua waandishi wa habari kwani wengi wao walikuwa wamebeba zana zao za kazi kama kamera, daftari ndogo za kuchukulia habari na vitendea kazi vingine.
“Polisi walikuwa wakiwazuia wapiga picha za televisheni kwa makusudi na wakati mwingine waliwapiga kwa vitako vya bunduki na cha kushangaza zaidi ni kitendo chao kuwaangalia tu ndugu wa Ditopile wakiwapiga na kuwamwagia maji waandishi wa habari bila ya kuwachukulia hatua,” alisema mwananchi mmoja aliyekuwepo katika eneo la tukio.
Akizungumzia tukio la askari polisi kumpitisha Ditopile katika unaotumiwa na majaji, Tibaigana, alisema kutokana na vitendo vilivyofanywa na ndugu wa Ditopile siku za nyuma, maafisa wa polisi waliokuwa wamemchukua mtuhumiwa huyo kutoka rumande, waliamua kumpitisha mahabusu huyo kwenye mlango wa nyuma wa jengo la mahakama badala ya mlango wa mbele.
“Kitendo hicho kimeleta usumbufu mkubwa kwa uongozi wa mahakama kwani mlango ule baadaye iligundulika kwamba hutumiwa na majaji tu wanapoingia na kutoka kazini. Tunaomba radhi kwa usumbufu huo na tumeanzisha uchunguzi ili tuweze kuchukuwa hatua za kinidhamu dhidi ya wote waliohusika,” alisema Tibaigana.
Kamishna huyo wa polisi, pia alilaani vurugu zinazofanywa na ndugu wa Ditopile mahakamani dhidi ya waandishi wa habari wanapokuwa kazini kwani jeshi la polisi lisingependa kuonyeshana ubabe na familia hiyo.
“Tatizo kubwa limetokea kwa ndugu wa Ditopile. Inaelekea walishafahamu kwamba ndugu yao atapata dhamana na ndiyo maana walikusanyika kwa wingi, kwa mbwembwe na kwa ubabe mkubwa na hivyo kusababisha mapambano kati yao na nyie waandishi wa habari.
“Katika hali ya kawaida, ningetegemea ndugu wa Ditopile kuwa katika hali ya utulivu na pengine wengi wao kubakia nyumbani wakiomba dua kwani si rahisi kufahamu mahakama ingeamua vipi.
"Natoa onyo kwa ndugu zake kwa vitendo vya ubabe walivyokwisha kuvionyesha mbele ya umma hadi sasa. Sitegemei kwamba kesi yake itakapopangwa kusikilizwa kuwepo na sababu za upande wa serikali kuomba wapigwe marufuku na mahakama kuwazuia wasikilize kesi ya ndugu yao.”