Na Mwandishi Wetu
MAREKANI imesema imefurahishwa na hatua ya Tanzania kupeleka majeshi yake kudumisha amani katika nchi zenye machafuko na imeahidi kuipa misaada mbalimbali ya kijeshi ikiwamo mafunzo ili kujiimarisha zaidi.
Naibu Kamanda wa Majeshi ya Marekani Ulaya, Williams Ward, alimwambia Rais Kikwete juzi alipokutana naye Ikulu jijini Dar es Salaam, kuwa Marekani imeandaa sera maalum kuisadia Tanzania kuimarisha majeshi yake kwa lengo la kuiwezesha kuendeleza sera yake ya kudumisha amani.
"Marekani imetusifia sana kwamba pamoja na uchanga wetu katika mambo ya kijeshi, tumeweza kuwa mstari wa mbele kudumisha amani katika nchi zenye machafuko na ujio huo ni wa mazungumzo ya kushirikiana nao katika masuala ya kijeshi," alisema Rais Kikwete baada ya kuondoka Naibu Kamanda huyo.
Alisema Marekani imepanga kuimarisha uhusiano wake na Tanzania, hasa katika mambo ya kijeshi kwa lengo la kutoa fursa kwa majeshi ya nchi hizo mbili kubadilishana uzoefu na mbinu mbalimbali za kijeshi.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, pamoja na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizofikia mafanikio makubwa katika masuala ya kijeshi, bado inahitaji kujifunza kutoka wataalam wa nchi zingine ili kuweza kujiimarisha zaidi.
"Elimu haina mwisho, wenzetu wanatusifia kwamba tunafanya vizuri katika majeshi yetu, lakini bado tunahitaji wataalam wa kufundisha mbinu zaidi ya kijeshi," alisema Kikwete na kuongeza.
"Hii ni katika kuheshimu sheria za jeshi kwamba katika kipindi ambacho mwanajeshi hayupo vitani, anatakiwa kujiandaa kwa vita kwa mazoezi siku zote."
Hivi karibuni Tanzania ilipeleka wanajeshi 80 kulinda amani katika nchi ya Lebabon wakishirikiana na wanajeshi wengine kutoka Umoja wa Mataifa. Tanzania pia imekuwa mstari wa mbele kushiriki katika ulinzi wa amani katika nchi zenye machafuko barani Afrika.