SAKATA la kukwama kwa usajili wa gari la zimamoto la Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, limechukua sura mpya baada ya uongozi wa manispaa hiyo, kuwatuhumu baadhi ya watendaji wa Wizara ya Miundombinu kwa mchezo mchafu.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka Manispaa ya Temeke, vimeieleza Tanzania Daima kuwa, tayari uongozi wa juu wa manispaa hiyo umekwishajipanga kukabiliana na mbinu zinazofanywa na maofisa wa Wizara ya Miundombinu, kukwamisha usajili huo.
Habari zimeeleza kuwa, kukwama kwa usajili wa gari hilo, ni mpango wa kuikomoa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, baada ya watendaji wake kukataa kutekeleza matakwa ya maofisa wa Wizara ya Miundombinu katika usajili wa gari hilo.
Wizara ya Miundombinu imekataa kulisajili gari hilo kwa maelezo kuwa halina ‘Manufactural Warrant’ ya kuthibitisha kama ni jipya na imeishauri manispaa hiyo ikubali kulisajili kama mtumba.
Manispaa ya Temeke imeukataa ushauri wa wizara, na imeitaka iandikie barua ya kuonyesha kuwa gari hilo si jipya, ili ichukue hatua za kisheria dhidi ya wakala wake.
Ofisa mmoja wa idara ya utawala ya Manispaa ya Temeke aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini, alisema ‘Manufactural Warrant’ ilikwishapelekwa wizarani, lakini maofisa wa wizara hiyo wanaikataa bila sababu za msingi.
“Hili gari ni jipya kabisa, lina ‘Manufactural Warrant’ na tumeishaipeleka wizarani, lakini cha ajabu wanaikataa, wanasema siyo yenyewe, sasa mkurugenzi amewataka watuandikie kuwa hilo gari si jipya ili achukue hatua za kisheria dhidi ya wakala wa gari hili,” alisema ofisa huyo.
Alisema tayari wakala wa gari hilo amekwisha kutaarifiwa kuhusu madai kuwa gari hilo, aina ya Benz si jipya. Lakini wakala huyo anaelezwa kushitushwa na madai ya wizara na anakusudia kuishitaki kwa kumuharibia soko.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Idd Nyundo aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa, anashangazwa na madai ya wizara kwa sababu ukaguzi wa awali uliofanywa na watalaamu ulionyesha kuwa gari hilo ni jipya.
“Mara ya kwanza alikuja fundi kutoka wizarani, akalikagua gari, akaridhika kuwa ni jipya, wakaagiza mtu wa zimamoto nae aje akague, akaja akathibitisha kuwa ni jipya, tukawa tunasubiri usajili, ikawa kimya, sasa tunaambiwa si jipya, hatujui wanataka nini, inashangaza!” alisema Nyundo.
Nyundo alithibitisha kuwa ameitumia wizara barua ya kutaka ithibitishe kwa maandishi kama gari lililonunuliwa na manispaa yake ni mtumba ili achukue hatua za kisheria dhidi ya wakala wa gari hilo.
Hata hivyo, mpaka juzi maofisa wa Wizara ya Miundombinu walikuwa wakisisitiza kuwa hawajapokea ‘Manufactural Warrant’ kutoka Manispaa ya Temeke kama walivyoagiza, bali kilichowasilishwa ni Warrant Guarantee ya vipuri.
Habari kutoka Idara ya Mitambo na Umeme ya Wizara ya Miundombinu zinaeleza kuwa Warrant Guarantee haitoshi kuthibitisha kama gari ni jipya.
Zinasema watendaji wa Manispaa ya Temeke, waliohusika na ununuaji wa gari hilo wanajaribu kuficha ukweli na walitegemea wizara haitakuwa makini katika ukaguzi, hivyo wakaamua kutumia njia zisizo halali katika usajili wa gari hilo.
“Mara ya mwisho, walichokileta hapa ni Warrant Guarantee ya vipuri, si ya gari, tukawakatalia, wakaomba muda zaidi ili wakaitafute, tangu walipoondoka hawajarudi tena.
“Gari la mtumba na jipya ni tofauti, hilo lililonunuliwa na Temeke, halifiki sh milioni 300, na cha kushangaza, inawezekanaje watu watumie miezi miwili kutafuta ‘Manufactural Warrant’, hata kama waliliagiza Ujerumani lilikotengezwa gari hilo, ingeshafika, hapo kuna usanii, kuna pesa imeliwa,” alisema ofisa huyo.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa gari hilo lilinuliwa kwa sh 333, 375, 651.
Hii si mara ya kwanza kwa watendaji wa serikali na serikali za mitaa kutofautiana katika utekelezaji wa majukumu.
Katika Manispaa ya Kinondoni, mvutano wa kiwanja ilipojengwa baa marufu ya Rose Garden imeibua ufa mkubwa baina ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Baraza la madiwani wa manispaa hiyo.
Wakati madiwani wakisisitiza kuwa baa hiyo imejengwa kinyume cha sheria, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli, ana msimamo tofauti kuwa baa hiyo iko pale kihalali, na anayetaka kuivunja, aandae mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kulipa fidia.