JESHI la Polisi mkoani hapa, limeingia katika mgogoro na wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Kyela, baada ya kumuachia mfanyabiashara mmoja anayedaiwa kuwalawiti watoto wa kiume wanaosoma katika shule hiyo.
Mgogoro huo umeibua chuki baina ya wazazi na Jeshi la Polisi, kwa kile kinachodaiwa na wazazi hao kuwa, baadhi ya viongozi wa jeshi hilo wanamlinda mfanyabiashara huyo licha ya kubainika kuwa anawalawiti wanafunzi.
Tanzania Daima, iliambiwa na wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo kwa nyakati tofauti kuwa, walibaini kuwepo kwa vitendo vya ulawiti dhidi ya watoto wa kiume wenye umri kati ya miaka 13 na 16, wakiwamo watoto yatima, miezi kadhaa iliyopita na kuamua kulifuatilia suala hilo mpaka walipothibitisha ukweli.
Kwamba katika uchunguzi wao walifanikiwa kugundua nyumba ya wageni iliyokuwa ikitumiwa na mfanyabiashara huyo kuwalawiti wanafunzi.
Walisema, baada ya kubainika ukweli dhidi ya tuhuma hizo, mfanyabiashara huyo alipelekwa polisi, lakini aliachiwa huru muda mfupi baadaye na polisi wakamkamata kinyozi mmoja ambaye majina yake yanafanana na mfanyabiashara mlawiti na kubambakiwa kesi hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda wa wiki mbili kuhusiana na mkasa huo ambao umevuta hisia za wakazi wa mji wa Kyela, umebaini kuwa hasira za wazazi wa watoto wanaodaiwa kulawitiwa na mfanyabiashara huyo ziliibuka baada ya makamanda wa polisi wa wilaya hiyo kumkingia kifua mfanyabiashara huyo na kisha kumtoa rumande alikokuwa akisubiri kupelekwa mahakamani.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi wilayani Kyela, vilieleza kuwa mfanyabiashara huyo anatoka kabila moja na viongozi wa juu wa jeshi hilo ngazi ya wilaya.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kyela, Mrakibu wa Polisi, Jeremia Mashoko, alikiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini alikataa kutoa ushirikiano kwa madai kuwa si msemaji wa jeshi.
Hata hivyo Kamanda Mashoko alisema kwamba, jalada la shauri hilo lipo kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleman Kova.
Alipoulizwa kwa njia ya simu, Kamanda Kova alishangazwa na taarifa hizo na kueleza kuwa hajui lolote kuhusiana na kesi hiyo.
Alitaka taarifa kutoka kwa Kamanda Mashoko, alielezwa kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), ambaye yuko safarini.
Mmoja wa wazazi wa watoto hao aliyezungumza na gazeti hili, George Kyamba, alithibitisha kuwa mtoto wake mwenye miaka 14, mwanafunzi wa darasa la sita ni miongoni mwa watoto waliolawitiwa na mfanyabiashara huyo.
Alisema watoto wao walipoitwa kwenye gwaride la utambulisho, ghafla walivamiwa na askari, wakachukuliwa na kwenda kufungiwa kwenye chumba ambako inadhaniwa kuwa walitishwa wasimtaje mfanyabiashara huyo.
Alisema ushahidi wa daktari aliyewafanyia uchunguzi watoto hao unathibitisha, watoto hao wameharibika sehemu ya haja kubwa kutokana na vitendo hivyo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kyela hakuweza kupatikana kuthibitisha taarifa hiyo, baada ya kuelezwa yuko safari nje ya wilaya hiyo.
“Kweli wanafunzi hao walifikishwa hospitalini hapa lakini kazi hiyo ilifanywa na DMO mwenyewe, na hivi sasa yupo safarini, yeye anajua alichokifanya kwa kuwa polisi ndio waliowaleta watoto hao wafanyiwe uchunguzi hapa,” alisema Kaimu Mganga Mkuu, Dk. Julius Sanga.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kyela, Lothi Kilanga, alieleza kuwa taarifa ya kuwalawiti wanafunzi shuleni kwake ilitolewa na mmoja wa wazazi aliyemtaja kwa jina la Robert Mwaseba.
Alisema Mwaseba aligundua kuwapo kwa vitendo hivyo baada ya kuona mabadiliko kwa mtoto wake pamoja na kumuona akiwa na fedha nyingi kila wakati, na alipombana alitoboa siri ya kulawitiwa na mfanyabiashara huyo.
Alisema, mtoto huyo alieleza kuwa fedha hizo wamekuwa wakipewa na watu wanaowapeleka kwenye nyumba ya kulala wageni na kwenye pagale ambako hulawitiwa na kupewa fedha kati ya sh 2,000 hadi sh 4,000 akiwa na wenzake.
Diwani wa Kata ya Kyela Mjini, Vicks Mahenge, naye alikiri kuwa na taarifa kuhusu tukio hilo na kwamba tayari baraza la kata (WDC) limekwisha kuketi na kulijadili ili kujua kiini cha watoto hao kuingiliwa kinyume cha maumbile na watu wazima, tena wenye ushawishi mkubwa kifedha.