LEO wananchi wa Ghana duniani kote pamoja na wapenda amani duniani wanasherehekea miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo na kuweka rekodi ya kuwa taifa la kwanza la weusi barani Afrika kujipatia uhuru kutoka kwa dola ya Kiingereza, iliyokuwa inaporomoka baada ya kuwa kinara wa dunia kabla ya kuibuka kwa Marekani na Urusi.
LEO wananchi wa Ghana duniani kote pamoja na wapenda amani duniani wanasherehekea miaka 50 ya uhuru wa taifa hilo na kuweka rekodi ya kuwa taifa la kwanza la weusi barani Afrika kujipatia uhuru kutoka kwa dola ya Kiingereza, iliyokuwa inaporomoka baada ya kuwa kinara wa dunia kabla ya kuibuka kwa Marekani na Urusi.
Pamoja na leo kuwa siku ya furaha hata hivyo, nchi hii haitegemei kuiadhimisha vyema kutokana na kugubikwa na tatizo kubwa la umeme lililoondokea kuwa sugu tangu miaka ya 1990 kama ilivyo kwa Tanzania.
Wakati tatizo la umeme upande wa Tanzania likianzia mapema miaka ya 90, nchini Ghana lilianzia mwishoni mwa miaka hiyo na hivi karibuni, Ghana imewekwa gizani huku huduma nyingi pamoja na biashara zikiathirika kwa kiasi kikubwa na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.
Kama ilivyo kwa Tanzania, matatizo ya umeme nchini humo yamesababishwa na kiwango kidogo cha maji katika chanzo kikuu cha umeme huku kukiwa hakuna vyanzo vingine mbadala kutokana na matatizo ya kifedha pamoja na kutokuwapo kwa mikakati imara ya muda mrefu ambayo pia serikali ya Tanzania imelaumiwa.
Ghana inategemea umeme unaozalishwa kutoka Bwawa la Volta huko Akosombo, ambako ndiko chimbuko kuu la umeme katika gridi ya taifa.
Bwawa la Volta ambalo linazalisha asilimia 60 ya mahitaji ya umeme, lilijengwa mwaka 1965 kwenye Mto Volta, linazalisha megawatts 912 za umeme na karibu megawatts 160 huko Kpong, bwawa dogo lililojengwa kilometa 25 chini ya mkondo wa mto.
Mamlaka husika zimedai kwamba kulega lega kwa uzalishaji wa umeme kumesababishwa na kiwango kidogo cha maji yanayotoka katika Mto Volta, ambao vyanzo vyake vitatu White Volta, Black Volta na Red Volta vipo Burkina Faso, ambako mvua haikunyesha ipasavyo.
Kutokana na hali hiyo, kina cha maji kimepungua chini ya wastani wa mita 72 zinazohitajika kuzalisha umeme.
Hata hivyo pamoja na matatizo hayo ya umeme, serikali tayari imeshanunua mitambo ya dharura ya kuzalisha umeme kutoka Marekani kutatua tatizo hilo kwa muda kabla ya kuangalia mkakati wa muda mrefu.
Ukiachia dosari hiyo, katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Ghana ina mengi ya kujivunia kwa sasa ukilinganisha na nchi nyingine za Kiafrika.
Ulikuwa usiku wa manane wa Machi 6, mwaka 1957 yaani nusu karne iliyopita, kengele za kanisani zililia katika jiji zima la Accra.
Bendera ya Uingereza ilishushwa taratibu nje ya kiwanja cha Bunge huku bendera ya taifa jipya ya rangi za kijani, dhahabu na nyekundu ikichukua nafasi.
Eneo si mbali kutoka hapo palipokuwapo mlingoti wenye bendera hiyo ya kikoloni, Kwame Nkrumah, baba wa Uafrika, alionekana akicheza kidogo na kutoa hotuba kali juu ya ndoto mpya, uhuru mpya na Afrika mpya.
Uhuru wa Ghana ulikuwa ishara ya matumaini kwa bara zima, na ukawa mwanzo mpya ambao waziri mkuu wa Uingereza wakati huo, Harold Macmillan, alikuja kuuita ‘upepo wa mabadiliko’.
