Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali ifikirie upya tatizo la msongamano Dar
Serikali ifikirie upya tatizo la msongamano Dar
By Habari Tanzania | Published  03/9/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

DHAMIRA ya serikali ya kuondoa tatizo la msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam, sasa inaonekana kuwa ndoto za alinacha.

Kwamba serikali imekuwa na ndoto za kulitatua tatizo hili kwa muda mrefu, imepanga mipango na jinsi ya kuitekeleza, lakini kadiri siku zinavyokwenda mbele, mipango hiyo haitekelezeki na tatizo nalo linazidi kuongezeka.

Usumbufu unaosababishwa na tatizo la usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam, hasa wanaotumia usafiri wa jumuiya, ni mkubwa, lakini umekuwa sehemu ya maisha yao, hivyo wanalazimika kuuzoea.

Tatizo la usafiri, licha ya kuwa kero, pia linachangia kwa kiasi kikubwa kudumaza shughuli za maendeleo, pia nidhamu kazini.

Imekuwa kawaida kwa watumishi wa serikali na hata wale wa sekta binafsi kuchelewa kufika katika sehemu zao za kazi, sababu ya kuchelewa ikiwa ni tatizo la usafiri.

Kwa wale ambao bado wanatunza muda wa kufika ofisini asubuhi, kama ulivyopangwa kwa mujibu wa taratibu za kazi, hao ni wale waliohiari kujitesa, kuamka alfajiri kuwahi usafiri wa kuwafikisha kazini.

Hawa nao wanaishi ndani ya tatizo jingine, sehemu kubwa ya maisha yao imehamia katika sehemu zao za kazi, nyumbani wanaonekana kama wakimbizi, hii ni kwa sababu wanalazimika kuamka alfajiri kuwahi usafiri na wanarejea majumbani mwao usiku, kisa tatizo la usafiri!

Tumeandika baadhi ya kero wanazokutana nazo wakazi wa Dar es Salaam kutokana na tatizo la usafiri kwa makusudi, tukiamini kuwa zitawagusa na kuwazindua viongozi husika, ambao tunadhani hivi sasa hawaguswi na adha hii, kutokana na tofauti ya maisha ya Watanzania ilivyo sasa.

Sisi tunaamini kuwa, kama serikali ikiamua, inaweza kulitatua tatizo hili katika muda mfupi.

Tujiaminishe hivyo, kwa kutambua kuwa serikali ina uwezo wa kutafuta njia mbadala zitakazorahisisha usafili kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Jiulize, inawezekanaje, kwa serikali yenye uwezo wa kujenga kilomita 1,000 za barabara ambazo gharama yake inakadiriwa kufikia sh bilioni 500, kushindwa kutenga fungu la fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam?

Tunajua, serikali ina mpango wa kuleta mabasi ya abiria yaendayo kasi ili kukabiliana na tatizo hili, lakini hatuamini kama mpango huo utatekelezwa katika muda uliopangwa.

Hatuamini kwa sababu tangu mpango huu ulipotangazwa, umekuwa ukisogezwa mbele kila mara. Aidha, tuna shaka kama mpango huu utakuwa suluhisho la kudumu la tatizo hili.

Hilo linatokana na imani tuliyonayo kwamba magari yanayokusudiwa kuletwa, ni makubwa, yasiyofanana na barabara zetu, hivyo yanaweza kuwa chanzo kingine cha msongamano.

Tunapenda kuishauri serikali, igeuke na itazame mipango yake ya nyuma iliyoipiga teke, ambayo ingawa utekelezaji wake una gharama kubwa, lakini inaweza kuwa suluhisho la kudumu.

Tunakubaliana na serikali kwamba mpango wa kujenga barabara zinazopitisha magari juu, ni ghali, ingawa zinaweza kuondoa tatizo hili.

Lakini mpango uliowahi kutangazwa na Prof. Mark Mwandosya, wa kutumia njia ya reli au ya majini badala ya barabara, ndio pekee unaoweza kuondoa tatizo hili.

Tunasisitiza tena kuwa, inawezekana kujenga reli ikawa ni gharama kubwa, lakini tuna uhakika kuwa kama itajengwa, inaweza kuondoa kabisa tatizo la usafiri na msongamano wa magari jijini, kinyume cha kupanua barabara huku watu na magari wakizidi kuongezeka.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.