UAMUZI wa Kanisa Anglikana duniani kuwapa miezi saba wenzao wa Marekani kuacha kukumbatia tabia za kishoga ndani ya kanisa hilo, umeanza kulitikisa taifa hilo kubwa ambalo liko katika hatari ya kuondolewa katika umoja wa madhehebu hayo.
Mtikisiko huo tayari umeonyesha kumgusa Askofu shoga aliyesababisha mtafaruku mkubwa tangu alipowekwa wakfu mwaka 2003, Gene Robinson na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo nchini humo, Askofu mwanamke, Katherine Jefferts Schori.
Katika mkutano wake uliofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwezi Februari, Kanisa Anglikana lilitangaza rasmi kupiga marufuku kuwekwa wakfu kwa maaskofu mashoga.
Sambamba na hilo, kanisa hilo liliyapa miezi saba, hadi Septemba 30 mwaka huu, makanisa ya Marekani na kwingineko duniani, yanaounga mkono ushoga kutubu na kuacha kushabikia vitendo hivyo ambavyo lilivieleza bayana kuwa ni kinyume cha mafundisho ya Biblia.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kufikiwa kwa Azimio la Dar es Salaam lililotangaza rasmi kuwakataa mashoga ndani ya kanisa hilo, Robinson, mmoja wa maaskofu wenye ushawishi mkubwa nchini Marekani, alieleza kushangazwa na uamuzi huo.
Robinson ambaye ni Askofu wa Jimbo la Hampshire, amekaririwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, akilitaka kanisa hilo duniani kuacha kujadili masuala ya ushoga na badala yake kuyafanyia kazi maandiko ya Injili.
Msimamo huo wa Robinson ndiyo ambao umekuwa ukitolewa na viongozi wengi wa kanisa hilo nchini Marekani, tangu maaskofu wa kanisa hilo walipotoa tamko lao hilo jijini Dar es Salaam, siku chache zilizopita.
Naye Askofu Mkuu Schori, ambaye ameendelea kuunga mkono suala la ushoga kutambulika ndani ya kanisa hilo, alisema ingawa bado mawazo yake hayajabadilika katika kutetea suala hilo, aliwataka waumini wenzake kuacha kulipigania jambo hilo ‘japo kwa sasa.’
“Kuishi pamoja ndani ya jumuiya ya Kikristo, ina maana kila mtu atilie maanani mahitaji na umuhimu wa mwingine kwa makini.
“Kama tutapunguza hulka na silka katika kipindi hiki cha malumbano ya ushoga, basi tutakuwa tumepata mbinu ya kumaliza tatizo hilo na kuwa kitu kimoja bila kugawanyika,” alisisitiza Schori.
Alisema kuwa, endapo suala la ushoga litachukua sura mpya ndani ya kanisa hilo, kuna hatari ya kanisa hilo la Marekani kutengwa katika ushirika wa Anglikana wapatao milioni 77 duniani kote.
Kanisa hilo lilianza kupata misukosuko baada ya Askofu Robinson kujitangaza hadharani kuwa ni shoga aliposimikwa mwaka 2003 kuwa Askofu wa Kanisa la Marekani.