Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wapelelezi wa rada waja kuinoa TAKURU
Wapelelezi wa rada waja kuinoa TAKURU
By Habari Tanzania | Published  03/1/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu, Oslo, Norway

KITENGO cha Kupambana na Rushwa cha Serikali ya Uingereza (SFO), kinajiandaa kuja nchini kuipa mafunzo ya kukabiliana na makosa ya ufisadi, Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU).

Wataalamu wa SFO wanakuja nchini wakati wakiendelea kufanya uchunguzi dhidi ya Kampuni ya vifaa vya kijeshi ya BAE System ya nchini humo kwa tuhuma za kula rushwa na kuiuzia Tanzania rada chakavu kwa bei ya juu kuliko ilivyostahili.

Kuja huko kwa maoafisa wa SFO, moja ya taasisi zinazoheshimika sana nchini Uingereza kulibainishwa juzi na Rais Jakaya Kikwete wakati akifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Norway, Jens Stoltenberg.

Kikwete alisema, maofisa hao wa SFO wanakuja nchini baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair kukubali ombi la Kikwete la kuitaka nchi hiyo ije kuisaidia TAKURU katika vita yake dhidi ya rushwa.

“Nilipokuwa ziarani Uingereza, katika mazungumzo yangu na Waziri Mkuu Tony Blair, nilimwomba atusaidie kuiwezesha taasisi yetu kupamba na rushwa kwa kuwapatia mafunzo ya kitaalamu watendaji wake. Blair alikubali ombi langu,” alisema Rais Kikwete akimweleza Stoltenberg.

Alisema, tayari Mkurugenzi Mkuu wa TAKURU, Edward Hosea, yuko Uingereza alikokwenda kukutana na watendaji wa SFO kwa lengo la kujadiliana na kupanga programu za mafunzo hayo.

SFO inaichunguza BAE System inayotuhumiwa kulipa kwa siri kamisheni ya dola milioni 12 kwenda katika akaunti moja ya Mtanzania iliyoko Uswisi, fedha zinazoonekana kuwa nyingi na ambazo zinahusishwa na mgawanyo unaoweza kuwagusa maofisa wa kampuni hiyo ya usambazaji silaha.

Kinara wa kashfa hii kwa upande wa Tanzania, ambaye kwa muda mrefu anatajwa kuwa na uhusiano wa masuala ya kijeshi na viongozi wa serikali, amekiri kwamba kiwango hicho cha fedha kilihamishiwa katika akaunti yake iliyoko Uswisi.

Malipo hayo yanayoonekana kufanywa kwa mlango wa nyuma, yanawakilisha asilimia 30 ya thamani ya mkataba mzima, jambo linaloongeza shaka ya kuwapo kwa vitendo vya ufisadi.

Wakati hivi sasa akionekana kuwa tayari kuisaidia Tanzania, mwaka 2002 Blair aliunga mkono kwa nguvu, mauzo hayo ya rada, mbali ya aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa katika serikali yake Clare Short na Waziri wa Fedha, Gordon Brown, kupinga.

SFO, ambayo hivi karibuni ililazimishwa kuachana na uchunguzi wa malipo ya kamisheni ya ununuzi wa silaha yaliyofanywa kati ya BAE na Saudi Arabia, kwa sasa imeapa kufa na suala la Tanzania.

Kwa upande wa Tanzania, wafanyabiashara wanaotajwa katika sakata hilo la rada ni Sailesh Vithlani na mshirika wake, Tanil Somaiya.

Vithlani pia anatajwa kuwa mtu ambaye mwaka 2000 alihusika pia katika ununuzi wa ndege ya Rais iliyogharimu dola za Marekani milioni 40, ambayo kama ilivyo kwa rada, ni moja ya mambo yaliyolalamikiwa kuhusishwa na vitendo vya rushwa.

Akizungumza juzi, Kikwete ambaye mara kadhaa amelazimika kujibu tuhuma zinazohusiana na sakta hilo la rada, alisema kuwa ili TAKURU iweze kutekeleza majukumu yake kisayansi na kwa kulingana na hali ya sasa, inahitaji uwezeshwaji mkubwa wa vifaa na mafunzo.

Rais Kikwete pia alisema wakati TAKURU itakapoanza kufanya kazi chini ya sheria mpya ya rushwa, si yeye wala kiongozi mwingine yeyote atakayeingilia utendaji wake wa kazi.

“Napenda nikuhakikishieni kwamba, mimi binafsi na serikali yangu, tunayo dhamira ya dhati ya kukabiliana na tatizo la rushwa. Moja ya hatua nilizochukua ni pamoja na kuipatia TAKURU sheria itakayoipa nguvu na mamlaka kutekeleza majukumu yake bila woga na bila ya kuingiliwa na mtu yeyote. Hata mimi mwenyewe sitawaingilia katika utendaji wa kazi zao,” alisema Kikwete.

Kikwete alitoa ahadi hiyo miezi kadhaa baada ya Serikali nyingine ya nchi za Scandinavia ya Denmark mwishoni mwa mwaka jana kutangaza uamuzi wa kupunguza msaada wake wa sh bilioni 4.1 sawa na asilimia 20 ya fedha zake za msaada katika bajeti kuu kutokana na kile ilichokieleza kuwa ni kucheleweshwa kwa sheria mpya kukabiliana na vitendo vya ufisadi.

Hata hivyo siku chache tu baada ya uamuzi huo wa Denmark, serikali iliwasilisha rasimu ya muswada huo kwa wadau ambao unatarajiwa kujadiliwa katika kikao cha mwezi ujao cha Bunge.

Iwapo muswada huo utakuwa sheria, basi TAKURU itaongezewa meno na kuwa na uwanja mpana zaidi wa kukabiliana na vitendo vya rushwa ambavyo chini ya Sheria Namba 16 ya Mwaka 1971 ilikuwa haiwezi kuvitimiza.

Muswada huo pamoja na mambo mengine, utaiwezesha TAKURU kuwafilisi viongozi na watumishi wa umma watakaotiwa hatiani kwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi.

Chini ya sheria hiyo, PCB itapewa mamlaka ya kufungua kesi ya daawa (civil case) kuomba mahakama itoe amri ya kumfilisi kiongozi au mtumishi atakayetiwa hatiani katika kesi ya jinai.

Kutokana na sheria hiyo mpya, kitaundwa chombo kitakachojulikana kama Bodi ya Taifa ya Kuzuia Rushwa ambayo kazi yake itakuwa kuishauri TAKURU katika utendaji wake wa kila siku.

Mbali ya hayo, sheria hiyo pia itaiwezesha TAKURU kumchunguza na kumfikisha mahakamani kiongozi au mtumishi wa umma anayeishi maisha ya anasa tofauti na kipato chake.

Mtumishi wa namna hiyo atatakiwa kutoa maelezo na vielelezo kuthibitisha namna alivyopata mali hizo kutokana na kipato chake kinachotambulika.

Sheria hiyo pia, ambayo itagusa hata katika taasisi binafsi, itajumuisha rushwa ya ngono kuwa miongoni mwa vitendo vya ufisadi ambavyo vitamweka hatiani mtuhumiwa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.