Kweli upepo huo uliendelea kuvuma na kugeuka kuwa kimbunga ama tufani iliyokuja kusambaratisha ukoloni katika bara zima.
Baada ya hapo Ghana ilipitia katika kile kilichoitwa siasa ya usoshalisti, udikteta wa majenerali, soko huria la walafi kabla ya kuibuka na matumaini mapya yanayoshuhudia ikipata mafanikio kwa kadiri ya muda unavyokwenda.
Katika miaka ya 1950 ilikuwa Ghana ikijulikana kama Gold Coast (Dhahabu ya Pwani) kutokana na uzalishaji wake mkubwa wa dhahabu.
Ghana ilianguka vibaya kipindi cha miongo mitano kutokana na mfumo usioelewaka wa usoshalisti, ubepari wa kiliberali, maingilio ya jeshi hatimaye Ghana ikaibuka, uchumi wake ukikua taratibu katika kile ambacho Patrick Smith, mhariri wa jarida la Africa Confidential, anakihesabu kuwa moja ya nchi zenye mfumo imara wa vyama vingi barani Afrika.
Ni safari ndefu, wakati ukipata uhuru, Ghana ilikuwa na utajiri mkubwa wa mali asili, miuondombinu hai, mfumo bora wa elimu na sekta imara ya utumishi na akiba ya kigeni ya dola milioni 481.
Uchumi wake ulikuwa sawa na wa Korea Kusini au Malaysia.
Iwapo utalinganisha nchi hizi na Ghana kati ya mwaka 1957 na sasa utaona Ghana imerudi nyuma,” anasema Patrick Smith.
Wakati jua likianza kuziwakia nchi zilizokuwa zikitawaliwa na falme za kikoloni barani Afrika na Asia katika miaka ya 1960, hakukuwa na mtu aliyekuwa na wasiwasi na Afrika.
Wasiwasi zaidi ulielekezwa barani Asia. Nchi karibu zote za Afrika zilikuwa zimebarikiwa kwa utajiri mkubwa wa madini na eneo bora na kubwa la kilimo.
Asia, kwa mfano ilikuwa na matatizo pamoja na idadi kubwa ya watu kulinganisha na uwezo wake katika kuwalisha au kuwahudumia. Miongo mitano baadaye, Afrika ndio bara masikini zaidi duniani. Nusu ya watu wake wanaishi chini ya dola moja kwa siku.
Wastani wa kuishi unazidi kuanguka, watu wakiishi wastani wa miaka 46. Asia, imeipiga kumbo Afrika kinyume na ilivyotarajiwa, pengine kutokana na sababu zikiwamo; wakoloni hawakuigawa sana Asia kikabila kama walivyofanya Afrika; mifumo ya utawala ya Asia kwa mfano India ililenga uboreshaji serikali; Katika Afrika walilenga katika kupora na kuuza nje malighafi nje ya nchi yao. Katika Asia, jiografia katika sekta ya bahari ilikuwa nafuu kiusafirishaji.
Ilikuwa rahisi kusambaza bidhaa na teknolojia. Kwa mfano, kulikuwa na wimbi la ukuaji wa maendeleo na uchumi Japan. Nchi za Asia zilitilia mkazo katika uwekezaji wa elimu na sekta ya afya kwa nguvu kazi zao.
Nchini Ghana, rais wa kwanza wa taifa la kisasa la Ghana, alikuwa kiongozi mahiri na mpinzani mkubwa wa ukoloni, Kwame Nkrumah. Kwa miaka 10 akiwa madarakani, Mwanaideolojia huyu wa Kiafrika alianzisha mikakati mingi ya kiuchumi. Aliwekeza katika miradi lukuki mikubwa mikubwa ikiwamo Bwawa la Akosombo ambalo lipo katika Ziwa Volta, ziwa kubwa zaidi duniani lililotengenezwa na binadamu.
Lakini kupitia bwawa hilo lililo tegemeo la kuzalisha umeme, halikuwasaidia ipasavyo watu waishio eneo husika.
Nkrumah alitilia mkazo mageuzi ya kisiasa na kiuchumi akijaribu kuongeza uzalishaji kupitia vyama vya ushirika.
