Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Fomu za siri, si siri tena
Fomu za siri, si siri tena
By Habari Tanzania | Published  03/4/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
  • Zafungiwa maandazi mitaani

    FOMU za siri za maelezo binafsi ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne za uchaguzi wa michepuo ya masomo ya kidato cha tano pamoja na vyuo vya elimu ya juu maarufu ‘Sel form’, zimezagaa mitaani.

    HabariLeo Jumapili imefanikiwa kuzipata fomu hizo za siri zikiwa zimetengenezwa mifuko na nyingine zikitumiwa kufungia bidhaa mbalimbali vikiwemo vitafunwa anuai kama vitumbua, chapati na maandazi.

    Fomu hizo pia zimezagaa katika maduka ya vipodozi na mahitaji ya kila siku, huku wateja wakihifadhiwa bidhaa mbalimbali wanazonunua katika maduka hayo. Maduka yanayoongoza kuwa na mifuko ya fomu hizo ni yaliyopo maeneo ya Mwenge, Temeke, Kariakoo na Posta.

    Fomu hizo zilizoandikwa F4-SEL pamoja na mwaka husika, zimepatikana zikionyesha zilitumika miaka mitatu tofauti kuanzia mwaka 1999 hadi 2001. Mifuko pamoja na fomu zenyewe zinaonyesha maelezo yote yaliyojazwa na mwanafunzi husika kuanzia picha yake ikiwa imepigwa muhuri wa shule anayosoma, michepuo na shule alizochagua, shule anayosoma pamoja na matokeo ya maendeleo yake ya masomo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

    Pia inaonyesha nambari yamtihani, nambari ya kituo, umri, vyuo vya elimu ya juu alivyochagua mwanafunzi husika pamoja na saini ya mwalimu mkuu na jinsi alivyomtathmini mwanafunzi.

    Kwa upande wa kumtathmini mwanafunzi, zinaonyesha wazi jinsi mwalimu mkuu alivyoonyesha uwezo wa mwanafunzi wake na michepuo na vyuo vya elimu ya juu anavyopaswa kuchaguliwa mwanafunzi huyo.

    Miongoni mwa fomu ambazo HabariLeo Jumapili imezipata, ni za wanafunzi waliomaliza Shule za Sekondari za Mpwapwa mkoani Dodoma, Rwegarulila, Jangwani na Shule ya Wasichana ya St. Francis za Dar es Salaam. Fomu hizo hujazwa na wanafunzi wanaokuwa katika hatua za mwisho za kumaliza kidato cha nne na shule husika inaziwasilisha Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi, kwa ajili ya kutumika wakati wa uchaguzi wa wanafunzi baada ya kupatikana kwa matokeo ya kidato cha nne.

    Kila mwanafunzi wa Tanzania Bara na wakimbizi wanaotambuliwa na serikali, hutakiwa kujaza fomu hizo siku chache kabla au baada ya kumaliza mtihani wa kidato cha nne. Baada ya muda kadhaa uliopangwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupita, fomu hizo zinatakiwa kuteketezwa kwa kuchomwa ili mtu mwingine asizipate.

    “Ni kweli fomu hizi tunajua zinaibwa na walinzi waliowekwa kulinda sehemu zilipohifadhiwa na hii yote inatokana na uzembe wa Wizara kutozichoma kwa haraka kama inavyotakiwa… …Wizi huu ni wa muda mrefu na hata maofisa wa hapa Elimu ya Sekondari wanafahamu, lakini hawaoni tatizo”, alisema mmoja wa wafanyakazi wa wizara ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake kwa hofu ya kukosa kibarua.

    Inadaiwa wahusika wa wizi wa fomu hizo, wanazipeleka kwa wateja maalum wanaotengeneza mifuko ambao nao wanaiuza mifuko sehemu mbalimbali za jijini Dar es Salaam. Mfuko mmoja huuzwa sh. 25 kwa wafanyabiashara, huku wanaoiba karatasi hizo wizarani huziuza kwa bei ya maelewano kwa watengenezaji mifuko.

    Akizungumzia hali hiyo, Afisa Elimu Kiongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ricky Mpama alishangaa kuelezwa na mwandishi wa gazeti hili juu ya kupatikana kwa fomu hizo. “Hizo fomu ni confid ntial (siri), sijui imekuwaje watu wameweza kuzipata, lazima kuna sehemu kumefanyika uzembe lakini naomba tuwasiliane Jumatatu (kesho) ili niweze kufuatilia zaidi kwa sasa siwezi kujua kilichotokea na nipo safarini”, alisema Mpama.

    Mpama alisema kwa kawaida fomu hizo zinasimamiwa na kuhifadhiwa na Idara ya Elimu ya Sekondari ambao wanapaswa kuzificha ili mtu mwingine asiweze kuzifikia. Serikali imekuwa mara zote ikisisitiza usiri wa nyaraka zisizotakiwa kuzagaa mitaani, lakini inaonekana msukumo wa kudhibiti haujawekewa mkazo zaidi.

  • How would you rate the quality of this article?
    1 2 3 4 5
    Poor Excellent
    Add comment
    Comments


    Article Options
    Your Favorite Articles
    View All Favorites
    Articles to Read
    You Recently Viewed...
    Popular Articles
    1. Unaifahamu Jambo Forums?
    2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
    3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
    4. Is Tanzania a safe place to invest?
    5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
    No popular articles found.
    Popular Authors
    1. Habari Tanzania
    2. Mzee Mwanakijiji
    3. Marshy Abdu
    4. Linda Garner
    5. Nthelezi Nesaa
    6. Prosper Kwigize
    7. Ramadhan Semtawa
    8. Salehe Mmoro
    9. Manyerere Jackton
    10. Ndesanjo Macha
    No popular authors found.