Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Polisi sasa wamuanika mbunge Msomi feki
Polisi sasa wamuanika mbunge Msomi feki
By Habari Tanzania | Published  03/4/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Charles Mullinda

HATIMAYE, Jeshi la Polisi nchini, limetamka rasmi kuwa Mbunge wa Buchosa, Samuel Chitalilo (CCM), alighushi vyeti vya elimu yake na aliwadanganya wapiga kura wake.

Limesema, uchunguzi wa kina lilioufanya, umethibitisha pasipo shaka kwamba, Chitalilo hakusoma Uganda, wala jina lake halitambuliki katika Shule ya Sekondari Katikamu, anayodai kusoma, pamoja na kwenye Baraza la Mitihani la nchi hiyo.

Mkurugenzi Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, aliiambia Tanzania Daima kwa njia ya simu jana kuwa, wamethibitisha Chitalilo ni miongoni mwa wanasiasa wengi waongo, lakini hawezi kushitakiwa kwa sababu elimu si kigezo cha mtu kuwa mbunge.

Alisema polisi walikamilisha uchunguzi wa suala hilo tangu mwaka jana na kulipeka kwa DPP kwa ajili ya hatua zaidi dhidi ya Chitalilo, hata hivyo DPP alilirudisha faili hilo kwa DCI kwa maelekezo kuwa mbunge huyo hana kosa linaloweza kumtia hatiani.

“Ni kweli, uchunguzi wetu umebaini kuwa Chitalilo alisema uongo, alighushi vyeti vyake, hakusoma Uganda, jina lake halipo katika hiyo shule wala katika Baraza la Mitihani la Uganda, lakini ubunge haukuwekewa sifa ya elimu.

“Sisi tulikamilisha uchunguzi wetu mapema tu, tangu mwaka jana, tukapeleka jalada kwa DDP, yeye akatafakari, akaona kisheria hakuna kosa, hawezi kushitakiwa, hivyo akalirudisha faili kwetu kwa maelekezo mengine,” alisema Manumba.

Alisema hatua ilifikiwa kutokana na ukweli kwamba wanasiasa wengi ni waongo, kwamba huwa wanatoa ahadi nyingi kwa wapiga kura wao, lakini hawazitekelezi, hivyo Chitalilo, naye anawekwa katika kundi la wanasiasa wa aina hiyo.

Kamanda Manumba alisema vyombo pekee vilivyobaki, vyenye uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya Chitalilo, ni chama chake cha CCM pamoja na taasisi anayoitumikia (Bunge).

Alisema, polisi imekwishafanya mawasiliano ya ndani na vyombo vinavyohusika na viko huru kuchukua hatua yoyote dhidi ya Chitalilo kulingana na taratibu zilizojiwekea.

Manumba alisema CCM ni chama chenye taratibu zake, hivyo wanaweza kuchukua hatua zinazofaa kwa mbunge huyo kama wataona inafaa na Bunge kadhalika nalo lina kanuni na taratibu zake, hivyo Spika anaweza kuchukua uamuzi unaofaa kama itaona inapaswa kufanya hivyo.

Kuhusu wapiga kura wa Buchosa, Manumba alisema polisi wamefanya kazi yao na wameeleza ukweli, hivyo ni jukumu lao kuamua, baada ya kubaini kuwa mbunge wao si mkweli, kutomchagua tena ama kumchagua tena kama wanampenda.

Tanzania Daima ilipowasiliana na Spika wa Bunge, Samuel Sitta kwa njia ya simu jana, simu yake ilikuwa inaita bila majibu, na Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, simu yake ilikuwa haipatikani.

Madai ya Chitalilo kughushi vyeti vya elimu yake na kuwadanganya wapiga kura wake, yaliibuliwa na mshindani wake kisiasa, Alfred Ngotezi, ambaye alifungua kesi polisi Januari 21, 2006 mjini Sengerema Mwanza.

