WATAALAMU wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Tanga, jana waligundua bomu katika ghala la kuhifadhia vyuma chakavu linalomilikiwa na mfanyabiashara mmoja jijini hapa.
Bomu hilo ambalo limepelekwa katika vikosi vya JWTZ kwa ajili ya kuchunguzwa, liligundundulika kwenye ghala la Gharib Ally Saidi, lililopo Kitongoji cha Mwazange. Saidi aliwaambia waandishi wa habari kuwa alipoliona bomu hilo, alilitilia mashaka ingawa aliogopa kuripoti polisi akihofia kukamatwa.
“Nilikuwa nimelitenganisha ma vyuma vingine chakavu baada ya kulitilia mashaka kutokana na umbo lake kuwa la ajabu ajabu,” alisema Saidi.
Alisema alijaribu kuwauliza watu mbalimbali ambapo moja wapo aliyejitambulisha kwake kuwa ni mwanajeshi alimwelezwa kuwa bomu hilo limekwisha muda wake.
Hata hivyo baada ya mfanyabiashara huyo kubaini kuwa ni bomu, alitoa taarifa polisi ambao walipolichunguza na kubaini kuwa ni bomu waliwataarifu JWTZ na wataalamu wake waliamua kulichukua.
Akizungumza mara baada ya kufika katika tukio hilo, mtaalamu kutegua mabomu kutoka JWTZ Sajenti Christian Heliyogere, alisema bado wanachunguza bomu hilo ni la aina gani na limetengenezwa nchi gani.
Baadhi ya Wafanyabishara wa chama chakavu waliozungumza na Mwananchi, walipongeza Jeshi la Polisi pamoja na JWTZ kwa kufika haraka kwenye ghala hilo na pia kuonyesha ushirikiano mkubwa katika kuliondoa.
Waliliomba jeshi hilo kuangalia uwezekano wa kuwapatia vifaa vinavyoweza kubaini kuwepo kwa mabomu katika shehena za vyuma wakati gari zinapoingiza mizigo katika maghala.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi nchini limeanzisha kampeni maalum ya kuelimisha wafanyabiashara wanaonunua na kuuza vyuma chakavu ili waweze kuyatambua mabomu.
Katika kampeni hiyo ambayo wataalamu wa Jeshi la polisi wanatembelea maeneo mbalimbali ambayo yanauzwa vyuma chakavu Jijini hapa na kuwaelimisha wafanyabiashara umuhimu wa kuchunguza vyuma wanavyonunua.