WATOTO wawili wa miaka tisa na 11, raia wa China, wamefanikiwa kupanda mlima Kilimanjaro hadi kileleni. Mlima wa Kilimanjaro una urefu wa mita 5,895, imefahamika. Watoto hao ndugu ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi, Zhang Muyuan(9) na Zhang Muyao(11), waliupanda mlima huo Februari 22 mwaka huu wakiwa na kundi la watu wazima.
Kwa mujibu wa gazeti moja mjini Beijing, watoto hao wamevunja rekodi ya kuwa watoto wadogo kuweza kuupanda mlima huo wakimzidi mtoto wa miaka 12 wa Kimarekani aliyewahi kufika kileleni mwa mlima huo.
Kabla ya kuupanda mlima Kilimanjaro, watoto hao waliupanda mlima Siguniang uliopo nchini China wenye urefu wa mita 5,025. Muyao alisema wamekuwa wakifanya mazoezi ya kupanda kwenye barafu iliyo ngumu. Kwa sasa wanajiandaa kuupanda mlima Jaya ambao pia ni mrefu. Muyao aliwaeleza waandishi wa habari kuwa baada ya kufanikiwa kufika kileleni, alianguka na kufikiria angefariki dunia. Hata hivyo kundi la watu wazima aliofuatana nao walimuokoa.
Hata hivyo wakazi wa China wamepinga kitendo cha mtoto huyo wa miaka tisa kuupanda mlima Kilimanjaro. Mwalimu wa jimbo la Zhejiang, Lin Weiping aliandika barua katika gazeti moja la jioni, liitwalo Yangte akilalamika mtoto huyo kuwekwa katika hatari hiyo ya kupoteza maisha na kuhoji nani aliyetoa taarifa za uongo za mtoto huyo ili aruhusiwe kuupanda mlima huo.
Habari za gazeti hilo zimeripoti kuwa taratibu zilizowekwa kwa wapandaji mlima huo kuwa hairuhusiwi mtoto wa chini ya miaka 10 kupanda mlima. Muyuan anatimiza miaka 10 Aprili mwaka huu. Wakati wa kupanda mlima huo alidanganya umri wake.
Afisa Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa(TANAPA), Catherine Mmbena alisema umri wa chini wa kupanda mlima Kilimanjaro ni miaka 16. Hata hivyo, hakuwa na maelezo juu ya watoto hao kuweza kupanda mlima huo.