SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inatarajia kutumia sh bilioni 214.8 katika bajeti ya mwaka 2006/2007.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mambo ya Fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame, alipozungumza na waandishi wa habari.
Akifafanua, alisema sh bilioni 110.35 zinatarajiwa kutumika kwa matumizi ya kawaida na sh bilioni 104.44 kwa matumizi ya mandeleo.
Alisema kwamba pato la taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 6.2 kutoka asilimia 5.6 mwaka uliopita.
Waziri huyo alitamba kuwa bajeti hiyo imelenga kumkomboa mnyonge kutoka kwenye lindi la umaskini.
Alisema kwamba serikali haitapandisha kodi katika vyanzo vyake mbali mbali vya mapato, ili kufanikisha mpango wa serikali wa kupunguza mfumko wa bei za bidhaa mbali mbali.
“Serikali katika mwaka ujao wa fedha haikusudii kuongeza kodi katika vyanzo vya mapato, badala yake itaimarisha mkakati wa ukusanyaji mapato,” alisema Dk. Makame.
Alisema katika mwaka huu wa fedha kasi ya mfumko wa bei inatarajiwa kupungua kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.5
Dk. Makame alisema kutokana na kasi ya ukuaji wa uchumi, pato la taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 6.2, iwapo mipango mbali mbali ya maendeleo itafanikiwa kwa kushirikiana na wahisani.
Alisema Zanzibar ilikumbwa na misukosuko ya mfumko wa bei, hasa bei ya bidhaa za chakula na mafuta, ambapo mfumko wa bei ulifikia asilimia 9.7 kutoka asilimia 8.1 mwaka 2004.
Alisema serikali imepanga kukusanya mapato kutoka katika vyanzo vya ndani sh bilioni 83.17.
Katika bajeti hiyo, serikali inatarajia kutekeleza miradi ya maendeleo 39 na programu 13.
Dk. Makame alisema katika bajeti iliyopita sehemu kubwa ya mapato ya serikali ilikwenda katika ulipaji wa mishahara na uendeshaji wa shughuli mbalimbali na kupewa kipaumbele zaidi katika sekta za elimu, afya, mawasiliano, uchukuzi, ujenzi, maji, na kilimo.
Alisema serikali iliweza kukusanya asilimia 89.34 ya mapato yake katika kipindi cha Julai mwaka 2005 hadi Machi, mwaka huu, ikiwa ni kodi ya ushuru wa forodha na kodi ya mapato.
Wananchi wengi wanasubiri serikali itasema nini juu ya masilahi ya watumishi wa umma katika mwaka ujao wa fedha.
Katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar walipendekeza mshahara wa kima cha chini ufikie sh 100,000 kwa mwezi badala ya sh 50,000 za sasa.
Bajeti hiyo inatarajiwa kusomwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kesho, huku sekta ya biashara ikilalamikiwa kuwa imedorora kwa kiwango kikubwa Zanzibar .