Na Kizitto Noya
SERIKALI itaendelea kupiga marufuku biashara za kimachinga mitaani na kuwataka wafanyabiashara hao kwenda katika maeneo yaliyotengwa na kujiunga na vikundi vya biashara ili wapewe mikopo ya kuendeleza biashara zao.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Kandoro alisema mwishoni mwa wiki kuwa biashara za mitaani hazina tija wala mwanga wa maendeleo na zinawafanya wafanyabiashara hao kuendelea kuwa maskini siku zote.
"Mtu anazunguka kutwa nzima na soksi mbili, vitambaa vitatu vya mikononi na maji katuni moja. Hapa atakuwa na maendeleo gani?" alihoji Kandoro.
Kandoro alisema kuwa mpango wa serikali wa kuwataka machinga waende katika maeneo waliyopangiwa umelenga kuwasaidia wafanyabiashara hao kujikomboa na umaskini badala ya kuwaangamiza kama inavyofikiriwa na baadhi ya watu.
Kwa mujibu wa Kandoro, mtu anayetetea machinga waendelee kufanya biashara katika mitaa ya kati kati ya jiji hawatakii mema wafanyabiashara hao kwani kwa kukaa huko hakuna namna serikali ikawafahamu na kuwapa mikopo.
Alisema serikali sasa imekamilisha makubaliano na benki mbalimbali kutoa mikopo kwa wafanyabiashara hao kwa riba nafuu kwa lengo la kuwawezesha kuendeleza mitaji yao na kuondoka na umaskini.
"Wewe ukishabikia machinga abaki barabarani humsaidii, huuangalii hatma yake ya miaka kumi ijayo. Leo anatembea barabarani kwa kuwa ana nguvu akizeeka ataishi vipi?" alihoji Kandoro.
Alisema kwa mujibu wa nadharia ya uchumi, uchumi endelevu unatokana na shughuli za uzalishaji mali tofauti na kazi za kimachinga zinazofanywa bila jitihada za kuzalisha bidhaa zingine. Alisema Machinga wanatakiwa kujifunza kuzalisha mali na kuiendeleza badala ya kutembeza mali iliyokwishazalishwa ili kujiletea maendeleo endelevu