POLISI mkoani humu wamemtia nguvuni mfanyabiashara maarufu wa mjini Kyela anayedaiwa kuwalawiti watoto wa kiume wanaosoma katika Shule ya Msingi ya Kyela.
Hatua hiyo inakuja kufuatia malalamiko ya wazazi wa watoto hao kuwa Jeshi la Polisi limekuwa likimlinda mfanyabiashara huyo.
Hii ni mara ya tatu kwa mfanyabiashara huyo kukamatawa, kwani alishawahi kukamatwa mara mbili na kuachiliwa katika mazingira yasiyoeleweka.
Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo, (jina tunalo) kumekuja baada ya amri hiyo kutolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova, aliyetuma timu ya makachero wilayani humo.
Kamanda Kova alitoa amri hiyo siku moja baada ya gazeti hili kuripoti kuwa polisi wilayani humo wamekuwa wakisita kumkamata mfanyabiashara huyo anayetuhumiwa kufanya vitendo hivyo vya kinyama.
Mfanyabiashara huyo anatuhumiwa kuwalawiti wanafunzi wanne wa kiume wenye umri wa kati ya miaka 13 na 14 wanaosoma katika Shule ya Msingi ya Kyela iliyopo wilayani humo.
Akizungumzia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, Kamanda Kova alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, ambapo ataungana na wenzake watatu wanaotuhumiwa kwa makosa hayo.
Kova alisema awali watuhumiwa wengine watatu walitiwa mbaroni kutokana na tukio hilo, ambapo kulizuka malalamiko miongoni mwa wazazi na wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi juu ya kutokamatwa kwa mtuhumiwa ambaye inadaiwa ndiye mhusika mkuu wa makosa hayo.
Alisema kuwa mfanyabiashara huyo anadaiwa kuwalawiti wanafunzi wa kiume wa darasa la nne na sita katika shule hiyo kwenye nyumba ya kulala wageni ya Makete Half London iliyo jirani na eneo lake la biashara.
Kova alisema vitendo hivyo vinadaiwa kufanywa na mfanyabiashara huyo kati ya majira ya saa 8:00 mchana Januari 12 mwaka huu, Februari 5 saa 7:00 mchana na Februari 6 saa 9:00 alasiri katika nyumba hiyo ya kulala wageni na katika pagala la nyuma ya nyumba hiyo ya kulala wageni.
Alisema kutokana na mvutano baina ya Jeshi la Polisi na wazazi, alilazimika kumtuma Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Emanuel Kabwogi, kwenda Kyela na kikosi maalumu cha makachero, ambao walifuatilia tukio hilo kwa undani na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa.
Alisema mbali ya kumnasa mtuhumiwa huyo na wenzake, bado jeshi hilo linaendelea na upelelezi mkali na kila aliyehusika au kuguswa na tukio hilo atachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, Kova amewatoa hofu wazazi wa watoto wanaodaiwa kufanyiwa unyama huo kwamba wawe watulivu katika kipindi hiki wakati Jeshi la Polisi linafanya kazi yake