NA NJUMAI NGOTA
SERIKALI imeandaa mkakati maalum wa kuwateketeza kunguru waliozagaa jijini Dar es Salaam, kuanzia wiki ijayo.
Mpango huo utatekelezwa kwa usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na kwamba lengo ni kupunguza kero zinasababishwa na kunguru hao.
Ofisa kutoka kitengo cha wanyamapori ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema mpango huo utafanyika baada ya kupata malalamiko mengi kutoka kwa wakazi wa jiji kuhusu kunguru hao.
Baadhi ya kero za kunguru hao ni kuchafua nguo zilizoanikwa, kupora maandazi, vifaranga vya kuku, bata, na wengine kushambulia watu wanaopanda kwenye miti yenye viota vyao.
Pia kunguru hao wameripotiwa mara kadhaa kubeba vijiko, nguo za ndani na kuchafua mazingira kwa kutoa vinyesi vingi maeneo wanayolala.
Kwa mara ya kwanza, kunguru wanaokera jijini Dar es Salaam waliletwa wachache kutoka Zanzibar kwa lengo la kula mizoga, lakini sasa wanakadiriwa kuwa karibu 600,000.
Ofisa Uhusiano wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Sheiba Lal alipoulizwa kuhusiana na mpango huo wa kuwaangamiza kunguru alikiri kuwepo, lakini hakutaka kuzungumzia zaidi suala hilo.
Sheiba alisema wizara inatarajia kutoa taarifa rasmi wiki ijayo wakati utekelezaji utakapoanza.
"Ni mapema mno kulizungumzia suala hili, wiki ijayo itatangazwa na gharama za mpango zitaelezwa,"alisema.