Pia alianzisha magereza ambayo aliyatumia kuwafunga wapinzani wake wa kisiasa bila kuwafungulia mashitaka pamoja na kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Na aliweka kodi kubwa katika nchi hii iliyokuwa katika ushindani wa sekta ya viwanda na mzalishaji mkubwa ya kakao.
Pamoja na kuheshimika wakati huo na hadi sasa, kwa kiasi fulani miongoni mwa wanaharakati weusi huku akiwa na ndoto ya kuifanya Afrika kuwa huru na moja, Nkurumah anaelezwa kuwa aliendekeza ukiukaji wa haki za binadamu, rushwa, na kuubomoa uchumi wa nchi.
Hakukuwa na maombolezo makubwa wakati alipong’olewa madarakani katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) mwaka 1966.
Lakini hata hivyo hata mapinduzi hayo hayakuleta matokeo yaliyotarajiwa. Mapinduzi baada ya mapinduzi yalikuwa kama ada, huku yakimuingiza jenerali mmoja baada ya mwingine kuwa rais.
Hatimaye Ghana iliondokana na mazoea ya kutawaliwa na majenerali mwaka 1981 wakati mapinduzi mengine yalipomwingiza Luteni wa jeshi la anga, Jerry Rawlings, ambaye aliposhika usukani wa nchi alivipiga marufuku vyama vya siasa. Ilikuwa shughuli pevu.
Mamia ya watu walihamishwa kutoka jela usiku na hawakusikika tena. Mwaka 1982, majaji watatu na ofisa mstaafu wa jeshi walitekwa na kuuawa kikatili. Lakini ikijulikana, Rawlings aliingia kama simba aliyejeruhiwa na kuonyesha makucha yake, alikuja kugeuka kuwa mwanakondoo mwema.
Baada ya kubadili dini kuwa Mkristo, aliondokana na uvaaji wa magwanda ya kijeshi na kutinga na suti na alianzisha katiba mpya, akiurudisha mfumo wa vyama vingi vya siasa, na kuitisha uchaguzi wa rais mwaka 1992. Rawlings aliwania na kushinda katika uchaguzi huo kama ilivyokuwa tena mwaka 1996.
Lakini wakati muhula wake wa urais madarakani ulipofikia tamati, kwa mastaajabu ya wengi, aliiheshimu katiba aliyoiweka mwenyewe na kuondoka madarakani.
Wala hakulituma jeshi liingilie kati wakati mtu aliyetaka amrithi madarakani aliposhindwa katika uchaguzi na John Kufuor, ambaye kwa sasa yuko katika awamu ya pili na ya mwisho.
“Sifa zinapaswa zimwendee Rawlings,’’ anasema Richard Dowden, mkurugenzi wa taasisi ya Royal African Society.
“Aliinusuru Ghana kuingia kaburini. Na ijapokuwa aliingia madarakani akiwa na mawazo ya Kimarxist, haraka haraka aliachana nayo wakati alipoujua ukweli wa demokrasia kisiasa.
“Inakuwa vigumu kwa Waghana kujua nini kilichowavuruga kiasi hicho huko nyuma kwa kutawaliwa na vurugu,” anasema Patrick Smith. Mgawanyiko wa kisiasa nchini Ghana daima umechangiwa na tofauti ya kimawazo kati ya wa mrengo wa kushoto na kulia na si tofauti ya kiukoo au kikabila. Na pia inawahusisha wasomi wa daraja la kati,” anasema.
Waghana tangu enzi za ukoloni wamekuwa wakipata elimu nzuri. Lakini hili liliboreshwa zaidi kipindi cha Rais Kufuor. Katika muongo uliopita alitumia kati ya asilimia 28 na 40 ya bajeti ya Ghana katika elimu kwa mwaka.
“Kingine, mtaji wa kiuchumi wa Ghana ni watu wake,” anasema Smith. Mashirika ya kimataifa ya kiraia yamejaa Waghana huku Kofi Annan, ambaye hadi hivi karibuni alikuwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) akiwa kinara wa watumishi hao. Taasisi za Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Tume ya Uchumi ya UN-Afrika na Umoja wa Afrika (AU), nafasi nyeti za juu zimekuwa zikishikwa na Waghana kuliko nchi nyingine yoyote ya Afrika.
