INAWEZEKANA kusema, pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Petro Atletico ya Angola, ni hofu tupu kwani kila moja ina hofu dhidi ya mwenzake.
Kadiri siku zinavyosogea, ndivyo joto la pambano hilo litakalopigwa Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, linavyozidi kupanda.
Wakati Yanga ikipiga marufuku wapenzi na mashabiki kuhudhuria mazoezi yake kwa hofu ya kupelelezwa, hadi kufikia jana, taarifa za kuwasili kwa Atletico, zilikuwa siri.
Licha ya Shirikisho la Sola la Angola kuthibitisha ujio wa timu hiyo, si Yanga wala Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walio na taarifa rasmi ya kuwasili kwa wageni hao.
Florian Kaijage, ambaye ni Ofisa Habari wa TFF, alisema hadi jana mchana, walikuwa hawana taarifa za kuwasili kwa timu hiyo, licha ya kuelezwa itafika.
“Tumewasiliana na viongozi wa soka Angola, wamethibitisha kuja kwa timu hiyo, lakini hawakuwa tayari kusema ni lini na msafara wa watu wangapi,” alisema Kaijage.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa timu zote mbili, waamuzi wa mechi hiyo ya Jumapili kutoka Msumbiji, walitarajiwa kuwasili jana jioni.
Mwamuzi wa kati ni Justino Faduco huku wasaidizi wakiwa ni Henriques Langa na Edmundo Xavie Macamo.
Viingilio vya mechi hiyo ni sh 15,000 kwa Jukwaa Kuu, sh 8,000 kwa Jukwaa la Kijani na sh 3,000 Mzunguko.
Ikicheza nyumbani, Yanga inalazimika kupata ushindi mnono kabla ya matokeo ya mechi ya marudiano itakayopigwa wiki mbili baadaye mjini Luanda, Angola.