Kama Serikali haitaleta zile hadithi za mgema akisifiwa, basi huenda ajira nchini zikawa nje nje kama alivyoahidi Rais wa nchi, Bwana Jakaya Kikwete.
Kundi la kwanza kunufaika na ajira hizo ni wahitimu wa kidato cha sita waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza hadi la tatu.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Margreth Sitta aliwaambiwa wabunge jana kuwa wasomi hao watapelekwa kwenye ualimu wa Sekondari ili kufidia upungufu wa walimu nchini.
Akasema Serikali katika mkakati wake huo wa kupambana na upungufu huo wa walimu itawapa mafunzo ya mwezi mmoja wahitimu hao ili waweze kufundisha.
Akasema chini ya mpango huo walimu 3,500 wataajiriwa na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa walimu.
Akasema walimu hao baada ya mafunzo ya mwezi mmoja watapatiwa cheti chenye hadhi ya diploma na ifikapo mwezi Agosti mwaka huu watakuwa darasani wakifundisha.
Amesema Serikali imetenga Sh. Bilioni 8 kwa kazi hiyo ambayo itafanywa katika vyuo saba vya Butimba (Mwanza), Mtwara, Morogoro, Monduli (Arusha), Tabora, Tukuyu (Mbeya) na Korogwe (Morogoro).
Aidha akasema Serikali chini ya mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondali, MMES itawapatia ajira walimu 3,207 wenye stashahada kutoka vyuo mbalimbali.
Pia akasema itachukua wahitimu 500 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao watakuwa tayari kufundisha na kuwapa ajira.
Waziri huyo ameongeza kuwa pia Serikali itaingia mikataba mipya na walimu waliostaafu ambao bado wana uwezo wa kufundisha warudi madarasani na kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa walimu.
Uhaba mkubwa wa walimu katika shule za Sekondari umeibuka baada ya kuanzishwa kwa mpango MESS ambapo shule nyingi zimejengwa na kusajili wanafunzi hivyo kukosa walimu wa kukidhi mahitaji.
Tatizo hilo likakomaa baada ya Waziri Mkuu kuagiza wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kukosa nafasi za Sekondari wapewe nafasi hizo.
Katika kampeni zake kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka jana Rais Kikwete aliwaahidi Watanzania kwamba atazalisha ajira miliono moja katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.