Kesi hiyo ilipewa namba SEN/IR/104/2006 na katika madai yake, Ngotezi alieleza kuwa, Chitalilo aliwadanganya wapiga kura na vyombo vya dola kuhusu elimu yake wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na 2000.

Alidai kwamba, wakati wa uchaguzi mkuu, Chitalilo alitoa vipeperushi akieleza kuwa yeye ni mhitimu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Katikamu nchini Uganda mwaka 1991, na kwamba alihitimu na kutunukiwa stashahada kutoka Manchester Uingereza mwaka 2003, ingawa hakutaja jina la chuo husika.

Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, ambaye aliwahi kuzungumzia kesi hiyo kwa nyakati tofauti katika vyombo vya habari, alikaririwa na gazeti hili akieleza kuwa jarida la kesi hiyo linafanyiwa upelelezi na makachero wa polisi wa makao makuu kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa (Interpol).

Mwapachu alikaririwa kwamba amewaagiza polisi kulishughulikia suala hilo haraka na apatiwe taarifa ambazo aliahidi kuziweka hadharani.

Naye Spika Sitta alilizungumzia suala hilo. Alisema kughushi ni kosa la jinai hivyo kama ikibainika kuna mbunge aliyeghushi, sheria itachukua mkondo wake.

Katika hatua ya kushangaza, wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa Sengerema na Buchosa, Sebastian Masso wakati akitoa maamuzi kuhusu pingamizi la mgombea wa NCCR-Mageuzi, Adrian Tizeba alilomuwekea Chitalilo, alisema baada ya kufuatilia madai ya utata wa elimu ya Chitalilo, ameridhika kuwa anayo elimu aliyoijaza kwenye fomu namba 10B (5).

Hata hivyo uamuzi huo wa Masso unapingana na taarifa za upelelezi uliofanywa na polisi kuhusu suala hilo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Ras_Twin)
    Rating
    Ni aibu kama mtu mwenye dhamana ya kuiwakilisha serikali anaweza kuachwa na serikali aendelee na ubunge licha ya uongo mkuu alioutoa na ambao ndio umemuwezesha kupata nafasi hiyo. Sina hakika mtu huyo alipokula kiapo kugombea na kuwa mbunge alisema nini na serikali inasemaje juu ya mtu anayesema uongo chini ya kiapo. Kama hakuna sheria ya kumtia hatiani na iwekwe sasa maana upo uwezekano mkubwa kuwa wananchi wa jimbo lake walimchagua wakiamini upeo wake kulingana na elimu aliyonayo unaweza kumsaidia kuwafikisha watakako. Na hata huyo Msimamizi wa Uchaguzi wa jimb hilo atoe maelezo ya uchunguzi wake na ukionekana kuwa wa "zimamoti" naye achukuliwe hatua. Inasikitisa saana kuona wananchi wanakoseshwa haki yao kwa rushwa za watu na ubovu wa mfumo wa utawala wa sheria.
    RAS_TWIN
     
  • Comment #2 (Posted by Anonymous)
    Rating
    Its true there's no qualification or degree to be an MP anywhere in the world lakini most MP''s ninavyojua mimi in foreign countries especially UK most of them hold a degree and it doesn't have to be in Politics.I'm suprised kwamba they haven't taken any actions against him maana kughushi vyeti is an criminal offence.I know this man Samwel Chitalilo very well in infact hajamaliza hata darasa la saba ameishia la sita.He doesn't have any type of qualifications whether certificate/diploma na English yake ni aibu tupu utafikiri sio mbunge.Hata Kiswahili chake utajua tu hajasoma.Kazi yak ni kujaza mimba wasichana kwa kuwadanganya atawaoa.Huyu mtu ana watoto 5 kutoka wanawake tofauti kila kona ya Tanzania hata nje ya nchi.Its sad kwanba viongozi wetu badala ya set a good example to citizens lakini ndio hivyo.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.