JUZI, Kamati ya Dawa ya Mkoa wa Dar es Salaam ilitoa taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu ukaguzi iliyoufanya katika maduka yanayouza dawa za binadamu katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Takwimu zilizotolewa na kamati hiyo ambazo ziliripotiwa katika vyombo vya habari juzi na jana zinaonyesha mambo ambayo kimsingi yanapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka.
Kamati hiyo, iliyokuwa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro ilitoa matokeo ambayo kwa kiwango kikubwa yanaonyesha hatari kubwa wanayokabiliwa nayo wakazi wengi wa Dar es Salaam, jiji linalokadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni tatu.
Kandoro katika taarifa yake hiyo alisema kwamba, ukaguzi wao, ulibaini kuwa asilimia 99 ya maduka yote yaliyokaguliwa katika kipindi cha mwaka 2005/06 yalikutwa yakiwa na kasoro nyingi za kisheria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kamati ya Kandoro, maduka hayo yalikutwa yakiuza dawa halisi au bandia ambazo ubora na usalama wake ulikuwa haujahakikiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Kamati hiyo iliyofanya ukaguzi katika jumla ya maduka 1,217 ilibaini pia kwamba, asilimia 95 ya maduka hayo hayakuwa na wauzaji wenye sifa za kufanya kazi hizo za uuzaji.
Kama hiyo haitoshi, ukaguzi huo ulibainisha pia kwamba, asilimia 54 ya maduka hayo yalikutwa yakiendesha biashara hiyo tete kwa maisha ya binadamu pasipo kuwa na vibali vya kufanya hivyo.
Katika mazingira ya hatari kabisa, maduka 18 kati ya hayo yalikutwa yakiwa yanatoa huduma za tiba pamoja na kukutwa na vifaa vya hospitali kama vile vifaa vya kutolea mimba na vya kufanyia tohara.
Mambo hayo yote ni nje ya yale maduka yanayofikia asilimia 43 ambayo wamiliki wake waliamua kuendesha shughuli zao katika majengo ambayo hayakidhi matakwa ya kitaalamu.
Hitimisho la matokeo ya kamati hiyo lilikuwa ni kwamba, matokeo yalikuwa yakidhihirisha kuwapo kwa ongezeko kubwa la ukiukwaji wa sheria unaofanywa na wamiliki wa maduka hayo.
Aidha, kamati hiyo ilisema bayana kwamba, matokeo hayo yalikuwa yakionyesha athari za kiafya ambazo watumiaji wa huduma zitolewazo katika maduka haya wanaweza kukabiliana nazo.
Athari zilizotajwa na kamati hiyo ni pamoja na kuweka usugu wa vimelea vya maradhi katika mwili kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa kupitia wauzaji wasio na taaluma.
Si hilo tu, athari nyingine ni maambukizi ya magonjwa kama UKIMWI yanayoweza kusambaa kutokana na kutumiwa kwa vifaa visivyo salama kama sindano na visu vya upasuaji.
Matokeo hayo kwa maelezo yoyote yale yanaonyesha namna rushwa katika taifa hili ilivyofika katika hatua ya kuanza kugusa afya za wananchi wake moja kwa moja.
Tunasema hivyo tukiamini kabisa kwamba, watu wanaofungua biashara ya dawa za binadamu wanafanya hivyo katika maeneo yenye uongozi na wanatakiwa si tu kuwa na kibali ya TFDA bali leseni nyingine za biashara ambazo kimsingi hutolewa baada ya taratibu kadhaa kufanywa.
Lakini pia, wale ambao walifikia hatua ya kukutwa na vifaa kama vile vya kutolea mimba wanathibitisha jambo moja kwamba, shughuli hiyo batili hufanywa katika mazingira ya hatari yanayowaweka mabinti wadogo katika usalama mdogo kabisa kimaisha.
Kwa sababu hiyo basi, tunapenda kuipongeza kamati kwa kazi ngumu na nzuri iliyofanya, na wakati huo huo kuziasa taasisi mbambali za umma kama TAKURU, TRA, TFDA na nyingine kuchukua hatua za mara moja kukabiliana na hatari za namna hiyo kitaifa na si Dar es Salaam pekee. Sote tunapaswa kutambua kuwa maisha ni bora kuliko kingine chochote.