“Pia utawakuta madaktari wa Ghana wakiwa wametapakaa Marekani, Ulaya, India, Pakistan, na Saudi Arabia, na hivyo kuifaidisha nchi kutokana na fedha wanazotuma nyumbani,” anasema Smith.
Hata hivyo kutapakaa kwa wataalamu hao nje ya nchi wanaokenda kutafuta malisho bora kumekuwa mkuki mkali kwa Ghana na Afrika kwa ujumla. Afrika hupoteza wastani wa wataalamu 70,000 kila mwaka wanaokwenda katika nchi zilizoendelea na hivyo kupata hasara kubwa ya kusomesha wengine na wakati huo huo ikikabiliwa na upungufu.
Mbaya zaidi, nchi za Afrika zilizojaribu kuwasomesha wataalamu wengine kuziba pengo hilo, zilijikuta zikikwama baada ya kulazimishwa kuondoa bajeti ya mpango huo mwishoni mwa miaka ya 1970 na mwanzoni mwa miaka 1990 kwa amri ya Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) na Benki ya Dunia (WB).
Ni WB ndiyo iliyomtaka Rawlings afukuze nusu ya watumishi wake katika sekta mbalimbali za umma na kusababisha wengi wakimbilie ng’ambo na kuibua uhaba wa wataalamu wa daraja la wasomi.
Kwa kufuata masharti ya WB, Ghana ilinufaika kwa kupewa msamaha wa madeni, thamani ambayo hailingani hata kidogo na wataalamu hao. Lakini ukilinganisha na sera za IMF, hazikusaidia sana kuboresha ukuaji wa uchumi wala kipato cha Waghana kiuchumi.
Viwanda vilivyotamba katika miaka ya 1970 wakati sekta hiyo ilipokuwa ikikua kwa kasi na kuweza kuzalisha vitu vyake yenyewe kama vile vitanda, vyandarua, dawa za mbu, kamba na vinginevyo, kwa sasa vitu hivyo vinaagizwa kutoka India na China na hata dawa na magari madogo yaliyokuwa yakitengenezwa nchini humo yametokomea.
“Baada ya kuanguka kwa sekta hizo, kwa mara nyingine dhahabu na kakao inategemewa kiuchumi,” mhariri huyo wa Africa Confidential anasema. Utegemezi wa sekta ya aina moja huifanya nchi ishindwe kuendelea vyema. Bei ya bidhaa za Afrika nje ya bara inanunuliwa kwa kiwango cha chini, mara nne ya kulinganisha na za nchi zilizoendelea.
Utiliaji mkazo elimu sasa umeanza kuonyesha matumaini. Ghana sasa ina sekta ya habari ya mawasiliano inayokua pamoja na sekta ya huduma mbalimbali. Sekta hizo sasa zinawakilisha asilimia 25 ya uchumi wa taifa ambao unaendelea kukua sambamba na kilimo ambacho kinawakilisha asilimia 40 ya pato la taifa huku zikiajiri asilimia 60 ya nguvu kazi na wastani wa kuishi ukiwa umepanda kufikia miaka 58 kwa sasa.
Waghana, Patrick Smith anasema wamekosa sekta imara ya ujasiriamali.“Serikali haijafanya juhudi za kutosha katika sekta hii, pamoja na kwamba serikali si ya kifisadi,” anasema.
Kwa mujibu wa taasisi huru ya kimataifa ya kupambana na rushwa, (Transparency International) kwa kweli, Ghana iko katika nusu ya kwanza ya nchi zisizoendekeza rushwa, ikiwa ni moja ya nchi bora barani Afrika. Nchi zenye nguvu kiuchumi katika sekta ya biashara barani Afrika, Nigeria na Kenya, zina mfumo wa kisiasa uliokithiri kwa rushwa.
Bado kuna jingine la kufurahisha, anasema Myles Wickstead, ambaye aliongoza Kamishina ya Afrika.“Ghana imepitia katika mchakato wa kisiasa na imetulia sasa na rais wake anaheshimika sana kimataifa kama ilivyoonyesha wakati alipokalia uenyekiti wa AU hivi karibuni.
Mchakato wa tathminni wa Afrika umeonyesha kwamba Ghana imefikia mahali pazuri na watu wake wamekomaa pamoja na kuwa na malengo mazuri kwa ajili ya hali ya baadaye ya nchi yao.