.Washindwa kumfikisha mahakamani
.Hatma ya dhamana yake bado kitendawili
Na Ester Bulaya
POLISI wamedaiwa kukwamisha kusikilizwa kwa ombi la dhamana dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ditopile Mzuzuri (58) anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia.
Hayo yalidaiwa na mawakili wanaomtetea mshitakiwa huyo, baada ya kushindikana kusikilizwa ombi hilo lililopangwa kusikilizwa jana katika Mahakama Kuu mbele ya Jaji Augustine Mwarija.
Akiongea baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, wakili Dk. Ringo Tenga, alidai hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya polisi na magereza kwa ajili ya kumpeleka mteja wao kusikiliza hatma ya kupata dhamana au kuendelea kusota rumande.
Tenga alidai walipowasiliana na magereza, walidai tayari walikwisha muandaa mteja wao na walikuwa wakisubiri polisi wa kwenda kumchukua gerezani na kumpeleka mahakamani.
Aliendelea kudai kuwa mahakama ilishatoa kibali cha kufuatwa Ditopile gerezani tangu juzi, lakini walishangaa kusikia polisi hawana taarifa hiyo.
"Hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya magereza na polisi, lakini kama kibali mahakama imetoa tangu jana (juzi), magereza nao wanasema wameshamuandaa wanasubiri askari, nao wanadai hawana taarifa... inatuchanganya sana, lakini ndiyo tumekwama mpaka kesho asubuhi," alisema.
Aliongeza kuwa: "Kiutaratibu watu wanaohusika kwenda kuwachukua na kuwarudisha mahabusu ni polisi na siyo magereza ambao kazi yao ni kuwapokea na kuwahifadhi.
Watu mbalimbali wakiwemo ndugu wa mshitakiwa, walifurika mahakamani hapo ili kushuhudia hatma ya Ditopile kama atapata dhamana na kurudi uraiani au ataendelea kusota rumande hadi siku ya hukumu.
Hivi karibuni, Ditopile alibadilishiwa shitaka na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) baada ya kusikiliza maelezo ya mashahidi waliokuwepo kwenye tukio, ambayo yatatumika katika ushahidi kesi hiyo itakaposikilizwa.
Ditopile alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Novemba 6, mwaka jana na kusomewa shitaka la mauaji ya Hassan Mbone (33) aliyekuwa dereva wa daladala, anadaiwa kufanya kosa hilo Novemba 4, mwaka jana, saa 1.30 usiku katika njia panda ya Kawe na Bagamoyo. Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa leo.