Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Al Qaeda sasa wamsaka mtoto wa Princess Diana
Al Qaeda sasa wamsaka mtoto wa Princess Diana
By Habari Tanzania | Published  03/6/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

GENGE la Al Qaeda nchini Iraq, limeanza kujiandaa kumteka na baadaye kumuua, mjukuu wa Malkia Elizabeth, Mei mwaka huu, wakati atakapokuwa nchini humo kwa mazoezi ya kijeshi.

Wataalamu wa masuala ya kigaidi wa nchini Uingereza wamekaririwa na gazeti maarufu la udaku nchini humo, The Sun,wakisema wamenasa taarifa za siri kuhusu mpango huo katika mitandao kadhaa ya kigaidi.

Prince Harry (22), mtoto wa Prince Charles na Princess Diana, ambaye hivi sasa yuko katika mafunzo ya kijeshi, anatarajia kwenda nchini Iraq kwa ajili ya mazoezi makali ya kijeshi yatayohusisha mafunzo ya utekaji nyara.

Mtaalamu wa masuala ya kigaidi, Neil Doyle, ameonya kuhusu vikosi vya kigaidi nchini Iraq, kumsubiri kwa hamu mwana ukoo huyo wa kifalme.

Katika mafunzo yanayofanyika wiki hii, kabla hata ya kwenda Iraq miezi miwili ijayo, Harry na wenzake kutoka kikosi cha Blues and Royals watafundishwa mbinu za kupambana na watekaji wa Al-Qaeda nchini Iraq.

Tayari wakuu wa usalama nchini Uingereza wameshaanza kuchukua tahadhari kuhusu kuwapo kwa uwezekano wa Harry kutekwa, jambo ambalo linaweza likawa ni pigo kubwa kwa Uingereza na harakati zake za kukabiliana na ugaidi iwapo ataonyweshwa kwenye televisheni akiwa mateka au ameuawa.

Harry, ambaye yuko katika nafasi ya tatu katika urithi wa ukoo wa kifalme pamoja na askari wake 12, watapokea mafunzo baada ya tovuti zinazomuunga mkono kiongozi wa Kiislamu mwenye msimamo mkali, Omar Bakri, kutoa vitishio dhidi yake.

Moja ya vitisho hivyo ni ujumbe uliosomeka: “Prince Harry atapelekwa Iraq kuuawa na Waislamu.”

Ujumbe mwingine ulisomeka: “Mungu mwenye enzi atampatia kile anachostahili kama ilivyokuwa kwa makafiri wenzake.”

Na tovuti nyingine ijiitayo ‘Resistance4Islam’ iliongeza: “Bila shaka anajitakia kifo.”

Harry atakwenda Iraq ambako hadi hivi sasa askari zaidi ya 100 wa Uingereza wameshauawa na atakuwa katika Jimbo la Maysan, eneo la hatari, ambalo hadi hivi sasa askari wa nchi hiyo 23 wameshauawa katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliyopita.

Pamoja na hatari na vitisho hivyo, taarifa zinaeleza kuwa, Harry, kijana matata ambaye wakati fulani alivaa nguo yenye alama ya manazi wa Ujerumani, amedhamiria kutimiza ndoto yake kwenda kufanya doria huko Iraq.

Katika mji wa Majar al-Kabir, askari wa kikosi cha Red Caps walichinjwa na genge la wanamgambo Juni 2003. Mwaka mmoja baadaye katika mji mkuu wa jimbo hilo, Al Amarah, dereva shujaa, Johnson Beharry, alituzwa tuzo ya Victoria Cross, ikiwa ya kwanza katika kipindi cha miaka 22 baada ya kuokoa kikosi chake cha 30 kutokana na kuzima jaribio la uendeshaji wa shambulio la kushtukiza.

Askari wa Uingereza katika eneo hilo la Maysan wamekuwa wakipambana kwa miezi kadhaa na Waislamu wa Shia wanaoungwa mkono na Iran, ambao wanamtii kiongozi wa madhehebu hayo nchini humo, Muqtada al-Sadr.

