Kivumbi cha mjadala wa bajeti ya Serikali ya 2006/07 iliyowasilishwa wiki iliyopita, kimetimka leo Bungeni baada ya waheshimiwa kuanza kuichambua kama karanga.
Pamoja na hotuba ya bajeti, pia waheshimiwa hao waliojifua tangu Ijumaa iliyopita wamejadili ile ya mwelekeo wa uchumi.
Hotuba ya bajeti iliwasilishwa na Waziri wa Fedha, Bi. Zakia Meghji wakati ile ya mipango ilisomwa na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa.
Katika kuonyesha kuwa waheshimiwa wabunge wamepania kutoa dukuduku lao kama walivyotumwa na wananchi kuwawakilisha bungeni, tayari wabunge 70 wameshatuma maombi kwa Sipika wa Bunge hilo Bw. Samwel Sitta wakiomba wapewe nafasi ya kuchangia.
Pamoja na wabunge wengi kuipokea bajeti hiyo, kuna maeneo ambayo wawakilishi hao wameapa kuwaweka kati Mawaziri husika hadi watoe maelezo ya kueleweka.
Miongoni mwa maeneo ambayo wabunge wameonyesha kutokuridhishwa nayo ni pamoja na kuwapo kwa ongezeko la ushuru wa muda wa maongezi kwa simu za mkononi.
Wakati Waziri wa Fedha akiwasilisha hotuba yake, baada ya kusoma eneo hilo la nyongeza ya ushuru kwa mawasiliano, ilisikika miguno kutoka kwa wabunge, kitu kinachoonyesha hawakukubaliana naye.
Aidha baadhi ya wanasiasa hasa kutoka upinzani wameonyesha wasiwasi wao wakidai kuwa bajeti hiyo ni kiini macho.
Kwa mfano, chama cha Chadema katika taarifa yake kimedai kuwa bajeti hiyo haijalenga kumkomboa Mtanzania masikini hususani wa kijijini kama ilivyoahidiwa katika ilani ya CCM ya mwaka 2005.
Bajeti imeshindwa kuainisha masuala ya msingi ambayo kama yangezingatiwa yangeweza kutatua matatizo mengi ya msingi. Na hii imetokana na ukweli kuwa bajeti haikuwa na dira ambayo kimsingi ndio ungekuwa muongozo, chama hicho kikasema.
Kimesema bajeti hiyo inakosa mwongozo, na dira na kwamba imeandaliwa kwa kuzingatia agenda tatu tofauti (MKUKUTA, Ilani ya CCM, MDGS na Dira ya taifa) ambavyo vyote hazikufanyiwa upembezi yakinifu na kuzifanya kuwa dira moja.
Aidha chama hicho kimesema kwa vile ahadi ya Serikali ni kuboresha kilimo ili kupanua ajira, kuondoa njaa na kupunguza umaskini wa kipato kwa Watanzania, utekelezaji wa wazo hilo kibajeti ulitakiwa kuonekana.
Aidha chama hicho kinasema hoja ya serikali kuwa mambo mengi ya Wizara ya Kilimo yatashughulikiwa na Wizara ya Miundombinu haionyeshi ukweli wa kiutekelezaji kwa sababu, Wizara ya Miundombinu kwa sasa inabeba mzigo mkubwa wa mawasiliano na ujenzi na mbaya zaidi hata yenyewe imeporomoka kutoka 12.4% hadi 11%, kikasema chama hicho.
’’Lazima Serikali ikiri kuwa imedhamiria kuua kilimo ambacho kinachangia zaidi kuliko sekta yoyote katika pato la taifa (44%) na hivyo Watanzania ambao kwa kiasi kikubwa ni wakulima wategemee maumivu,’’ chama hicho kikadai.