Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Ajali haina kinga, lakini inaepukika
Ajali haina kinga, lakini inaepukika
By Habari Tanzania | Published  03/9/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

AJALI haina kinga. Msemo huu ni kawaida kutamkwa na watu wengi, hasa inapotokea ajali.

Kwa namna moja ama nyingine, msemo huu umelemaza akili za wengi, kwani hata kama ajali inapotokea kwa uzembe wa dereva au uzembe wa serikali, bado jamii itaamini kuwa ajali haina kinga.

Sipingani na dhana kwamba ajali haina kinga, la hasha, lakini naamini kuwa ajali inaepukika.

Tanzania ni moja ya nchi zinazoathiriwa sana na ajali za barabarani, ambapo maelfu ya wananchi wakiwamo watoto wasio na hatia hupoteza maisha na mali zao kila mwaka kutokana na ajali.

Zipo ajali ambazo hazina kinga, lakini zipo zinazoweza kuepukika kama madereva wangekuwa makini zaidi.

Yapo mambo mengi yanayosababisha kutokea kwa ajali hizi, na moja ya mambo hayo ni ulevi wa pombe, mirungi, bangi na hata aina nyingine ya dawa za kulevya.

Baadhi ya madereva hutumia aina mbalimbali ya kilevi kwa madai kuwa kinawasaidia kuwa macho muda wote, hasa wale madereva wa magari makubwa, na kuwaongezea umakini, dhana ambayo ni potofu.

Hata hivyo, jambo kubwa na lililowazi ni kwamba ajali nyingi zinatokana na uzembe.

Uzembe huo upo kuanzia serikalini. Wasimamizi wa sheria za usalama barabarani hawako makini kusimamia sheria hizo. Wanashuhudia mabasi ya abiria yanavyojaza kupita kiasi, wanashuhudia madereva wasio na leseni, wanashuhudia mabasi yakikimbia kwa mwendo kasi usiotakiwa, wanashuhudia mabasi yaliyolegeza vidhibiti mwendo, wanashuhudia mabasi mabovu ambayo yamechakaa kufanya safari, lakini yote wanayaachia kwa sababu tu ya kulambishwa ‘pipi’ na makondakta.

Hapa naongelea rushwa. Askari wengi wa usalama barabarani wanapokea rushwa, hilo halina ubishi, kwani tunaposafiri na mabasi hayo, tunaona mabasi yakisimamishwa kwa muda kwa makosa mbalimbali, lakini kondakta akishuka, huweka pesa kwenye gazeti na kuwaachia wahusika.

Kwanza, ni makosa kwa askari kuzungumza na makondakta kwenye vichaka au nyuma ya basi. Mambo hayo yanatia aibu na kichefuchefu.

Haya mambo yanafanyika na wizara husika zinajua, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa, na matokeo yake ajali zinazidi kutafuna nguvu kazi ya taifa. Huo ni uzembe mkubwa unaochangia ajali nyingi za barabarani.

Ukichukua mfano wa ajali za mara kwa mara za treni, hasa za Reli ya Kati, nyingi zinatokea kwa sababu ya uchakavu wa injini na barabara za reli hiyo.

Hivi sasa shirika hilo la TRC liko hoi, lakini serikali ipo, ikiendelea kushuhudia maafa. Huo ni uzembe kwani ni bora huduma ya treni hiyo ikikasimama.

Achilia mbali ajali za treni, ukija kwenye vivuko na usafiri wa majini hali ni mbaya zaidi. Vipo vivuko na vyombo vya usafiri wa majini ambavyo vimechakaa na vinahatarisha maisha ya wasafiri na mali zao.

Chukua mfano wa kivuko cha Kigamboni. Chukua mfano wa ajali mbaya ya meli ya mv Bukoba, yote hiyo ni uzembe.

Lakini serikali ipo, imetulia, inasubiri maafa yatokee ndipo ianze kuchukua hatua.

Uzembe mwingine ni wa madereva na wamiliki wa vyombo hivyo vya kusafiria.

Wamiliki wa mabasi wanapaswa kuhakikisha madereva wanaowapa dhamana wana sifa na elimu waliyoipata kwenye vyuo vinavyojulikana, lakini kwa sababu ya kuogopa kuwalipa gharama kubwa, huamua kuwaajiri madereva wasio na sifa. Huo nao ni uzembe.

Kwa upande wa madereva, hali ni mbaya zaidi. Wengi ni wazembe. Kama nilivyosema awali kwamba baadhi ni walevi na kutokana na ulevi huo, hawazingatii sheria za usalama barabarani.

Kutokana na ulevi huo, madereva wamekuwa wanapuuza sana alama za barabarani. Wanapuuza vipeperushi vinavyoeleza wazi kuwa usiendeshe wakati umelewa. Bado tunasema ajali haina kinga!

Lakini uzembe mwingine, tena mkubwa, uko kwa abiria wenyewe. Abiria wanashuhudia madereva wao wakienda mwendo kasi ajabu huku wakishindana na mabasi mengine, lakini hakuna anayethubutu kusema au kulalamikia hali hiyo, lakini wanalalamikia moyoni na ajali ikishatokea, kila mmoja hujitokeza kulalamika kuwa dereva alikuwa anakwenda kwa kasi kubwa. Nasisitiza tena kuwa kinga ya ajali ipo, lakini jamii haiko tayari kuitumia.

Abiria hao hao wanajua kabisa kwamba gari haliruhusiwi kujaza mafuta likiwa na abiria, lakini wanakubali basi walilopanda lijaze mafuta na wao wakiwamo.

Ajali ikitokea bado tunasema haina kinga!

Abiria wanashuhudia basi limejaa, hali hiyo hutokea hasa kwa daladala, lakini wako tayari kuingia na kujibana kiasi cha kushindwa kupumua kama vile hakuna mabasi mengine, lakini ajali ikitokea, wanakuwa wa kwanza kusema ajali haina kinga.

Kwa kifupi, abiria wengi ama ni waoga ama hawajui haki zao, ndiyo maana wakati mwingine wananyanyaswa na makondakta na madereva na wasijue la kufanya.

Watanzania tuondoe fikra kuwa ajali haina kinga.

Dhana au fikra hiyo, kwa namna moja inafanya ajali ziongezeke na madereva kushindwa kuwajibika kwa dhana kuwa hata kama ajali ikitokea, haina kinga.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.