Chanzo cha juu cha habari cha kijeshi kilisema hivi karibuni kwamba: “Harry’ anaingia katika eneo hatari la Maysan.” Lakini hakuna wa kumzuia kutokana na uamuzi wake.

Wakiwa kama askari wa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano, vikosi vya Prince Harry vya Blues na Royals vitafanya mazoezi hayo ya kujilinda baada ya usiku wa wiki iliyopita kusafirishwa kutoka kambi yao iliyopo Windsor, Berks, kwenda kambi ya kijeshi ya Bodney iliyo karibu na Msitu wa Thetford huko Norfolk.

Kipindi cha siku chache zijazo, watafanya mazoezi huku askari kutoka vikosi vingine wakijifanya kuwa wapiganaji wa adui walio katika hali na mazingira ya Kiiraq.

Ukanda huo wa mazoezi uko Ireland Kaskazini, ambako ulikuwa maalumu kwa ajili ya kupambana na machafuko ya nchini humo na sasa umefanyiwa marekebisho kuendana na mazingira ya Iraq.

Wakuu wa jeshi wamebuni mazingira ambayo Harry na wenzake watashikiliwa mateka ndani ya jengo lililopo eneo hilo.

Waokoaji nao wataendesha operesheni ya kujibu mapigo kwa lengo la kumuokoa. Kambi hiyo ambayo mazingira yake Harry na askari wake watakutana nayo nchini Iraq, ina maeneo madogo madogo yaliyojengwa na vijumba vidogo dogo nje ya jengo ambavyo vinatoa sura halisi ya eneo la adui.

Kwa mujibu wa mkakati huo, mchakato wa mafunzo hayo pamoja na mambo mengine unamuandaa Harry aonekane akifanya doria katika eneo lenye uwezekano wa kutekwa akiwa katika gari la kijeshi nchini ‘Iraq’.

Askari kutoka kikosi kingine watacheza kama magaidi wenye silaha wanaomkamata Harry na kumchukua mateka kwenda kwenye jengo dogo karibu na ukanda huo.

Hata hivyo kikosi cha Harry kitalazimika kulipua jengo hilo katika operesheni ya uokoaji, wakitumia mbinu ya kumchukua mateka ambaye kwa kawaida huvishwa kitambaa chekundu.

Aidha, Harry na kikosi chake watafundishwa na kuboreshwa ujuzi wao katika kuyaepuka mashambulio ya kushtukiza na mabomu ya kutegwa barabarani.

Vyanzo vya habari kutoka vikosi vya Blues na Royals vilisema: “Pamoja na kwamba Harry anatendewa kama askari mwingine yeyote, havingependa kuona akiangukia mikononi mwa adui, kwa sababu hakuna ubishi iwapo ataangukia huko matokeo yatakuwa mabaya kabisa na ushindi mkubwa kwa magaidi.

Mtaalamu wa ugaidi Doyle alisema: “Harry anaweza kuonekana kuwa zawadi kwa makundi hayo ya wana mgambo wenye msimamo mkali ambaye kukamatwa kwake litakuwa tukio kubwa na la kushangiliwa kwao.”

Uamuzi wa kumpeleka Iraq ulitangazwa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Jenerali Sir Richard Dannatt, baada ya kushauriana na Malkia Elizabeth pamoja na baba yake, Prince Charles.

Prince Harry amepewa jukumu la kawaida la kuongoza kikosi chake cha ukomando. Hata hivyo kuna taarifa kuwa, wakuu wa jeshi watafanya mpango wa siri bila Harry mwenyewe kujua, ambao ni kumuandalia kikosi kitakachomfuatilia kwa karibu ili iwapo lolote litamtokea waweze kumuokoa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Tony Blair alimsifu Harry akisema: “Ni kijana shupavu, anayetaka kuwa sehemu ya kikosi na jeshi. Hilo linaonyesha jinsi alivyo na sifa za kipekee.”

Baba yake mdogo, Prince Andrew alipokuwa na umri wa miaka 22 pia alijiunga katika vita ya Falklands mwaka 1982, akipigana dhidi ya Agentina.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.